*************************************
Na John Walter-Manyara
Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa wilaya ya Kiteto mkoa wa Manyara ,imefanikiwa kurejesha mahindi gunia 45 katika kijiji cha Loltepes.
Mkuu wa TAKUKURU wilaya ya Kiteto Venance Sangawe amesema mahindi hayo ni sehemu ya gunia 90 ambazo Takukuru iliingilia kati kurejesha.
Sangawe amesema diwani wa kata ya Sunya aliemaliza muda wake, Musa Brayton na mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi katika kata hiyo Abdi Puputo walishindwa kutimiza masharti waliyokubaliana na kijiji ya kulipa mahindi hayo baada ya kulima shamba la kijiji ekari tisini.
Ameongeza kuwa makubaliano kati ya watu hao na kijiji ilikuwa ni kulipa gunia moja kwa kila ekari tangu mwaka 2017 hivyo kwa kushindwa kufanya hivyo Takukuru imeamua kuisaidia kijiji kurejesha mahindi hayo.
Akikabidhi mahindi hayo kwa mwenyekiti wa kijiji cha Loltepes Mkuu wa wilaya ya Kiteto Tumaini Magessa, amewataka viongozi wa kijiji na shule kuhakikisha mahindi hayo yanatumika kwa ajili ya chakula cha wanafunzi wa shule za Loltepes na Loiborsoit zilizopo katika kijiji hicho.
Huo ni mwendelezo wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa mkoa wa Manyara katika kurejesha na kukabidhi mali kwa wahusika halali ili kuondoa migogoro isiyokuwa ya lazima.