Mkurugenzi wa Utawala na rasilimali Watu Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw. Victor Katagere akizungumza na Watumishi wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka DART katika Kikao kazi cha taasisi zilizoko chini ya Wizara yake Kwenye Ofisi za Wakala Ubungo Maji Jijini Dar es Salaam Julai mosi 2020.Mtendaji Mkuu wa DART Ronald Lwakatare akitoa maelezo ya utangulizi kwa Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw. Victor Kategere kabla ya kuzungumza na Watumishi wa Wakala Jijini Dar es Salaam Julai mosi 2020.
*********************************
Na. Mwandishi Wetu, DART.
Watumishi wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), wametakiwa kufanya kazi kwa bidii, weledi na kujituma ili kufanikisha ndoto za Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli za kuwa na Tanzania mpya.
Maagizo hayo yametolewa Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw.Victor Kategere, alipozungumza na Watumishi wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kwenye kikao kazi cha kukumbushana majukumu ya utendaji kwa watumishi wa umma wa taasisi zilizoko chini ya Wizara hiyo.
Amesema DART ni taasisi muhimu sana ambayo inategemewa katika kupunguza changamoto za msongamano na foleni katika Jiji la Dar es Salaam, hivyo ni wajibu wa watumishi kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa.
“Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam zaidi ya milioni 6 wote wanawatazama na wanamatarajio makubwa sana kwenu katika kuwapatia huduma ili hatimaye shughuli zao za maendeleo zirahisishwe, hivyo uwepo wetu katika taasisi hii na Serikali kwa ujumla ni wa maana” Alisema Kategere.
Aidha aliwaasa watumishi kuendelea kufuata Sheria Kanuni na taratibu zote za utumishi wa umma, hasa suala la kutunza na kuhifadhi siri za Serikali kwani kumejitokeza baadhi ya watumishi wasio waaminifu ambao wamekua wakitoa nyaraka nyeti na za siri kwenye mitandao ya kijamii jambo ambalo si sawa.
“Maadili yanakataza kabisa kwa watumishi kutoa nyaraka nyeti za Serikali mitandaoni na hata kwa watu ambao haziwahusu , jambo ambalo ni hatari sana kwa mustakabali wa Taasisi na nchi kwa ujumla” Alisisitiza Mkurugenzi huyo.
Kategere alisema kuwa, utendaji kazi kwa watumishi wa umma kwa nyakati hizi unatakiwa uwe wenye tija na unaotoa matokeo chanya hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inafanya mageuzi makubwa kwenye miundombinu kuelekea Tanzania ya Viwanda.
Vilevile amesema ameridhishwa na maandalizi ya mfumo mpya wa Tehama ambao utasaidia katika ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki, hivyo akasisitiza umuhimu wa DART kuendelea kuwa wabunifu ikizingatiwa kwamba dunia sasa inaendelea kukua kimaendeleo ambapo mambo mengi yanafanyika kidijitali.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa DART Mhandisi Ronald Lwakatare, akizungumza katika kikao hicho amesema Wakala unaendelea na usanifu na ujenzi wa miradi ya barabara za Mabasi Yaendayo Haraka katika Barabara ya Kilwa kuelekea Mbagala na matarajio ni kuendelea kupanua mtandao kuelekea katika maeneo mengine kadiri bajeti itakavyoruhusu.
“Tunaendelea na ujenzi wa miundombinu katika maeneo mengine ya Jiji na lengo letu ni kuhakikisha kule kote ambako tumefanya utafiti na kujiridhisha kunafaa kuwa na barabara ya mwendokasi tunapeleka huduma hiyo” Alisema Mhandisi Lwakatare.
Amesema kuwa Taasisi yake inajipanga pia kuhakikisha inafanya utafiti katika Jiji la Dodoma ambalo ndio makao Makuu ya Nchi kuona ni barabara zipi zitafaa kwa ajili ya kujenga miundombinu ya barabara za Mabasi Yaendayo Haraka.
“Nilimsikia Mh.Rais wakati wa uzinduzi wa jengo la Tarura kuwa anatamani Jiji la Dodoma liwe na barabara za mabasi yaendayo haraka pamoja na treni za haraka, sisi tumelichukua na tunajipanga ili wataalam wetu waende angalau kwa kuanzia kutathmini nini cha kufanya ili kama jukumu hilo tutakabidhiwa tulitekeleze kwa kiwango cha hali ya juu” Alisema.
Awali akimkaribisha Bw. Kategere, Mhandisi Lwakatare alisema janga la ugonjwa wa Corona lilisababisha hasara kubwa katika uendeshaji wa Mabasi Yaendayo Haraka kwani zaidi ya asilimia 70 ya mapato hayakupatikana kutokana na utaratibu wa kubeba abiria kulingana na idadi ya viti vilivyomo kwenye basi.
Alisema uwezo wa mabasi ni kubeba abiria 140 lakini idadi ya viti ni 40 tu hivyo unakuta uendeshaji unakuwa wa hasara kwani mabasi hayo ya haraka yamebuniwa kubeba abiria waliosimama zaidi ya wale waliokaa.
Mhandisi Lwakatare alibainisha kuwa, mipango ya kuimarisha usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka inaendelea vyema na mwishoni mwa mwaka huu ana imani mzabuni aliyepewa kazi ya kununua mabasi atakamilisha kazi hiyo ili hatimaye kuwa na mabasi ya kutosha kwa ajili ya kurahisisha usafiri Jijini Dar es Salaam.
Aidha alisema kuwa umuhimu wa kuongeza idadi ya mabasi umekua mkubwa kutokana na kuongezeka kwa watumiaji wa usafiri huo, kwani wakati mradi unaanza ulikua unahudumia watu 70,000 kwa siku ambao kwa sasa wameongezeka hadi kufikia 200,000 kwa siku.
Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka – DART ni Taasisi iliyo chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI, yenye jukumu la kusimamia na kuendeleza miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka katika Jiji la Dar es Salaam.Taasisi nyingine zilizoko chini ya TAMISEMI ni pamoja na Tume ya Utumishi wa Walimu, Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa,Tarura, Shirika la Masoko Kariakoo,Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo pamoja na Shirika la Elimu Kibaha.
Mwisho.