Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla akizungumza na wadau mbalimbali wa Sekta ya Utalii wakati wa Uzinduzi wa Mkakati wa Kukukuza Utalii wa ndani leo jijini Dar es salaam.
***********************************
Na. Aron Msigwa – WMU.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla ametoa wito kwa watanzania wajitokeze kuwekeza katika biashara ya Utalii kwa kuwa masharti ya kuwekeza katika biashara hiyo yamerahisishwa tangu Serikali ya Awamu ya tano ilipoingia madarakani.
Dkt. Kigwangalla ameyasema hayo leo jijini Dar es salaam wakati akizindua Mkakati wa Kukuza Utalii wa ndani unaolenga kutoa ajira na kuwahamasisha watanzania washiriki na kuwekeza katika sekta ya utalii na kuvitembelea vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini.
Amesema tangu kuingia Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli yamefanyika mabadiliko mbalimbali yaliyolenga kuleta tija na kuifungamanisha sekta ya utalii na maendeleo ya watu kwa kuhakikisha wananchi wananufaika na sekta hiyo.
Dkt. Kigwangalla amesema Serikali ilifanya jitihada za makusudi za kulegeza masharti na kushusha viwango vikubwa vya tozo vilivyokuwepo ambavyo vilikua vinawazuia wafanya biashara wadogo hasa wazawa washindwe kuingia katika sekta hiyo.
Amesema tangu kuondolewa kwa masharti hayo watanzania wazawa wanaofanya biashara ya huduma za utalii wameongezeka kutoka 1100 hadi kufikia 2000 wengi wao wakiwa watanzania.