Mwenyekiti wa Kikundi Kazi cha Kilimo chini ya mwamvuli wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC) Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya akiendesha kikao cha sita Jijini Dar es Salaam
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya ambaye ni Mwenyekiti wa Kikundi Kazi cha Kilimo akiwa pamoja na Mama Jacqueline Maleko Mwenyekiti mwenza wakati wa kikao cha sita cha Kikundi Kazi Jijini Dar es Salaam leo
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya ambaye ni Mwenyekiti wa Kikundi Kazi cha Kilimo akiwa pamoja na Wajumbe wa Kikundi Kazi cha Kilimo leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni Mwenyekiti Mwenza Mama Jacqueline Maleko na kulia kwake ni Dkt. Godwill Wanga, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (Picha zote na Issa Sabuni – Wizara ya Kilimo)
…………………………………………………………………………………..
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya ametoa wito kwa Wakulima wa Tanzania kujiunga katika vikundi ili kuunganisha nguvu na kuja na miradi mikubwa ambayo itakuwa rahisi kupata mikopo kutoka kwenye Taasisi za Fedha kama Benki ya Kilimo (TADB).
Katibu Mkuu ameyasema hayo leo wakati akifungua kikao cha sita cha Kikundi Kazi cha Kilimo chini ya Baraza la Taifa la Biashara, kikao kilichofanyika Jijini Dar es Salaam.
Bwana Kusaya amesema Tanzania ya Viwanda inajengwa na Wakulima wanaolima kwa tija; Jambo hilo haliwezekani bila ya msaada wa Taasisi za Fedha.
“Bila ya mikopo hakuna miradi mikubwa itakayofanikiwa. Niwaombe Wakulima wa mazao yote na hasa Wakulima wanaolima mazao yenye thamani kubwa kama mboga, matunda na maua kuwa ili kilimo kichangie kwenye uchumi wa viwanda kwa kuzalisha malighafi kwa ajili ya viwanda vyetu ni vyema Wakulima wawe kwenye vikundi; Kwa kufanya hivyo, mtachangia kwenye uchumi wa viwanda.
Aidha Katibu Mkuu Gerald Kusaya ameongeza kuwa Wakulima wa mazao mengi ya biashara hawajiunga katika vikundi na kuongeza kuwa fursa nyingi za masoko ya kilimo zinapatikana kwa kuwa kwenye vikundi.
“Wakulima itumie fursa ya kupata mikopo na uwezeshaji kwa kukaa kwenye vikundi kama Vyama vya Ushirika lakini pia tumie fursa ya masoko ya mazao kwa njia ya mitandao kama SOKO LA BIDHAA TANZANIA (TMX).
“Soko la bidhaa ni mahali rasmi ambapo wanunuzi na wauzaji wa bidhaa hukutanishwa pamoja ambapo wote ni wanachama au huwakilishwa na Wanachama. Sasa ili Wakulima wauze bidhaa au mazao yao ni vizuri wakawa katika vikundi”. Amekaririwa Katibu Mkuu.
Soko la bidhaa limegawanyika katika maeneo makubwa matatu ambayo ni: – Soko la mauzo ya papo kwa papo – (Spot Exchanges). Bidhaa huuzwa kwa bei ya papo kwa papo. Uchukuaji na malipo ya bidhaa hufanyika sio zaidi ya siku mbili baada ya mauzo.
Eneo la pili ni soko la mauzo ya mkataba unaotekelezwa baadaye (Futures exchanges). Bei ya bidhaa hukubaliwa siku hiyo hiyo kwa malipo na uchukuaji bidhaa utakaofanyika baada ya kipindi fulani, kwa mfano baada ya siku 90. Huwezesha kujikinga na athari za kubadilika kwa bei.
Na tatu ni soko la mauzo ya mkataba wenye uchaguzi wa kutekelezwa (Options). Bei ya bidhaa hukubaliwa leo kwa ada na sio lazima malipo na uchukuaji bidhaa ukafanyika baada ya kipindi kilichokubaliwa.