Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa aliyekuwa Mwalimu na mwimbaji wa kwaya ya SDA Kurasini mwalimu Samson Kibaso kabla ya mazishi yaliyofanyika Juni 30, 2020 katika kijiji cha Ingrichini Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara.
Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Mwalimu na mwimbaji wa kwaya ya SDA Kurasini mwalimu Samson Kibaso likishushwa kaburini wakati wa mazishi yake yaliyofanyika Juni 30, 2020 katika kijiji cha Ingrichini Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Mwita Waitara akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa aliyekuwa Mwalimu na mwimbaji wa kwaya ya SDA Kurasini mwalimu Samson Kibaso kabla ya mazishi yaliyofanyika Juni 30, 2020 katika kijiji cha Ingrichini katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara.Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Mwita Waitara(kulia) akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka katika mazishi ya aliyekuwa Mwalimu na mwimbaji wa kwaya ya SDA Kurasini mwalimu Samson Kibaso, yaliyofanyika Juni 30, 2020 katika kijiji cha Ingrichini katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara.
*********************************
Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewaongoza mamia ya waomboleaji kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Mara, Mwanza, Simiyu na nchi jirani ya Kenya katika mazishi ya aliyekuwa mwalimu na mwimbaji wa Kwaya ya Kanisa la Wadventista Wasabato (SDA) Kurasini, Mwl.Samson Kibaso ambaye pia ni mtunzi wa wimbo wa Jumiya ya Afrika Mashariki.
Mazishi hayo yamefanyika Juni 30, 2020 katika Kijiji cha Ingrichini Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Mkoani Mara na kuhudhuriwa na viongozi wa Kitaifa wa Kanisa la SDA, Wachungaji kutoka konferensi mbalimbali za Kanisa hilo pamoja na viongozi wa Serikali akiwemo Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Mwita Waitara .
Akizungumza na waombolezaji, Mtaka amesema Mwalimu Samson Kibaso amefanya kazi kubwa ambayo imeacha alama ya utumishi wake si tu katika Kanisa la Waadvenista Wasabato(SDA) bali hata katika madhehebu mengine ambayo amefanya kazi nayo kupitia kazi yake ya utunzi wa nyimbo.
“Yapo maandiko yanasema hubirini kwa sauti ya kuimba, kupitia yeye (Kibaso) ameongoa wengi, amegusa wengi, tuna wachungaji ambao wangeweza kufa ndani ya kanisa wanaofahamika kimataifa lakini wasingetoka watu Kenya wakaja hapa; wote tunajua kuna shida ya kusafiri lakini kuna watu kutoka Kenya wakasema lazima wafike kuona safari ya mwisho ya huyu mtu mwema,” alisema Mtaka.
Aidha, Mtaka amesema atakuwa tayari kushiriki katika mambo ambayo Kanisa litayafanya kwa kumuenzi Mwalimu Samson Kibaso huku akibainisha kuwa heshima aliyopewa Mwalimu Kibaso inabeba taswira ya namna kazi ya Kwaya ya Kurasini inavyopokelewa na watu.
Katika hatua nyingine Mtaka ametoa wito kwa wazazi na walezi katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kuthamini elimu kwa kuhakikisha wanawapeleka watoto wao shule ili wapate elimu huku akisisitiza kuwa elimu ndiyo inaweza kuwawafanya wakashindana na watu kutoka maeneo mengine.
Akitoa mahubiri kabla ya mazishi ya Mwalimu Kibaso, Askofu wa Kanisa la Waadventista Wasabato(SDA) Jimbo la Kusini mwa Tanzania, Mch. Mark Malekana amemzungumzia Kibaso kuwa alikuwa na mchango mkubwa kwa kanisa, mtu mnyenyekevu pamoja na kipaji alichokuwa nacho, hivyo akatoa wito kwa waimbaji na walimu wengine kuacha kiburi na kutumia vipaji vyao kwa utukufu wa Mungu.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Mwita Waitara ametoa pole kwa familia, kwaya ya Kurasini na Kanisa la SDA na kubainisha kuwa anatambua kazi kubwa iliyofanywa na Mwalimu Samson Kibaso hivyo atakuwa tayari kushirikiana na familia, kwaya na kanisa katika kuenzi kazi zake.
Nao wanakwaya wa Kwaya ya SDA Kurasini wamesema wamempoteza, nguli wa muziki, mwalimu mahiri wa uimbaji na rafiki yao, huku wakiahidi kumuenzi kwa kuendelea kumuimbia Mungu ili kupitia uimbaji wao watu waendelee kumuona Mungu.
Mwalimu Samson Kibaso alizaliwa mwaka 1956 na amekuwa mwalimu wa kwaya ya SDA Kurasini tangu mwaka 1985, ambapo pamoja na kuwa mwalimu katika Kwaya ya SDA Kurasini Kibaso pia amefundisha kwaya ya madhehebu mbalimbali kama KKKT, Anglican na Moravian.
Pia alitunga na kufundisha nyimbo za taasisi mbalimbali ikiwemo muhimili wa mahakama pamoja na kutunga wimbo wa jumuiya ya Afrika Mashariki ambao mpaka sasa umekuwa ukiimbwa katika nchi zote zinazounda Jumuiya hiyo.