Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Utamaduni wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt.Emmanuel Temu (kushoto) akizungumza na Chifu Mazengo wa Pili (kulia) kuhusu mila na desturi za himaya hiyo wakati alipotembelea eneo la Chifu huyo lililopo Mvumi Jijini Dodoma Julai 01, 2020.
…………………………………………………………………………………..
Na Shamimu Nyaki –WHUSM
Serikali imeziagiza himaya za Kichifu kuwa na utaratibu wa kutoa elimu kwa jamii inayozunguka himaya zao ili ielewe mila na desturi za himaya hizo lengo ikiwa ni kuondoa migogoro inayotokea mara kwa mara.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Idara ya Utamaduni wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Emmanuel Temu wakati alipokuwa akitatua mgogoro kuhusu Serikali ya Kijiji kuruhusu mti unaotumika kufanyia ibada ya kimila kukatwa na mmoja wa wanakijiji wa kijiji cha Mvumi kilichopo mkoani Dodoma.
“Serikali inatambua mchango mkubwa wa Machifu katika kulinda, kuendeleza na kuhifadhi mila na desturi za taifa hili hivyo, ni vizuri himaya za kichifu kuwa na utaratibu wa kutoa elimu kuhusu mila hizo kwa jamii inayoizunguka ambayo itasaidia kila mwanajamii kuwa na uelewa wa utamaduni huo”alisema Dkt.Temu
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa wa Kijiji hicho Bi. Happines Pessa amesema kuwa Serikali ya kijiji inatambua baadhi ya maeneo ya kihistoria ambayo yapo kijijini hapo lakini ameitaka Himaya hiyo kuainisha maeneo mengine ambayo Serikali haiyatambui ili yaweze kulindwa na kutoruhusu wananchi kuyatumia katika shughuli za kijamii.
“Katika mikutano yetu ya kijiji tutatoa nafasi kwa Chifu Mazengo atoe elimu kwa wanakijiji kuhusu umuhimu wa utamaduni wa kimila katika taifa letu, lakini pia kutoa ushirikiano kwa Serikali kuhusu kuanisha maeneo hayo”alisema Bibi Happiness.
Katika hatua nyingine Wizara imetembelea maeneo yenye kumbukumbu za mila na desturi ikiwemo nyumba ya chifu Mazengo wa kwanza ambayo baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliwahi kulala wakati wa harakati za kukianzisha chama cha TANU alipofika mkoani Dodoma
…MWISHO..