Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, Bw. Fredrick Kanyondwi, akielezea huduma zinazotolewa katika Hospitali hiyo ikiwemo huduma ya Mama na Mtoto kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, alipotembelea na kukagua ujenzi wa Hospitali hiyo wakati wa ziara ya kikazi mkoani Kigoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, akitoa maagizo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, Bw. Anosta Nyamwoga, baada ya kutoridhishwa na ubora wa baadhi ya miundombinu ya Hospitali ya Wilaya hiyo, alipotembelea na kukagua ujenzi wake.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, Bw. Wilson Bigambo, akimuongoza Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, (kushoto), kuangalia majengo ya hospitali hiyo ya Wilaya alipotembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za Serikali. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayalina.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.Dkt. Philip Isdor Mpango, akimsikiliza mgonjwa Bw. Lucas Lulomona, aliyefika kupata huduma katika Hospitali ya Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, akizungumza na baadhi ya wakina Mama, walioshiriki katika kazi za muda mfupi za ujenzi wa majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Kanali Michael Ngayalina, kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Bw. Rashid Mchata.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.Dkt. Philip Isdor Mpango, akimuuliza Mfamasia wa Hospitali ya Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, Bw. Juma Lukanya kuhusu changamoto ya Kitengo cha Dawa, ambapo aliomba makabati ya kuhifadhi dawa alipotembelea hospitalini hapo mkoani Kigoma
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi wa Mkoa wa Kigoma na watumishi wa Hospitali ya Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma baada ya kumaliza kutembelea majengo ya hospitali hiyo.
Moja ya majengo ya Hospitali ya wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma linavyoonekana kwa sasa
……………………………………………………………………
Na. Josephine Majula na Peter Haule, WFM, Kigoma
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango, ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Kigoma kumsimamia ipasavyo mkandarasi anayejenga Hospitali ya Wilaya ya Buhigwe mkoani humo, baada ya kutoridhishwa na ubora wa majengo ikilinganishwa na kiasi cha shilingi bilioni 2.4 zilizotumika mpaka hivi sasa kujenga moiundombinu ya Hospitali hiyo.
Dkt. Mpango alitoa agizo hilo wakati alipotembelea na kukagua Mradi wa Ujenzi wa Hospitali hiyo ya Wilaya ambayo licha ya miundombinu yake kutokamilika ipasavyo imeanza kutoa huduma kwa wananchi kuanzia mwezi Juni, 2020.
“Ubora wa majengo hauendani na matarajio, inatakiwa iwe Hospitali ya Wilaya ya Kisasa kabisa hivyo muongeze usimamizi wa Mkandarasi, nitarudi tena hapa mwezi wa nane na mkandarasi afikishiwe salamu kuwa Waziri hakufurahishwa na ubora wa kazi kwa kuwa nikirudi nitaangali pia na thamani ya fedha kama fedha za wananchi zimewaletea kitu kinacholingana na fedha tulizotoa”, alieleza Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango alisema kuwa fedha ya wananchi haitakiwi kuchezewa kwa kuwa wanatozwa kodi hivyo inatakiwa kurudi kwao kwa kuwaletea huduma ambazo zinafanana na thamani ya jasho lao.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayalina alisema atayafanyia kazi maelekezo ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mpango, na pia akamuomba kusaidia kuwezesha mradi huo kukamilika ili utoe huduma stahiki kwa wananchi kwa kuwa Waziri huyo amefika na kujionea hali halisi ya huduma zinazotolewa.
Aidha alimshukuru Dkt. Mpango kwa kuendelea kufanya ziara katika Wilaya hiyo na kukagua miradi inayopatiwa fedha na Serikali na kuchukua hatua zitakazowezesha kupata thamani ya fedha za miradi.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Buhigwe, Bw. Fredrick Kanyondwi, alisema kuwa kiasi cha Sh. bilioni 2. 7 kilipokelewa kwa awamu nne na Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali hiyo ambayo imeanza kutoa huduma kuanzia Juni, 2020 kwa kutumia miundombinu iliyopo wakati ikisubiriwa kukamilika ili kutoa huduma kwa ufanisi.
Alisema ujenzi wa majengo ya Hospitali yametumia mfumo wa Force Acount ambapo jengo la Maabara limekamilika kwa asilimia 95, Mama na mtoto asilimia 87, utawala asilimia 99, jengo la wagonjwa wa nje asilimia 99 na majengo mengine kama la mionzi, jengo la dawa na kufulia ambayo kwa ujumla yametumia takribani Sh. bilioni 2.4.
Bw. Kanyondwi alisema kuwa bado kuna upungufu wa takribani Sh. milioni 200 baada ya ya Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe kubaini upungufu wa Sh. milioni 500 ambapo mwezi Juni zilitolewa Sh. milioni Sh. milioni 300 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo na kusalia shilingi milioni 200 ambazo zinahitajika ili kukamilisha ujenzi huo.