Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini wa Mkoa wa Manyara (Marema) Justin Nyari (kulia) akizungumza na mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Bilionea Saniniu Kurian Laizer (katikati) na Katibu wa Marema, Tariq Kibwe kwenye sherehe ya kumshukuru Mungu na kuwapongeza wachimbaji wake waliofanikisha upatikanaji wa madini ya Tanzanite yaliyouzwa shilingi bilioni 7.7.
……………………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu, Manyara
MWENYEKITI wa chama cha wachimbaji madini Mkoani Manyara, (Marema) Justin Nyari amekemea vikali maneno potofu yanayozungumzwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani, Bilionea Saniniu Kurian Laizer amedhulumiwa na serikali baada ya kupunjwa fedha alizouza madini yake ya Tanzanite shilingi bilioni 7.7.
Nyari ameyasema hayo jana wakati akizungumza kwenye kijiji cha Naepo Kata ya Naisinyai Wilayani Simanjiro nyumbani kwa Bilionea Laizer katika sherehe ya kumshukuru Mungu na kuwapongeza wachimbaji wake kwa kufanikisha upatikanaji wa madini hayo.
Amesema wanaotangaza habari hizo potofu wanapaswa kupuuzwa kwani bilionea Laizer amerahisishiwa kazi na Serikali kwa kupatiwa kiasi hicho cha fedha baada ya kununua madini hayo.
Amesema wanaozusha maneno hao wanapaswa kutambuwa kuwa mchimbaji akishapata madini kinachofuata ni tathmini na kupangiwa bei ya madini kisha biashara kufanyika bila kubaini mtu atakayenunua madini hayo.
“Laizer alipopata madini hayo yalifanyiwa tathmini ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya Tanzanite bila kujua ni serikali au nani atanunua madini haya kwani mtu yeyote angeweza kununua hivyo habari hizo potofu za kupewa bei ndogo au kupunjwa zinapaswa kupuuzwa,” amesema Nyari.
Amesema wanaishukuru Serikali kwa kununua madini hayo ya Laizer kwani hivi sasa kuna changamoto ya bei ya madini ya Tanzanite kutokana na janga la corona hivyo serikali imewarahisishia kazi.
Amesema Manyara wanatambua kazi nzuri inayofanywa na serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli kupitia Waziri wa Madini Dotto Biteko kwani inawajali wachimbaji wa madini wa eneo hilo.
“Tutaendelea kushirikiana na Serikali katika shughuli zetu za uchimbaji madini kwani ina malengo mazuri ya kuhakikisha watanzania wanaendelea kunufaika na madini haya tukipata mfano kwa Laizer na hata mimi natarajia kuwa bilionea mpya kupitia madini hayo ya Tanzanite,״ amesema Nyari.
Kwa upande wake bilionea Laizer amesema yeye aliridhika na bei iliyotolewa na serikali kwani hakupunjwa wala kudhulumika kama baadhi ya watu wanavyozusha kwenye mitandao ya kijamii.
Bilionea Laizer amesema alichokipata ndicho kilikuwa stahili yake hivyo anaishukuru serikali ya Rais John Magufuli na Waziri wa Madini Dotto Biteko kwa kufanikisha hilo.