Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai akizungumza hafla ya makabidhiano ya Kompyuta 20 alizozitoa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kwa ajili ya shule za sekondari za Wilaya hiyo, kushoto ni Mkurugenzi wa Elimu TAMISEMI, Ndugu Julius Nestory na kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kongwa aliyemaliza muda wake Ndugu White Zuberi.Hafla hiyo imefanyika katika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa.
Mkurugenzi wa Elimu TAMISEMI, Ndugu Julius Nestory akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya Kompyuta 20 zilizotolewa na Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kwa ajili ya shule za sekondari za Wilaya hiyo, katikati ni Mheshimiwa Spika na kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kongwa aliyemaliza muda wake Ndugu White Zuberi.Hafla hiyo imefanyika katika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa.
Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya Kompyuta 20 alizozitoa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kwa ajili ya shule za sekondari za Wilaya hiyo, kushoto ni Mkurugenzi wa Elimu TAMISEMI, Ndugu Julius Nestory na kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kongwa aliyemaliza muda wake Ndugu White Zuberi na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Dkt. Omary Nkulo .Hafla hiyo imefanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa.
Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai akikabidhi kompyuta kwa baadhi ya wakuu wa shule za sekondari za Wilaya ya Kongwa katika hafla ambayo ilihudhuriwa pia na baadhi ya viongozi wakiwemo Mkurugenzi wa Elimu TAMISEMI, Ndugu Julius Nestory, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kongwa aliyemaliza muda wake Ndugu White Zuberi na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Dkt. Omary Nkulo
PICHA NA OFISI YA BUNGE.
……………………………………………………………..
Na Debora Sanja, Bunge
Mkurugenzi wa Elimu kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Julius Nestory amemshukuru Spika wa Bunge, Job Ndugai kwa juhudi zake za kuchangia sekta ya elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa.
Mkurugenzi huyo alitoa shukrani hizo katika hafla ya kukabidhi kompyuta 20 zilizotolewa na Spika kwa ajili ya Shule za Sekondari za Wilaya ya Kongwa iliyofanyika katika Ofisi za Halmashauri hiyo.
“Nakushuru sana Mheshimiwa Spika kwa juhudi zako za kuchangia sekta ya elimu, mimi nimeshatembea halmashauri zote nchini zipo baadhi ya shule wanafunzi wake hawajawahi kuona kompyuta wanasoma kwa kuchorewa ubaoni,Mungu akubariki sana”
“Aidha, naipongeza Wilaya ya Kogwa kwa kufanya vizuri katika mitihani kati ya Wilaya za Mkoa wa Dodoma, Tunashukuru kwa kuwa kila mwaka matokeo yanapanda, naipongeza Serikali kwa mipango mizuri lakini kwa usimamizi imara wa Bunge,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kongwa, Dkt. Omary Nkulo alipongeza juhudi za Spika wa Bunge ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kongwa kwa kuendelea kuisaidia Kongwa.
“Mheshimiwa Spika amekuwa akitusaidia sana, siyo misaada yote inatoka kwa wafadhili bali kuna baadhi hutoa fedha mfukoni mwake, ni mdau mkubwa wa elimu na afya, ametusaidia nondo, bati, mifuko wa saruji ya kujengea shule na kiasi kikubwa cha fedha za Mfuko wa Jimbo hutumia katika sekta hizi mbili,” alisema.
Awali kabla ya kukabidhi kompyuta hizo kwa wakuu wa shule Spika Ndugai alishukuru kwa pongezi zote na kuzitaka baadhi ya shule ambazo zitakosa mgao huo kuwa na subira hadi hapo zitakapopatikana zingine.
“Shukrani kwa wadau waliotupatia kompyuta hizi , namshukuru Mkurugenzi wa Elimu kwa kututembelea Kongwa pamoja na kuzipatia fedha baadhi ya shule za sekondari za Kongwa kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa,” alisema.
Kompyuta hizo zimetolewa na Umoja wa Wanawake wa Kampuni ya Sigara Tanzania ambapo walimkabidhi Spika kwa ajili ya Jimbo la Kongwa.
Mwisho.