Na Mwandishi Wetu, Mbeya
SIMBA SC wamefanikiwa kutwaa taji la tatu mfululizo la ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya sare ya 0-0 na wenyeji, Tanzania Prisons jioni ya leo Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
Kwa sare hiyo, Simba SC wanafikisha pointi 79 baada ya kucheza mechi 32, wakiwaacha mbali watani wao wa jadi, Yanga SC wanaofuatia katika nafasi ya pili wakiwa na pointi 60 baada ya kucheza mechi 32 pia.
Simba imefika jumla ya mataji 21 ya Ligi Kuu ikizidiwa mataji 6 na watani zao Yanga ambao wametwaa ubingwa mara 27 Ligi Kuu Tanzania bara.
Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Mbao FC imeibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania, bao pekee la Waziri Junior dakika ya 65 Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.
Kikosi cha Tanzania Prisons kilikuwa; Jeremiah Kisubi, Michael Ismail, Benjamin Asukile, Vedastus Mwihambi, Nurdin Chona, Jumanne Elfadhil, Salum Kimenya/Ismail Azizi dk61, Ezekia Mwashilindi, Samson Mbangula, Jeremiah Juma na Adil Buha.
Simba SC; Aishi Manula, Haruna Shamte, Gardiel Michael, Erasto Nyoni, Kennedyy Juma, Gerson Fraga, Hassan Dilunga/Luis Miquissone dk67, Muzamil Yassin, Meddie Kagere, Ibrahim Ajibu/Clatous Chama dk46 na Mraj Athumani ‘Madenge’/John Bocco dk80.