Makamu mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Bara Mzee Philip Mangula jana tarehe 27 Juni, 2020 pamoja na mambo mengine, ameeleza sababu za kumchagua tena Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika uchaguzi ujao wa Mwezi Oktoba mwaka huu.
Mzee Mangula ameyasema hayo alipokuwa akitoa nasaha kwa makatibu wa wilaya zote nchini katika mafunzo yanayoendelea kwa watendaji hao Makao Makuu ya CCM Dodoma.
“Naamini mnajua kwamba, watakao fanya vibaya sijui watakuwa na maelezo gani, kazi alioifanya Rais wetu ya kutekeleza Ilani na ametekeleza hata yale yaliokwama miaka na miaka mengine aliamuliwa tangu mwaka 1973 ndani ya Halmashauri Kuu, ndani ya Mkutano Mkuu na kwa wanachama wote walishiriki katika kutoa maamuzi ya kuhamia dodoma, na mpaka iliundwa Wizara ya kuhamishia makao makuu Dodoma, ilihama kwani??” Mzee Mangula amehoji.
“Safari hii chama na kwenye Ilani imo Dkt. Magufuli alisema tutahama, katika kipindi changu cha urais tunahama! Tumahamia Dodoma, yupo aliyebaki Dar es salaam? Kuna wizara ipo Dar es salaam bado ndani ya miaka mitano hii?, kitu ambacho tumekiongelea kwa miaka tangu 1973 ni miaka mingapi hiyo!”. Mzee Mangula amefafanua
Makamu Mwenyekiti amesisitiza kuwa, ” kwa kazi hii, tuna mtu anayetaka tumpe moyo na tuoneshe nguvu zetu zote tumuunge mkono wote na dunia ijue kwamba huyu mtu anaungwa mkono na wapiga kura wake na wananchi wake.”
Awali, akimkaribisha Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu ameendelea kusisitiza mafanikio ya CCM yanategemea mambo matatu muhimu, Nidhamu ya Chama, Haki kwa wanachama ambao watajitokeza kugombea nafasi za uongozi na kujitolea kwa wanachama kutafuta ushindi wa Chama chetu.
Semina hiyo ya leo imehudhuriwa na Wenyeviti wa Jumuiya zote za CCM na Wenyeviti wa CCM wa Mikoa yote nchin.