……………………………………………………………………..
Aliyekuwa mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa wa Mkoa wa Manyara mwaka 2007 hadi 2015 Cosmas Bura Masauda amesema vigogo wanaompinga Rais John Magufuli Magufuli, huenda wana uraia wa nchi mbili.
Masauda akizungumza jana mjini Babati alisema yeye alikuwa mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa mwaka 2007 hadi 2015 hivyo anashangazwa na vigogo kama Bernard Membe wanampinga Rais Magufuli.
Alisema wanaompinga wanapaswa kutambua kuwa Rais Magufuli anapaswa kupita bila kupingwa kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu ili aone namna anavyoungwa mkono na watanzania na siyo kupingwa.
Alisema Membe hana uwezo wa kipambana na Rais Magufuli, kwani hata kwenye mkutano mkuu wa Taifa Dodoma mwaka 2012 alishindwa kwa kura na Januari Makamba na Mwigulu Nchemba kati ya watu 12 waliopitishwa NEC Membe alikuwa wa saba.
“Wewe kama ulishindwa na kina January na Mwigulu utamuweza Rais Magufuli hata akisimama na mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira kwa kweli atagaragazwa kwani Rais Magufuli ni wa kwanza kukubalika na wakulima na wafugaji,” alisema.
Alisema hata Membe akiachiwa aingie uwanjani hivi sasa hana mvuto Rais Magufuli ni mzalendo atamuacha mbali sana hivyo asijisumbue aachane na wazo hilo la kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Aliwataka vijana wachangamkie fursa ya kugombea ubunge na udiwani kwani Rais Magufuli ameirudisha CCM katika misingi bora na hata usipokuwa na fedha hivi sasa unaweza kugombea uongozi.
“Vijana changamkieni fursa hata ukiangalia mwaka 2015 fomu za kugombea ubunge ndani ya CCM ilikuwa shilingi milioni 2.1 na hivi sasa ni sh100,000 ni ishara tosha kuonyesha kililenga matajiri sasa hivi chini ya Rais Magufuli ni chama cha wanyonge,” alisema Masauda.
Alisema vijana wasijali lolote kwani CCM chini ya uenyekiti wa Rais Magufuli na Katibu Mkuu Dk Bashiru Ally imekuwa mpya na kimbilio la watu wanyonge tofauti na awali.
Alisema vijana wanachangamkia fursa kwani hata hivi sasa mjini Babati watia nia ya kugombea ubunge ndani ya CCM wapo zaidi ya 20 wakiwemo walimu 12 na madaktari sita.