NA FREDY MGUNDA,MAFINGA.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri mkuu,Uwekezaji Angellah Kairuki awataka wawekezaji wazawa kuiga mfano wa kampuni ya uchakataji nguzo za umeme ya Qwihaya General Enterprises Company Ltd kwa kuwekeza mtaji mkubwa wenye tija kwa watanzaji na serikali kwa ujumla kutoka na uwekezaji wake kujikita katika miji ambayo inakuwa kiuchumi.
Waziri Kairuki alieeleza kufurahishwa na kasi ya uwekezaji inayofanywa na kampuni hiyo kwa kuwekeza viwanda vya nguzo katika mikoa mbali mbali ukiwemo mkoa wa Kigoma na kutaka wadau wengine kuelekeza nguvu zao katika mkoa wa Kigoma badala ya kuwekeza Dar es Salaam ,Dodoma na mikoa mingine ambayo ni rahisi kufikika .
Kairuki alisema kuwa amefurahishwa na kampuni hiyo kwa kuamua kuwekeza kiwanda katika mkoa wa Kigoma upo pembezoni mwa nchini na wawekezaji wengi wamekuwa wakikwepa kuwekeza viwanda vyao katika mkoa huo kutokana na umbali ila kampuni hiyo ya Qwihaya imefanikiwa kuwekeza kiwanda cha kuchakata nguzo za umeme kama ilivyo katika mkoa wa Iringa.
“Nimesikia kwenye risala yenu kuwa hivi karibuni mtafungua kiwanda katika mkoa wa Kigoma na Njombe jambo ambao zuri kwa kuwa mnaendeleza kukuza uchumi pamoja na kuongeza ajira kwa wananchi wengi hasa vijana ambao wamekuwa hawana ajira rasmi” alisema
Alisema kuwa mkoa wa Kigoma upo pembezoni na serikali imejipanga kuendelea kuhamasisha wawekezaji kufika kuwekeza katika sekta mbalimbali katika mkoa huo kwa kuwa unakuwa kwa kasi kiuchumi na unamazingira mazuri ya uwekezaji hivyo wadau wanakaribishwa kuwekeza Kigoma.
“Kitendo cha Qwihaya kufika kuwekeza Kigoma ni uzalendo wa hali ya juu na mmefungua mlango kwa wawekezaji wengine kufika kuwekeza katika mkoa wa Kigoma wanahitaji kunufaika na sekta ya uwekezaji sio kwamba siwapongezi kwa kuwekeza kiwanda hapa Mafinga mkoani Iringa nawapongeza pia ila kwenda Kigoma mmefanya jambo zuri zaidi maana kupitia mkoa wa Kigoma mtakuwa na uwezo wa kuuza bidhaa zenu katika nchi za jirani na Tanzania “
Kairuki alisema mpango wa kampuni ya Qwihaya wa kufungua kiwanda cha kutengeneza dawa ya kutibu nguzo Kibaha ambacho kitakuwa ni kiwanda cha kwaza cha aina hiyo kwa Tanzania kwani alisema kwa sasa hakuna kiwanda cha dawa ya kutibu nguzo nchini .
Akizungumzia changamoto za miundo mbinu ya barabara ya Mgololo Mufindi alisema kuwa tayari TANROADS mkoa wa Iringa wamekwisha fanya upembuzi yakinifu juu ya barabara hiyo na wakati wowote itafanyiwa matengenezo ya kiwango cha lami .
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Qwihaya Leonard Maheda alisema kuwa kiwanda hicho kimeanzishwa mwaka 2007 kama kiwanda cha uchanaji mbao na mwaka 2015 kilianza kutengeneza nguzo baada ya kauli mbinu ya Rais Dkt John Magufuli juu ya serikali ya viwanda na hata kuzuia nguzo kutoka nje ya nchi .
Alisema kuwa kiwanda hicho kwa mwaka kinauwezo wa kuzalisha nguzo 800,000 na kuwa nchi nzima wanamiliki viwanda vitatu vya nguzo na wanakusudia kuanzisha kiwanda cha dawa za nguzo ambacho kitakuwa kiwanda pekee cha dawa za nguzo Tanzania .
Awali akisoma taarifa ya kiwanda hicho kwa waziri Kairuki ,kaimu mkurugenzi wa kampuni ya Qwihaya General Enterprises Ltd Benedicto Mahenda alisema kuwa gharama za uwekezaji wa kiwanda hicho ni takribani kiasi cha shilingi bilioni 15.
Alisema kuwa kwa kipindi kirefu kampuni imekuwa ikinunua malighafi za nguzo kutoka katika shamba la miti la Sao Hill iliyopo chini ya TFS na wamekuwa wakipata ushirikiano mkubwa kutoka kwa uongozi wa shamba hilo .
alisema kuwa soko la nguzo wamekuwa wakitegemea zaidi soko la ndani kupitia mteja mkubwa shirika la umeme Tanzania (TANESCO) na katika kipindi cha hiki cha utekelezaji wa mradi wa umeme vijijii (REA) awamu ya tatu) soko la nguzo limekuwa ni kubwa sana.
Naye mbunge wa jimbo la Mafinga Mjini Cosato Chumi alimpongeza muwekezaji wa kiwanda hicho kwa kuwa mzalendo kwa kuchangia shughuli za kimaendeleo katika sekta mbalimbali katika jimbo la Mafinga Mjini.
“Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Qwihaya Leonard Maheda amekuwa msaada mkubwa kwenye maendeleo ya jimbo langu kwani ametusaidia kuweka umeme kwenye shule zote za msingi na kusaidia kukuza sekta ya elimu kuanzia chini hadi ngazi ya sekondari”alisema Chumi
Chumi alisema kuwa kampuni hiyo imekuwa ikifanya kazi kwa weredi mkubwa kiasi kwamba hakuna malalamiko yoyote yale kutoka kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo tufauti ilivyo kwenye kampuni nyingine ambazo zimewekaza katika halmashuri ya Mji wa Mafinga.