********************************
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally, leo tarehe 26 Juni, 2020 amefungua semina ya mafunzo ya siku tatu kwa Makatibu wa CCM wa Wilaya zote nchini Makao Makuu Dodoma, ambapo ametumia fursa hiyo kufafanua masuala mbalimbali na kutaja mambo yanayovunja haki hasa katika kipindi hiki cha Uchaguzi.
Katibu Mkuu akifafanua masuala yanayovunja haki kwa makatibu hao amesema,
“Haki kubwa mnayoisimamia ni haki ya nchi hii kuendesha uchaguzi kwa amani na usalama, na yapo mambo yanayovunja haki, na yametajwa katika kanuni zetu. Moja ya jambo kubwa linalovunja haki ni Rushwa, rushwa za aina zote”.
Akifafanua rushwa amesema, ” Rushwa ziwe za ngono, ziwe za pesa, ziwe za kurubuniana na kuahidiana vyeo na kupeana zawadi, rushwa zote ni adui wa haki watendaji simamieni haki na kuepuka vitendo vya rushwa na kushughulika na wale ambao wanawarubani wanachama kwa rushwa.”
Aidha ameonya kuwa watendaji wasitumie kigezo cha haki kwa kuzuia rushwa kwa kubambikiza watu kesi wakati hakuna ushahidi.
Ameeleza kuwa, kusimamia haki ni kazi ngumu na ni ya hatari kwa kuwa unakuwa adui wa magenge ya kutafuta vyeo kileja leja.
Akisisitiza hilo amesema, “kuna watu hawataki kufanya kazi, wanadhani vyeo ni vya bure, vyeo vinapatikana kwa kazi, vyeo vya mipangilio na mipango haviwezekani ndani ya CCM ya sasa.” Amesisitiza Dkt. Bashiru.
Katibu Mkuu pia ametumia fursa hiyo kueleza umuhimu wa kusimamia nidhamu ya Chama kwa wanachama na watumishi wa Chama, pamoja na umuhimu wa kuwa na moyo wa kujitolea na kuwatambua wale wote wanaojitolea michango ya hali na mali katika kukiimarisha Chama chetu ngazi zote kuanzia Mashina, Matawi, Kata, Wilaya, Mikoa mpaka ngazi ya Taifa, kuwatia moyo zaidi na wafanye zaidi kwa uhai wa Chama.
Awali, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara Ndg. Rodrick Mpogolo akimkaribisha Katibu Mkuu, amewasisitiza Watendaji hao ngazi za wilaya kuyatumia mafunzo hayo kukiimairisha Chama katika maeneo yao ili kuwezesha ushindi wa kishindo Katika Uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Semina hii ni muendelezo wa mafunzo yanayoendeshwa ndani ya Chama kwa watendaji wa Chama ngazi mbalimbali.