Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Ndg. Amon Mpanju akifungua kikao cha siku mbili cha wataalam wa Kikosi kazi cha kupitia rasimu ya mpango kazi wa pili wa haki za binadamu kinachofanyika jijini Dodoma.Wengine pichani kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Haki za Binadamu Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Nkasori Sarakikya na kushoto ni Afisa Mchunguzi Mkuu na Mratibu wa Mpango kazi wa kwanza wa haki za binadamu Bw. Laurent Buliro kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
Wataalam wa kikosi kazi cha kupitia rasimu ya mpango kazi wa pili wa haki za binadamu wakimsikiliza mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Ndg. Amon Mpanju (hayupo pichani) wakati akifungua kikao cha kupitia rasimu hiyo.
Mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Ndg. Amon Mpanju akiwa katika picha ya pamoja na Wataalam wa kikosi kazi cha kupitia rasimu ya mpango kazi wa pili wa haki za binadamu baada ya kufungua kikao chao.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Ndg. Amon Mpanju akitaka kikosi kazi cha wataalam kutoka Wizara na Taasisi za Serikali zinazopitia rasimu ya Mpango kazi wa pili wa haki za binadamu kuibua vipaumbele vya msingi ambavyo vimekosekana katika mpango kazi wa kwanza ulioishia 2017.
“Mpango kazi wa kwanza ulioanza 2013 na kuishia 2017 haukuzingatia vipaumbele hivyo mpango kazi huu wa pili ulete vipaumbele vya msingi”.
Naibu Katibu Mkuu aliyasema hayo wakati akifungua kikao kazi hicho cha siku mbili kinachofanyika jijini Dodoma.
Aliongeza, kazi hii ya kupitia rasimu ya mpango kazi wa pili wa haki za binadamu ni muhimu kuifanya kwa umakini kwani inatoa muongozo wa kisera katika kusimamia masuala ya haki za binadamu na pia hauji kuwa mbadala wa mambo mengine ya haki za binadamu.
Mpanju aliwasisitiza wataalam hao kuwa mpango kazi huu uzingatie haki za kiraia, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni, kijamii, kimaendeleo na makundi maalum mfano wakulima na walemavu.
Aliongeza, mpango kazi wa pili wa haki za binadamu ni kipaumbele cha Serikali na utakuwa mwongozo wa kisera wa kukuza na kulinda haki za binadamu nchini na hivyo alisisitiza kuwa kila taasisi ihakikishe kwamba vipaumbele katika sekta zao zimo katika mpango kazi huu ili kuufanya uwe bora zaidi kwani mpango kazi wa haki za binadamu wa kwanza japokuwa ulipata mafanikio kadhaa lakini haukuzingatia vipaumbele.
Aliwasihi wataalam hao kufanya kazi kwa weledi na kwa kujituma na kutambua kwamba zoezi hili ni nyeti na ni la muhimu alisema, “nawasihi kutoa ushirikiano, kufanya kazi kwa weledi, kwa kujituma na kutambua kwamba zoezi hili ni nyeti na ni la umuhimu kwa kuwa ni mfumo wakuhakikisha Serikali inatimiza wajibu wake wa kukuza na kulinda haki za binadamu kwa wananchi wake.
Aidha, alizitaka asasi zisizo za Serikali kuweka mfumo mzuri wa kufuatilia masuala ya haki za binadamu katika Halmashauri hadi Serikali kuu na kutatua changamoto zilizokuwepo kwenye mpango kazi wa kwanza wa haki za binadamu. Kabla ya kuandaliwa kwa rasimu hii ya mpango kazi wa pili wa haki za binadamu maoni mbalimbali yalikusanywa kutoka kwa wadau katika mikoa mbalimbali Tanzania Bara na Visiwani na hivyo Naibu Katibu Mkuu alikitaka kikosi kazi hicho kuweka vizuri mawazo hayo kutoka kwa wananchi ili kupata mpango kazi ulio mzuri kwa Taifa.
Kikosi kazi hiki cha wataalam kimeundwa ili kupitia muongozo wa kisera unaolenga kutatua changamoto mbalimbali zilizojitokeza kwenye mpango kazi wa kwanza ambao ulikosa vipaumbele vya msingi.