NA EMMANUEL MBATILO
Kupungua kwa kasi ya Maambukizi ya Virusi vya Corona vimepeleka Maonesho ya 44 ya sabasaba ya mwaka huu kufanyika lakini kwa utaratibu maalumu uliowekwa na Wizara ya Afya kwaajili ya kujikinga na kusambaza maambukizi ya Virusi hivyo.
Ameyasema hayo leo Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Mhandisi Stella Manyanya alipotembelea viwanja vya Maonesho vya Mwalimu Nyerere na kujionea maandalizi ya Maonesho ya 44 ya sabasaba ambayo yanatarajia kuanza Julai 1 mwaka huu.
Akizungumza katika maonesho hayo Mhe.Stella amesema kuwa Wataweka utaratibu ambao utasaidia kuhakikisha wafanyabiashara wanajikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona pia na kuhakikisha wanatengeneza mazingira mazuri kwaajili ya dharura zitakozojitokeza.
“Maonesho haya yataendeshwa chini ya muongozo maalumu ambao utatolewa na wizara ya afya kuhakikisha kwamba tunafuata taratibu zote zinazotuwezesha kufanya shughuli zetu za kibiashara lakini wakati huo kuhakikisha kwamba tunaendelea kujilinda na maambukizi ya virusi vya Corona”. Amesema Mhe.Stella.
Hata hivyo Mhe.Stella amesema wamelenga kuyasajili makampuni yatakayofanya biashara kwenye maonesho hayo takribani 3600 lakini mpaka sasa wapo kwenye 75% na wengi wao ambao wamejitokeza kujisajili ni makampuni ya ndani huku makampuni ya nje ni machache ambayo yamekuwa yakifanya kazi hapa nchini .
Aidha amewataka wananchi wote kujitokeza kwa wingi ambao wamekuwa wakitengeneza bidhaa nzuri na wangependa bidhaa zao ziweze kutambulika na kufahamika ili waweze kuendelea kufanya biashara hata baada ya maonesho wafike na waendelee kujisajili Sabasaba.
Amesema watajidhatiti kuonesha maonesho kwanjia ya mtandao kwani kuna mazao kama mpunga na mahindi yamepatikana kwa wingi hapa mchini hivyo mazao hayo yatatangazwa kwa njia ya mtandao.
Pamoja na hayo Mhe.Stella amesema kutakuwa na mikutano kati ya wazalishaji na watu wateknolojia katika mazao hasa ya korosho,Kahawa,katani na mazao mengine mbalimbali hivyo kutakuwa siku ya kubadilishana mawazo kwa wafanyabiashara hao kati ya wazalishaji pamoja na watengenezaji wa teknolojia mbalimbali.
Kutakuwa na onesho la kipekee litakalo kwenda kwa jina la mvinyo na Mkeka kwaajili ya kutangaza mvinyo inayotengenezwa hapa nchini.