Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Bi. Sarah Msafiri akiongea na wadau wa Mafuta na gesi (ambao hawapo pichani), Kikao kilichofanyika Ofisi za Mkuu wa Wilaya Kigamboni kwaajili ya kujadiliana masuala ya usalama na afya mahali pa kazi kwa wanyafanyakazi wa sekta hiyo.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA Bi Khadija Mwenda akiongea kwenye Kikao na wadau wa mafuta na gesi, kwenye kikao cha Kujadiliana masuala ya utekelezaji wa masula ya usalama na Afya kwenye sekta hiyo, kilichofanyika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Jijini Dar es salaam,
Baadhi ya washiriki wa kikao cha wadau wa mafuta na gesi Wilayani Kigamboni wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya kigamboni wakati wa ufunguzi wa kikao kazi baina yao na Uongozi wa OSHA.
*******************************
Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Bi. Sarah Msafiri, ameyataka makampuni yanayojishughulisha na biashara ya mafuta na gesi kuimarisha mifumo ya kulinda afya na usalama wa wafanyakazi ili kuepuka athari zinazoweza kutokea endapo hakutakuwa na mifumo hiyo.
Ameyasema hayo alipofungua kikao cha mashauriano baina ya wadau wa sekta ya mafuta na gesi na menejimenti ya Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kilichofanyika katika ofisi ya Mkuu huyo Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
“Tunaweze kukwepa vyote lakini hatuwezi kukwepa suala la usalama kwenye uendeshaji wa shughuli hizi na kwa bahati mbaya sana usalama huu hauwezi kusema wewe unajilinda kwa asilimia mia moja lakini wenzako waliokuzunguka hawana mifumo ya kujikinga kwa kiwango hicho, itakuwa ni kazi bure, kwasababu ajali ikitokea katika kampuni moja itasababisha madhara kwa makampuni mengine ya karibu au katika wilaya yote na ikiwezekana hata Dar es Salaam nzima inaweza kuathirika,” alisema Bi. Msafiri.
Mkuu huyo wa wilaya amewasisitiza wawakilishi wa makampuni ya mafuta na gesi waliohudhuria kikao kuwashauri viongozi wao wa juu katika makampuni yao kuwekeza katika masuala usalama na afya ili kuwalinda wafanyakazi pamoja na mali za wawekezaji.
Aidha, Bi. Msafiri alisema uwekezaji katika usalama na afya una faida nyingi ikiwemo kuongeza morali miongoni wafanyakazi, kuongeza ubora wa bidhaa na huduma na hivyo kuleta tija katika uzalishaji kwa manufaa ya wawekezaji na serikali kupitia mapato ya kodi.
Akizungumza baada ya kuhitimisha kikao hicho, Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema madhumuni ya kikao ni kujenga uelewa wa pamoja kuhusu sheria na kanuni mbali mbali kuhusu afya na usalama kazini miongoni wadau wa sekta ya mafuta na gesi.
“Katika kikao hiki tutajadili mambo mbali mbali kuhusu usalama na afya katika sekta ya mafuta na gesi na kikubwa zaidi ni kwamba tutapata mrejesho wa namna ambavyo wadau wetu wamekuwa wakisimamia masuala ya usalama na afya na jinsi ambavyo kaguzi zetu katika maeneo hayo zimekuwa zikifanyika. Na kimsingi katika utekelezaji wa sheria yoyote ile msimamizi na watakelezaji wanapaswa kuwa na uelewa wa pamoja ili sheria husika iweze kutekelezeka,” alieleza Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA.
Baadhi ya washiriki wa kikao hicho akiwemo Leah John kutoka Kampuni ya Tipper na Bw. Moses Mgeni wa kampuni ya MOGAS wameishukuru serikali kupitia OSHA kwa kuandaa kikao hicho ambapo wamesema imekuwa ni fursa muhimu kwa pande zote mbili (OSHA na wadau) kujadiliana masuala ya msingi ambayo yatasaidia kuboresha mifumo ya usalama na afya katika sekta ya mafuta na gesi ambayo shughuli zake ni hatarishi zaidi kiusalama na afya.
OSHA ni taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu ambayo in jukumu la kusimamia Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake ambazo zina lengo la kuwalinda wafanyakazi dhidi ya ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.