…………………………………………………………………………………
~ Yapokea viti na meza 1,160
~ Ukaguzi maandalizi ufunguzi shule waendelea vyema
Na Mwandishi wetu Mihambwe
Changamoto ya uhaba wa Madawati kwa meza na viti imemalizwa kwa shule za Sekondari za Tarafa ya Mihambwe ambapo imepata jumla ya meza na viti 1160 kwa mchanganuo wa meza 580 na viti 580.
Hayo yamebainishwa wakati wa ziara ya ukaguzi maandalizi ya ufunguzi wa shule za msingi na Sekondari ambapo Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu alikagua miundombinu ya shule, meza na viti vipya vya shule mbalimbali za Sekondari na akapata fursa ya kuzungumza na Wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Mweminaki iliyopo kata ya Kitama.
“Shule zinafunguliwa Jumatatu Juni 29, 2020 Wanafunzi mjiandae vyema kuendelea na masomo yenu baada ya likizo ya dharura huku mkiendelea kuchukua tahadhari zote za kujikinga na Corona nyakati zote. Wazazi wote wahakikishe wanawapeleka Watoto wao kuendelea na masomo. Pia tumepokea meza na viti kwa ajili ya kusomea jitahidini mzitunze vyema.” Alisisitiza Gavana Shilatu.
Katika ziara hiyo Gavana Shilatu aliambatana na Maafisa Elimu Kata, uongozi wa Kata, uongozi vijiji husika na uongozi wa shule ambapo alishuhudia maandalizi ya usafi wa mazingira nje na ndani ya Madarasa tayari kuanza tena kwa masomo siku ya Jumatatu Juni 29, 2020.