Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Chama cha Mapinduzi(UVCCM), Ndugu Kheri James akizungumza na wanadodoma katika uzinduzi wa Tawi la Wakereketwa CCM Chato katika kata ya Uhuru Dodoma Mjini
Mbunge wa Dodoma Mjini Anthony Mavunde akizungumza na wanadodoma katika uzinduzi wa Tawi la Wakereketwa CCM Chato katika kata ya Uhuru Dodoma Mjini.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Chama cha Mapinduzi(UVCCM), Ndugu Kheri James akiwa na Mbunge wa Dodoma Mjini Mhe. Anthony Mavunde wakikata utepe kuashiria uzinduzi wa Tawi la Wakereketwa CCM Chato katika kata ya Uhuru Dodoma Mjini
Baadhi ya Wanachama waliyo jitokeza katika uzinduzi wa Tawi la Wakereketwa CCM Chato katika kata ya Uhuru Dodoma Mjini
Wanachama katika katika uzinduzi wa Tawi la Wakereketwa CCM Chato katika kata ya Uhuru Dodoma Mjini wakipata burudani
Mbunge wa Dodoma Mjini Anthony Mavunde akiburudika na wapiga kura wake katika uzinduzi wa Tawi la Wakereketwa CCM Chato katika kata ya Uhuru Dodoma Mjini
Msanii wa mziki wa kizazi kibya (Bongo fleva) Dotto akitoa burudani katika uzinduzi wa Tawi la Wakereketwa CCM Chato katika kata ya Uhuru Dodoma Mjini
………………………………………………………………………………………….
Na. Majid Abdulkarim, Dodoma
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi(UVCCM), Kheri James amezindua Shina la Wakereketwa wa CCM Chato lililopo kata ya Uhuru Dodoma Mjini huku akiwaomba watanzania na wakazi wa Dodoma kuendelea kumuunga mkono Rais Dk.John Magufuli ili kuwaletea maendeleo ya kiuchumi.
Kauli hiyo ameitoa leo alipokuwa akizindua Shina hilo lenye jina la eneo ambalo amezaliwa Rais Magufuli.
Amesema watanzania wana kila sababu ya kutembea kifua mbele kujivunia mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wake na kumpa miaka mitano mingine ili aendelee kulipaisha Taifa kiuchumi.
Amewatahadharisha watanzania kujiepusha na upotoshaji unaofanywa na wanasiasa hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 2020.
“Kuna wengine wameanza kuzusha maeneo ya kuonesha kama nchi haipo salama wakati si kweli na watanzania ni mashahidi, nawasihi kuendelea kufanya kazi kwa kutumia mazingira wezeshi waliyotengenezewa na serikali yenu kama mlivyoipa dhamana ya kuwatumikia,”amesema.
Ametoa wito kwa watanzania wasikubali kuchafuliwa hadhi ya maeneo yao na viongozi wa siasa kwa kusema kuwa hakuna usalama.
“Huwezi kuangushwa na Faru John Mkubwa ukasingizia kuwa umeshambuliwa ili kutafuta umaarufu hivyo watanzania msikubali viongozi wa siasa kuchafua miji yenu nyinyi endelea kuchapa kazi ili kuleta maendeleo ya katika maeneo yenu,” ameeleza.
Sambamba na hilo, amewashauri viongozi wa serikali kutowapa umaarufu viongozi wa siasa kwa kuwakamata kwa kuwa kitendo hicho kinawapa kiki ya kisiasa kwa kupiga kelele hovyo.
“Mwaka huu hawatatoboa hawana hoja za kuwasilisha kwa watanzania kwani serikali iliyoko madarakani imekamilisha hoja zote kwa asilimia 100, hivi kweli mtu ufanye mkutano Dar es salaam sijui wapi ukaenda Lindi Kilwa ukaleta chokochoko zako unasema serikali hii inanyanyasa wapinzani, kwanini hawakukuzuia huko kote, wamekosa hoja,”amesema.
Amewataka watanzania katika uchaguzi mkuu kuchagua viongozi bora na si wanaotumiwa na mabeberu.
“Kuna mtu nasikia anachukua fomu sijui jumatatu mara ooho ana vigogo sita hata uwe na vijiti, hivi kweli kuna mtu wa kushindana na Rais Magufuli,”amesema.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini,Anthony Mavunde ameweka wazi kuwa kwa kile anachokiona katika ngazi ya shina ni zaidi ya ukienda katika tawi hivyo ni ishara tosha kuwa wanadodoma wako tayari kufanya maajabu ifikapo Oktoba 2020 katika kusimika mafiga matatu ya CCM kama ilivyo kauli mbiu ya Magufuli miaka mitano tena.
Mavunde amesema kuwa serikali inayoongozwa na Rai Magufuli imefungua mtandao wa barabara katika jimbo hilo hasa kwa kuleta barabara ya mzunguko hivyo yeye kama mbunge ameahidi kila ambapo barabara hiyo itapita atahakikisha wananchi wa maeneo husika wanapata huduma za afya na gari ya wagonjwa ili kusogeza huduma za afya kwa wananchi wake.
“ Naomba nifikishie salamu kwa Rais Magufuli kuwa wanadodoma wanashukuru kwa kuleta maendeleo makubwa hivyo shukrani zetu ni kufanya maajabu makubwa ya kumrudisha Mhe. Magufuli kwa kumpa kura za kutosha kwa asilimia 100 pale itakapo fika Oktoba 2020,” amesema Mavunde.
Mavunde ambaye pia ni Mlezi wa shina hilo ameahidi kuboresha miundombinu katika shina hilo ili wanachama katika shina hilo waweze kupata Habari mbali mbali kwa kuwekewa Runinga na kukaa ili kupanga mipango ya kuleta maendeleo katika maeneo yao kwani shina hilo ni kitovu cha maendeleo katika kata hiyo ya Uhuru.