Waziri wa Ardhi Nyunba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akiangalia bango linaloonesha uzinduzi wa Ofisi ya Ardhi mkoa wakati wa hafla fupi ya kuzindua ofisi hiyo mkoa wa Tanga jana, Kulia kwa Waziri wa Ardhi ni Katibu Mkuu Mary Makondo na wa tatu kulia ni Mkuu wa mkoa wa Tanga martine Shigela.
Muonekano wa Ofisi mpya ya Ardhi mkoa wa Tanga ambayo imezinduliwa rasmi jana na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi.
Baadhi ya Wananchi waliohudhuria hafla fupi ya uzinduzi wa Ofisi ya Ardhi mkoa wa Tanga uliofanywa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi jana.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza katika hafla fupi ya kuzindua ofisi ya ardhi mkoa wa Tanga jana. Wa pili kulia ni Waziri wa Afya Ummy Mwalimu na wa pili kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Tanga Martine Shigela na kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Mary Makondo.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo akizungumza wakati wa halfa ya uzinduzi wa ofisi ya ardhi mkoa wa Tanga uliofanywa na Waziri wa Ardhi William Lukuvi jana.
Mkuu wa mkoa wa Tanga Martine Shighela akizungumza wakati wa halfa ya uzinduzi wa ofisi ya ardhi mkoa wa Tanga uliofanywa na Waziri wa Ardhi William Lukuvi jana.Kulia kwa mkuu wa mkoa ni Katibu Tawala mkoa wa Tanga Judica Omari.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akimkabidhi mmoja wa wananchi wa mkoa wa Tanga Hati ya umiliki ardhi jana wakati wa hafla fupi ya kuzindua ofisi ya ardhi mkoa wa Tanga jana. Kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Tanga Martine Shigela.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi (kulia) Mkuu wa mkoa wa Tanga Martine Shigela (wa pili kulia), Katibu Tawala mkoa wa Tanga Judica Omari (aliyevaa miwani) na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Mary Makondo (kushoto) wakiangalia samani za ofisi ya ardhi mkoa wa Tanga iliyozinduliwa jana
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akiwa katika picha ya pamoja na wananchi wa mkoa wa Tanga waliokabidhiwa Hati zao za umiliki wa ardhi wakati wa hafla ya uzinduzi wa ofisi ya ardhi mkoa wa Tanga jana.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Makatibu Tawala wa wilaya za mkoa wa Tanga (waliosimama mbele) wakati wa hafla ya uzinduzi wa ofisi ya ardhi mkoa wa Tanga jana.
Mbunge wa Jimbo la Lushoto Shabani Shekilindi (Bosnia) akizungumza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi ofisi ya ardhi mkoa wa Tanga jana.
Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Tanga Tumaini Gwakisa akitoa maelezo mafupi kuhusiana na ofisi yake wakati wa hafla ya uzinduzi wa ofisi ya ardhi mkoa wa Tanga uliofanywa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi jana (PICHA ZOTE NA HASSAN MABUYE WIZARA YA ARDHI).
……………………………………………………………………………………
Na Munir Shemweta, WANMM TANGA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeeo ya Makazi William Lukuvi ameagiza kutolewa Hati za umiliki wa ardhi ndani ya wiki pamoja pale mwananchi atakapokuwa amekamilisha taratibu zote za umilikishwaji ardhi.
Aidha, ameagiza wananchi kupatiwa hati zao za ardhi katika halmashauri waliolipia gharama za kupatiwa hati ili kuondoa usumbufu pamoja na gharama kwa mwananchi kufuatilia Hati kwenye Ofisi za Ardhi za mikoa.
Lukuvi alitoa agizo hilo jana wakati akizindua ofisi ya ardhi mkoa wa Tanga katika hafla fupi iliyofanyika jijini Tanga. Uzinduzi wa Ofisi hizo ulihudhuriwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo, Mkuu wa mkoa wa Tanga Martine Shighela, Kamishna wa Ardhi nchini Nathaniel Nghode, Katibu Tawala mkoa wa Tanga Judica Omari, Wakuu wa wilaya za mkoa wa Tanga pamoja na viongozi wa taasisi mbalimbali za mkoa wa Tanga.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, wizara yake imekamilisha ndoto za Rais John Pombe Magufuli za kuondoa usumbufu kwa wananchi kupata hati za ardhi pamoja kufuata huduma za ardhi umbali mrefu na kutolea mfano kuwa, mwananchi wa mkoa wa Tanga alilazimika kuifuata huduma ya ardhi mkoani Kilimanajaro.
‘’Umekamilisha taratibu zote za kupatiwa Hati hapa Tanga, unaambiwa ukachukue Moshi ilipo ofisi ya Kanda, Rais ameliona hilo maana gharama za ufuatiliaji ni kubwa kuliko hata ghrama ya kulipia hati yenyewe’’ alisema Lukuvi.
Aliwataka Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuhakikisha pale hati za maeneo yao zinapokamilika wamfuate Msajili Msaidizi wa Hati katika ofisi ya ardhi ya mkoa kwa lengo la Msajili huyo wa Hati kwenda kuzikabidhi hati hizo kwa wahusika kwenye halmashauri badala ya wananchi kuzifuta mkoani.
Kwa mujibu wa Lukuvi, kumbukumbu zote za ardhi katika mkoa zilizokuwa ofisi za Kanda nazo zimepelekwa mikoa husika na kutolea mfano kumbukumbu za mkoa wa Tanga ambazo awali zilikuwa zikihifadhiwa Dar es salaam na baadaye kuhamishiwa Moshi, Kilimanjaro sasa zimetunzwa Ofisi ya ardhi mkoa wa Tanga.
Alizitaja baadhi ya kumbukumbu zilizo katika Ofisi ya Ardhi mkoa wa Tanga kuwa, ni pamoja na Michoro zaidi ya 1,026, Ramani 5,400 pamoja na Hati 18,460 na kusisistiza kuwa hati pamoja na nyaraka nyingine zimetunzwa vizuri na wamiliki wake wanaweza kukopesheka bila matatizo yoyote.
Waziri Lukuvi aliongeza kwa kusema, tangu kufunguliwa kwa ofisi mpya ya ardhi mkoa wa Tanga tayari Hati zaidi ya 300 zimeandikwa na kusajiliwa kwenye mkoa na kusisitiza kuwa, uanzishwaji ofisi za ardhi kwenye mikoa siyo tu utaondoa usumbufu wa kufuatilia hati bali utapunguza pia migogoro ya ardhi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo alisema, jitihada zilizofanywa na serikali kuanzisha ofisi za ardhi za mikoa zina lengo la kumpunguzia mwananchi usumbufu wa kufuata huduma ya sekta hiyo umbali mrefu ambapo huduma hiyo ilikuwa ikipatikana ofisi za kanda na kila kanda ilikuwa ikihudumia mikoa mitatu au zaifi.
Alisema, Serikali kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi inakusudia ardhi yote nchini ipangwe, kupimwa na kumilikishwa ili wananchi waweze kupewa miliki huku hatua hiyo ikilenga pia kupunguza migogoro ya ardhi nchini.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigela amewataka wakurugenzi wa halmashauri za mkoa wake kuhakikisha wanaitumia vyema fursa ya uwepo ofisi za ardhi za mkoa katika kuwawezesha waanchi kupata hati zao kwenye eneo la halmashauri husika badala ya kwenda mkoani sambamba na kutatua migogoro ya ardhi kwa kutumia wataalamu waliopo ofisi ya ardhi ya mkoa.