Jengo jipya la mahakama ya hakimu mkazi Simiyu ambalo pia linajumuisha mahakama ya wilaya ya Simiyu lililozinduliwa jana na Jaji Kiongozi wa mahakama kuu ya Tanzania Mhe.Dkt.Eliezer Feleshi
Jaji Kiongozi wa mahakama kuu ya Tanzania Mhe.Dkt.Eliezer Feleshi,akikata utepe wa kuzindua jengo jipya la mahakama ya hakimu mkazi Simiyu ambalo pia linajumuisha mahakama ya wilaya ya Simiyu.
Jaji Kiongozi wa mahakama kuu ya Tanzania Mhe.Dkt.Eliezer Feleshi,akifunua pazia kuashiria uzinduzi wa jengo jipya la mahakama ya hakimu mkazi Simiyu ambalo pia linajumuisha mahakama ya wilaya ya Simiyu.
…………………………………………………………………………………
Na Lydia Churi- Mahakama Simiyu
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi amesema uzuri wa majengo ya Mahakama yanayojengwa hivi sasa hauna budi kuambatana na upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.
Akizindua jengo jipya la Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu pamoja na Mahakama ya wilaya ya Bariadi, Jaji Kiongozi pia amewataka watumishi wa Mahakama nchini kubadili mienendo na tabia zinazokiuka miiko na maadili ya kazi na Utumishi wa Umma ili waweze kutoa huduma kwa ubora unaostahili.
“Natoa Rai kwa viongozi wote kuhakikisha kwamba watumishi wote wa Mahakama wanatoa huduma nzuri zinazoendana na uzuri wa majengo, tujiepushe na lugha zisizofaa kwa wateja wetu ambao ni wananchi na wadau, tujiepushe na vitendo vya rushwa kwani rushwa ni adui wa haki”, alisema.
Alisema Mahakama haitasita kumchukulia hatua kali za kinidhamu na kisheria mtumishi yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vya rushwa. Aliwaomba Wakuu wa Mikoa na Wilaya kupitia kamati za Maadili ya Mahakimu kuwaelimisha wananchi kutumia kamati hizi kuwasilisha malalamiko ya mienendo isiyofaa kwa baadhi ya Mahakimu wanaokiuka maadili wanapotekeleza majukumu yao ya msingi ya utoaji haki.
Jaji kiongozi alisema uwepo wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu ni nafuu na ukombozi kwa wananchi wa Simiyu kwani awali walikuwa wakisafiri umbali wa kilometa 140 kwenda mkoani Shinyanga kufuata huduma za Mahakama. Alisema umbali huo mrefu uliwaathiri kwa kutumia muda wao mwingi kutafuta haki na pia wengine waliikosa haki kwa kukata tamaa na kushindwa kumudu gharama za kujikimu kwenda mkoani Shinyanga.
Kwa mujibu wa Jaji Kiongozi, moja ya mikakati iliyowekwa naMahakama ni kuhakikisha kila eneo jipya la kiutawala linapoanzishwa inajengwa Mahakama kwa kuwa huduma za Mahakama ni muhimu kama ilivyo huduma nyingine za Umma.
Wakati huo huo, Jaji Kiongozi amewaomba wakuu wa mikoa nchini kuwezesha Magereza mikoani mwao kwa kuipatia vifaa vya Tehama kwa ajili ya mikutano Mtandao (Video Conference) ili kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Mahakama ya Tanzania za kusikiliza mashauri kwa njia hiyo.
Jaji Kiongozi amesema Mahakama tayari imeweka mifumo ya Tehama kwenye mikoa mbalimbali nchini kwa ajili ya kufanya mikutano mtandao na endapo wadau hao wa Mahakama wataiwezesha Magereza, kazi hiyo itafanyika kwa urahisi.
“Wakati Mahakama imejaribu kwa kiasi inachoweza kupeleka vifaa vya Tehama kwenye baadhi ya Magereza, Mahakama sasa haiwezi kwasababu hatukuwa na bajeti, wadau wetu mtuunge mkono kuwezesha Magereza kuwa na vifaa hivyo”, alisema Jaji Kiongozi.
Alisema Magereza inakabiliwa na changamoto ya bajeti kwa ajili ya kununua vifaa hivyo pamoja na vitendea kazi vingine yakiwemo magari ya kuwasafirishia mahabusu na wafungwa kwenda mahakamani kwa ajili ya rufaa. Aliongeza kuwa baadhi ya wadau, huku akimtolea mfano Mkuu wa Mkoa wa Mbeya tayari wamepeleka vifaa vya Tehama kwenye Magereza.
Jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu lililozinduliwa ni la kisasa na shughuli nyingi za kimahakama zitatumia mifumo ya Tehama baada ya kuunganishwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambao utarahisisha matumizi hayo. Jengo hilo pia linajumuisha Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama ya wilaya pamoja na ofisi za wadau kama vile Waendesha Mashitaka, Ustawi wa Jamii, na Mawakili wa kujitegemea ambao wametengewa vyumba vya ofisi.