**************************************
NA ANDREW CHALE, ZANZIBAR.
MJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM, Hashim Salum Hashim amekuwa Kada wa 24 kuchukua fomu ya kupata ridhaa ya chama chake ya kuwa Rais wa Zanzibar.
Hashim Salum Hashim aliwasili majira ya saa Sita mchana na kisha kuchukua fomu hiyo na baadae alioata kuongea na waandishi wa Habari.
Akizungumza alisema:
“Nimekuwa Mwana CCM kwa muda mrefu na kwa miaka 15 nimeweza kuwa katika nyadhifa za kichama hadi sasa ikiwemo Mjumbe wa Mkutano mkuu wa CCM mkoa wa Mjini Magharibi.
Pia nafasi ya Katibu Mwenezi Wadi ya Kisima majongoo na Katibu uchumi na fedha tawi la Kikwajuni na zingine mbalimbali.” Alisema
Aidha, amesema amesukumwa kuchukua fomu kwa sababu nia anayo na nguvu anayo hivyo atanataka kuendeleza pale alipoishia Dkt. Ali Mohammed Shein.
“Ninataka kuhakikisha nafikia malengo katika sekta ya Afya, Jamii na kiuchumi.
Dkt. Shein amefanya mambo mengi sana. Nitakapopata nafasi nitaendeleleza yale yote aliyoanza na pia kuendeleza ikiwemo michezo.” Alisema.
Hashim Salum Hashim pia ni mdau mkubwa wa michezo ambapo ameaahidi kufikisha mbali katika michezo ikiwemo kuwa Mwanachama wa Shirikisho la soka la Dunia FIFA.
Wengine waliokwisha chukua fomu ni pamoja:
Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Mmanga Mjengo Mjawiri,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohammed Aboud Mohammed na Waziri wa Vijana na Michezo, Balozi Ali Karume.
pia wamo: Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masaun Yusuf, Waziri wa Mambo ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi na Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa.
Pia wamo: Aliewahi kuwa Waziri wa Habari, Utalii na Utamaduni Zanzibar, Rashid Ali Juma, Aliyekuwa Waziri wa Fedha na Mipango wa Zanzibar, ambaye ni Mwakilishi wa jimbo la Donge, Dkt. Khalid Salum Mohamed na Aliyewahi kuwa Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha.
Pia wamo: Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayub Mohammed Mahmoud,Hamis Mussa Omary,
Bakari Rashid Bakari na Mwakilishi wa jimbo la Mtoni na Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano, kupitia nafasi tano za Uwakilishi, Hussein Ibrahim Makungu maarufu “Bhaa’.
Pia wamo: Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salum Jecha, Mwanamama, Mwatum Mossa Sultan, Haji Rashid Pandu na Dkt. Abdulhalim Mohammed Ali.
Pia wamo: Mohammed Jafari Jumanne, Mohammed Hija Mohammed, Balozi Meja Jenerali Mstaafu, Issa Suleiman Nassor, Mbwana Bakari Juma, Mbwana Yahaya Mwinyi na Omary Sheha Mussa.
Tukio la kukabdhiwa fomu linatarajiwa kufungwa rasmi 30 Juni huku fomu hizo zikitolewa kwa kulipiwa Milioni moja zoezi zima likisimamiwa na Katibu wa Idara ya Organization CCM, Zanzibar, Cassian Galos.