Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiongoza kikao cha Kamati ya Usimamizi wa Mradi wa Udhibi,ti wa Sumukuvu kilichoshirikisha wizara za Kilimo,Mifugo,Viwanda,Tamisemi toka Tanzania Bara na Zanzibar leo mjni Morogoro.
Sehemu ya wajumbe wa kikao cha Kamati ya Kusimamia Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu nchini kilichoanyika leo mkoani Morogoro.
Wataalam toka wizara na taasisi zinazohusika na udhibiti wa Sumukuvu nchini wakiwa kwenye kikao cha kamati ya usimamizi wa mradi wa kudhibiti sumukuvu mjini Morogoro leo.
……………………………………………………………………………………
WADAU wa usalama wa chakula nchini wametakiwa kuisaidia serikali kutekeleza mradi mkubwa wa miaka mitano wenye lengo la kudhibiti tatizo la sumu kuvu ili ili kuboresha afya ya jamii kwa kuhakikisha taifa linazalisha na kuuza chakula salama na chenye kiwango cha ubora unaotakiwa kitaifa na kimataifa.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya wakati akifungua kikao cha pili cha kamati ya kusimamia mradi wa kudhibiti sumukuvu nchini (TANIPAC) kilichofanyika leo mkoani Morogoro.
Kikao hicho kinashirikisha pamoja na viongozi wa taasisi mbalimbali zinazotekeleza mradi pia wamo Makatibu Wakuu wanne kutoka wizara za Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Katibu Mkuu huyo alisema usalama wa chakula hapa nchini unategemea Kilimo kwa kiasi kikubwa, na kuongeza:” sote tunafahamu hakuna Taifa linalokuwa salama bila usalama wa chakula. Kwa kuzingatia umuhimu huo, tunalo jukumu kubwa la kuhakikisha kwamba tunaendelea kukipa Kilimo uzito unaostahili kwa kukabiliana na changamoto zinazojitokeza wakati wowote.”
Sekta ya Kilimo ndiyo inayoajiri zaidi ya asilimia 65 ya nguvu kazi na inachangia asilimia 30 ya pato la Taifa (GDP), huku ikichangia takriban asilimia 65 ya malighafi za viwandani na takribani asilimia 100 ya chakula kinachotumika ndani ya nchi.
“Napenda kumshukuru Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dk.John Pombe Joseph Magufuli, kwa uongozi wake mahiri katika kipindi hiki cha miaka mitano ambapo nchi imeendelea kuwa na utoshelevu wa chakula.” Alisema Katibu Mkuu Kusaya na kuongeza kuwa sasa ni wajibu wa wadau mbalimbali kuhakikisha chakula hicho ni salama.
Alisema watanzania wanapozungumza usalama wa chakula wanagusa sekta ya Kilimo ambao ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na jamii.
Alisema mojawapo ya changamoto hizo ni sumukuvu tatizo ambalo limekuwa likijirudia nchini Tanzania na hivyo kuifanyha serikali kuungana na wadau wengine kudhibiti hali hiyo.
“Kutokana na changamoto ya sumukuvu hapa nchini kwetu ambapo kwa taarifa nilizopata ni kuwa tatizo hili limekuwa likijirudiarudia kwa miaka mitatu mfululizo 2016, 2017, 2018 na 2019 utekeleaji wa mradi huu ni muhimu sana na hivyo nataka kila mmoja awajibike na sio wizara ya Kilimo pekee” alisema.
Mtaalamu wa Shirika la viwango nchini TBS, Dk Analyse Camara alisema kwamba tatizo la sumukuvu ni kubwa duniani na kwamba mtu anapotumia kiwango kikubwa cha sumu hiyo maisha yake yanakuwa hatarini, kufa au kwa watoto kudumaa.
Alisema uwepo wa sumukuvu ulitambulika duniani kwa takribani miaka 600 kabla ya kuzaliwa Kristo na kujulikana chanzo chake mwaka 1960 watu walipobaini uwapo wa sumu hiyo na athari zake kwa binadamu.
Alisema kuna sumukuvu aina 400 lakini yenye madhara makubwa ni ya Aflatoxin ambayo hukutwa katika nafaka aina ya mahindi na karanga.
Mradi wa TANIPAC wenye thamani ya dola za Marekani milioni 33.3 unajikita katika ujenzi wa miundombinu muhimu kama vile ujenzi wa maghala, uanzishwaji wa maabara kuu ya kilimo, kituo mahiri cha Usimamizi wa mazao ya Nafaka (“Postharvest Centre of Excellence for Grains”) na uimarishaji wa miundombinu ya kituo cha utafiti wa magonjwa ya Kabailojia-Kibaha.
Mradi huu unawekeza kwenye matumizi ya teknolojia sahihi kwa kuwashirikisha vijana ambao ndio muhimili wa uchumi.
Taasisi za VETA na SIDO, VTA na SMIDA kwa Zanzibar zitafundisha vijana 400 ili waweze kwenda kusaidia ujenzi wa vihenge vya kisasa vya kutunzia nafaka.
MWISHO
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Kilimo
MOROGORO
22 .06.2020