***************************
Na Masanja Mabula,PEMBA.
MAHAKAMA ya Mkoa wa Kaskazini Pemba imemrejesha rumande mtuhumiwa Hemed Mohammed Amour wa Daya Mtambwe wilaya ya Wete anayekabiliwa na kosa la kumlawiti wa mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 9.
Mtuhumiwa huyo mwenye umri wa miaka 20 alipanda mahakamani ambapo mwendesha mashtaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka wa serikaliMohammed Said Mohammed aliomba kesi hiyo ipangiwe siku nyengine kwa ajili ya utetezi.
“Mhe Hakimu kesi hii ipo kwa ajili ya utetezi, hivyo naomba upange siku nyengine”alishauri.
Hakimu wa Mahakama hiyo Abdalla Yahya Shamuhuna akiahirisha kesi hiyo alisema kesi hiyo itaendelea julai 6 mwaka huu kwani file lipo Chake Chake.
“File lipo Chake Chake hivyo kesi hii itaendelea tarehe 6/7/2020 na mtuhumiwa ataendelea kubaki rumande”alisema Shamuhuna.
Hata hivyo mtuhumiwa aliiomba mahakama impe dhamana akidai amekaa siku nyingi rumande ombi ambalo lilipingwa na upande wa mashtaka.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka inaeleza kwamba mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo tarehe 6/4/2019, majira ya saa nane na robo mchana ambapo alimlawiti mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 9 (jina tunalihifadhi) jambo ambalo ni kosa kisheria.
Kosa la kulawiti ni kinyume na kifungu cha 115(1) cha sheria ya adhabu namba 6/2018 sheria ya serikali ya mapinduzi ya Zanzibar.