Mabingwa wa kihistoria wa Tanzania bara timu ya Yanga imeshindwa kutamba mbele ya matajiri wa Chamazi Azam FC baada ya kugawana pointi moja kila moja kwa kutoka sare ya bila kufungana katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Mchezo ulikuwa mzuri zaidi kwa timu zote mbili kucheza kwa utulivu na ufundi wa aina yake kutokana na kuwa na viungo bora eneo la kati.
Hadi mwamuzi anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Heri Sasii aliyesaidiwa na Soud Lila na Mbaraka Haule wote Dar es Salaam wakimaliza mchezo hakuna aliyetoka na pointi tatu.
Kwa matokeo hayo, Azam FC inaendelea kushika nafasi ya pili ikifikisha pointi 58, na Yanga wakiendelea kushika nafasi ya tatu kwa pointi 56 baada ya wote kucheza mechi 30 sasa.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Metacha Mnata, Deus Kaseke, Jaffar Mohamed, Kelvin Yondan, Said Juma ‘Makapu’, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Haruna Niyonzima, Mapinduzi Balama/Mrisho Ngassa dk64, Ditram Nchimbi/Abdulaziz Makame dk79, Patrick Sibomana/Bernard Morrison dk46 na David Molinga/Yikpe Gislain dk64.
Azam FC; Benedict Haule, Nico Wadada, Salmin Hoza, Abdallah Kheri, Oscar Maasai, Mudathir Yahya, Iddi Kipagwile/Bruce Kangwa dk60, Bryson Raphael, Rochard D’jodi/Andrew Simchimba dk69, Never Tigere/Shaaban Iddi Chilunda dk60 na Iddi Suleiman ‘Nado’.