Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (kulia) akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Kelema alipofanya ziara ya kukagua zoezi la uwekaji wazi wa Daftari la Mpiga Kura pamoja na kuangalia uboreshaji wa taarifa za wapiga kura Wilayani Chemba.
Sehemu ya wakazi wa Kijiji cha Kelema wakifuatilia maelezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipofanya ziara wilayani Chemba.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (wa tatu kutoka kushoto) akinawa mikono kabla ya kuingia kwenye kituo cha uboreshaji taarifa katika daftari la mpiga kura Wilayani Chemba. Wa pili kutoka kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Mhe. Simon Odunga (kulia) ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chemba, Dkt. Semistatus Mashimba na wa pili kutoka kushoto ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Chemba Mhe. Zahara Michuzi.
Mkazi wa Kijiji cha Kelema Bw. Issa Kemu (kulia) akieleza jambo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama kuhusu utaratibu ulivyokuwa mzuri katika uboreshaji wa taarifa kwenye daftari la mpiga kura.
Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Mhe. Simon Odunga (kushoto) akieleza jambo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alipokuwa akikagua zoezi la uwekaji wazi daftari la wapiga pamoja na kuangalia uboreshaji wa taarifa za wapiga kura Wilayani Chemba.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akionyeshwa taarifa na wakazi wa Kijiji cha Kelema walioboresha taarifa zao kwenye daftari la mpiga kura alipokuwa kwenye ziara Wilayani Chemba.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akikabidhi kitambulisho cha Mpiga kura kwa Bi. Mwanamisi Mbuva mkazi wa kitongoji cha Mtungumu mara baada ya kuboreshwa kwa taarifa zake husika. Wa pili kutoka kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Mhe. Simon Odunga.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Chemba Mhe. Zahara Michuzi akieleza jambo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama kuhusu zoezi la uwekaji wazi wa Daftari la Mpiga Kura pamoja na uboreshaji wa taarifa za wapiga kura Wilayani Chemba. Kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chemba, Dkt. Semistatus Mashimba.
PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU
(KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)
OWM – KVAU
****************************
NA Mwandishi Wetu, Chemba
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ametoa pongezi kwa wananchi kwa hatua ya kujitokeza kwa wingi kwenye zoezi la uboreshaji wa taarifa kwenye daftari la wapiga kura ili waweze kushiriki katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu 2020.
Hayo yamelezwa na Waziri Mhagama alipofanya ziara wilayani chemba kujionea namna zoezi la uwekaji wazi wa Daftari la Mpiga Kura na jinsi taarifa za wapiga kura zilivyoboreshwa. Akiwa katika ziara hiyo alieleza kuwa tangu zoezi hilo la kuboresha taarifa lianze, imekuwa ni fursa kwa wananchi kuhakiki taarifa zao kwenye daftari hilo ikiwemo kufanya marekebisho kama vile majina, miaka ya kuzaliwa, na kuondoa taarifa za vifo.
“Uwekaji wazi wa daftari la wapiga kura ni wajibu wa kisheria na Tume ya Taifa ya Uchaguzi imekuwa ikitekeleza takwa hilo la kisheria kwa lengo la kuwawezesha wananchi kuboresha taarifa zao na hatua hiyo inaonesha utayari wao kushiriki kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu,” alisema Mhagama.
Alieleza kuwa kumekuwa na utaratibu wa daftari la mpiga kura kuboreshwa mara mbili toka uchaguzi ulioisha na uchuguzi unaofuata na utaratibu huo ni takwa kisheria. Tume ya Taifa ya Uchaguzi imehakikisha taratibu hizo zinafanyika.
“Awamu ya kwanza ya uboreshaji wa daftari la mpiga kura ilianza mwezi Julai mwaka 2019 na kuhitimishwa Februari 2020 huku awamu ya pili ilikuwa Aprili 2020 na ilihitimishwa Mei 2020 na baada ya hatua hizo daftari hilo huwekwa wazi,” alisema Mhagama.
Alifafanua kuwa Kifungu cha 11A cha Sheria ya Tume ya Uchaguzi sura namba 343 ya mwaka 2015, Tume hiyo ina wajibu wa kuweka wazi Daftari la wapiga kura ili wananchi waweze kuhakiki taarifa zao kama ziko sahihi, kutoa nafasi ya kufanya marekebisho kwa watu wenye matatizo au kama kuna makosa yalijitokeza, kutoa taarifa ya waliokufa ili waondolewe kwenye daftari na pia kuwapa nafasi wapiga kura kutoa mapingamizi dhidi ya mtu ambaye hana sifa kuwepo kwenye daftari.
Aliongeza kuwa kuelekea uchaguzi mkuu kumekuwa na ongezeko la wapiga kura waliojiandikisha ambapo jumla ya wapiga kura 29,804,992 wamejiandikisha wakati mwaka 2015 walikuwa 23,161,440.
Sambamba na hayo, Waziri Mhagama alitoa pongezi kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuweka mifumo mizuri ambayo imewawezesha wapiga kura kuhakiki taarifa zao kupitia tovuti ya tume hiyo ambayo ni www.nec.go.tz, kuwepo kwa kituo cha huduma kwa wapiga kura yaani “call center” na pia kwa kutumia simu ya kiganjani kwa kuandika ujumbe mfupi wa maneno kupitia *152*00#.
Aidha, Waziri Mhagama alitoa wito kwa wananchi kuwa wazalendo, kudumisha amani na utulivu wanapoelekea katika kipindi cha uchaguzi mkuu mwezi oktoba, 2020 na pia amewasihii kufuata sheria, taratibu na kanuni.
Kwa Upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chemba, Dkt. Semistatus Mashimba akitoa taarifa za takwimu juu ya zoezi la kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura alisema zoezi hilo limeenda vizuri na jumla ya wapiga kura 49,930 walijitokeza kuboresha taarifa zao kwenye daftari hilo la Mpiga Kura.
Naye Mkazi wa Kitongoji cha Mtungumu, Kata ya Paranga Bi. Mwanahamisi Mbuva ameishukuru Serikali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuwapatia wananchi fursa ya kuboresha taarifa zao kwenye daftari hilo pamoja na suala la uwekaji wazi wa daftari hilo ikiashiria demokrasia iliyopo nchini.
Katika ziara hiyo Waziri Mhagama alitembelea vituo vitatu kuangalia namna zoezi la uwekaji wazi wa Daftari la Mpiga Kura na jinsi taarifa za wapiga kura zilivyoboreshwa, kituo cha kwanza ambacho ni katika Kijiji cha Kelema kilichopo Kata ya Paranga, eneo la pili ilikuwa kitongoji cha Kidoka na alihitimisha ziara hiyo katika wilayani Chemba.
Zoezi la uboreshaji daftari la mpiga kura katika wilaya ya chemba awamu ya pili ilianza tarehe 17 Juni na kuhitimishwa Juni 20, 2020 na pia Jumla ya Vituo 274 vilikuwepo kwa ajili ya kuboresha taarifa za wakazi wa maeneo hayo.