Mwalimu Seleman Tyea Mwangu, akiwa amebeba maburungutu yake ya pesa baada ya kukabidhiwa. |
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi, akihutubia Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu Mkoani hapa. |
Mkuu wa TAKUKURU, Mkoa wa Singida, Adili Elinipenda (wa pili kulia) akizungumza kabla ya walimu hao hawajakabidhiwa fedha zao.
Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu mkoani hapa wakiwa kwenye mafunzo ya kupinga Rushwa ya Ngono yaliyoa andaliwa na TAKUKURU.
Maafisa wa TAKUKURU walioshiriki katika mafunzo.
Wanafunzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Mkoa wa Singida wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Mkuu wa TAKUKURU, Mkoa wa Singida, Adili Elinipenda akihutubia Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu Mkoani hapa.
Na Dotto Mwaibale, Singida.
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida imefanikiwa kuokoa sh.46,500,000/=Milioni za pensheni za walimu wawili waliodhulumiwa na mkopeshaji haramu.
Walimu hao waliodhulumiwa ni Loth Mwangu ambaye alikuwa anafundisha katika shule ya msingi Ilonga na Seleman Tyea ambaye alikuwa anafundisha katika Shule ya Msingi Endasiku zote za Wilaya ya Mkalama Mkoani hapa.
Akizungumza wakati wa kukabidhi fedha hizo kwenye ufunguzi wa Mafunzo ya kupinga Rushwa ya Ngono kwa Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu mkoani hapa kwa walimu hao ambazo walikabidhiwa na mkuu wa mkoa huo Dk. Rehema Nchimbi, Mkuu wa TAKUKURU, Mkoa huo Adili Elinipenda alisema taasisi hiyo Wilaya ya Mkalama ilipokea malalamiko kutoka kwa waalimu hao wastaafu waliokuwa wakilalamikia kudhulumiwa fedha zao za pensheni na mkopeshaji aliyejulikana kwa jina moja la Bhoke kupitia mikopo umiza.
Alisema Mwalimu Loth Mwangu alistaafu Julay 15 mwaka 2016, baada ya kustaafu alianza kukopa fedha kutoka kwa mkopeshaji huyo na kufikia jumla ya sh.9 Milioni kwa makubaliano ya kulipa kupitia fedha za pensheni atakazo lipwa na fedha hizo alikuwa akikopa kidogo kidogo kuanzia Julai hadi Desemba mwaka 2016.
Elinipenda alifafanua kuwa pensheni ya mwalimu huyo ilipotoka mkopeshaji huyo alimweleza mstaafu huyo kuwa anamdai jumla ya Sh.22,500,000/= kutokana na mkopo sawa na riba ya asilimia 215.
Aidha Mwalimu Seleman Tyea yeye alikopa sh.2,000,000/=kutoka kwa mkopeshaji huyo huyo kwa makubaliano ya kulipa kupitia fedha za pensheni ambazo alizikopa kuanzia mei hadi Desemba mwaka 2016 ambapo alistaafu may 16 mwaka 2016.
Baada ya pensheni mkopeshaji alimtaka Mwalimu huyo kulipa sh.24,000,000/=sawa na riba ya asilimia 1200.na mkopeshaji huyo alifanikiwa kumlipisha kiasi hicho kupitia Benki ya NMB Tawi la Singida.
Akizungumza baada ya kuwakabidhi fedha hizo walimu hao mkuu wa mkoa huo amewataka wakopeshaji haramu mkoani hapa kujisalimisha na wasipofanya hivyo mkono wa Takukuru na dola utawakuta na hakika hawatasalimika ni heri wajisalimishe kuliko kuwakuta huko waliko.
Baadhi ya wanafunzi walioshiri mafunzo hayo yaliyo andaliwa na TAKUKURU ya kupinga rushwa ya ngono kwenye vyuo, wamekiri kuwepo kwa vitendo hivyo lakini walikuwa hawajui malalamiko hayo wayapeleke wapi, kupitia mafunzo hayo wamepata uelewa na kwamba ikitokea hali hiyo watayaripoti mara moja malalamiko kwenye vyombo husika.