Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa (wa tatu kulia) akikagua matengenezo yaliyofanywa na Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Morogoro katika eneo la Kisegesa, Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro. Katikati ni Mkuu wa Kitengo cha Uhandisi kutoka TANROADS, Mhandisi Baraka Mwambage.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa akizungumza na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mlimba, Bw. Stephano Kaliwa, wakati walipokutana katika eneo la Kisegesa lililopata athari za mvua na kukata mawasiliano ya barabara kati ya wananchi wa Mlimba na Ifakara.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani), mara baada ya kukagua matengenezo yaliyofanywa na Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Morogoro katika eneo la Kisegesa, Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.
Mkuu wa Kitengo cha Uhandisi kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Morogoro, Mhandisi Baraka Mwambage (kushoto), akitoa maelekezo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, kuhusu hatua za matengenezo zinazoendelea katika mkoa wa Morogoro hasa maeneo yaliyopata athari kubwa za mvua
Muonekano wa sehemu ya barabara iliyofanyiwa matengenezo yenye urefu wa mita 24 katika barabara ya Ifakara – Taweta – Madeke (km 220) ambayo iliharibiwa na mvua na kukata mawasiliano kati ya wananchi wa Mlimba na Ifakara, mkoani Morogoro.
***********************************
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, amesema sasa Serikali iko katika hatua za kuunganisha mkoa wa Morogoro na mikoa jirani ya Njombe na Ruvuma kwa barabara ya lami ili kufungua mikoa hiyo yenye uzalishaji mwingi wa mazao, misitu na chakula.
Naibu Waziri huyo amezungumza hayo akiwa katika eneo la Kisegesa iliyopo katika Halmashauri ya Mlimba, Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro baada ya kukagua eneo lililokarabatiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS), ambalo lilipata athari kubwa za mvua zilizonyesha katika barabara hiyo na kukata mawasiliano kati ya wananchi wa Mlimba na Ifakara na hivyo kusababisha usumbufu kwa wasafirishaji.
“Niwatoe hofu wananchi wa maeneo haya na maeneo jirani kuwa Serikali yenu imejipanga kikamilifu kuhakikisha inapandisha uchumi wa mwananchi na Taifa hili kwa kuwaunganisha na barabara za lami siku zijazo”, amesisitiza Naibu Waziri Kwandikwa.
Amewahakikishia wananchi wa Kilombero na Mlimba kuwa Serikali itafanya marekebisho makubwa katika barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 220 kuanzia Ifakara hadi Madeke kwa kuwa sasa hivi kazi za usanifu zinaendelea kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami ili kuiunganisha na mkoa wa Njombe.
“Hizi hatua zinazoendelea za kukarabati ni kuhakikisha wananchi kwanza wanapita bila ya kupata usumbufu wowote lakini lengo la Serikali ni kuwaunganisha wananchi hawa kwa barabara za lami”, amefafanua Naibu Waziri huyo.
Kwandikwa ameelezea miradi ya ujenzi inayoendelea katika ukanda huo ikiwemo ya barabara ya kutoka Ifakara kuelekea Mikumi ambayo mkandarasi yupo eneo la mradi anaendelea na kazi na Serikali iko katika mpango wa kuunganisha mkoa wa Morogoro na Iringa kupitia Mlimba hadi Kilolo kwa barabara ya lami.
Katika kuunganisha mkoa wa Morogoro na Ruvuma Serikali imeshaifungua barabara hiyo kwa kuanza kuifanyika usanifu kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami kuanzia Lupilo kupitia Kilosa kwa mpepo hadi Namtumbo.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo ameelekeza Mameneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) wote nchini kutumia nafasi hii ambapo mvua zimesimama kukarabati maeneo yote yaliyoathirika na mvua na kukata mawasiliano kulingana na asili ya maeneo hayo kwa suluhisho la kudumu.
“Nimekuja kukagua na kutoa pole kwa wananchi wa maeneo haya hasa wa Mlimba na Taweta waliopata usumbufu kupitia barabara hii sasa inapitika na nimeagiza mkandarasi awe hapa kwa ajili ya ukarabati wa kudumu”, amesema Naibu Waziri huyo.
Awali akitoa taarifa kwa Naibu Waziri huyo Mkuu wa Kitengo cha Uhandisi kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Morogoro, Mhandisi Baraka Mwambage, ameeleza kuwa wameweza kufungua mawasiliano katika barabara hiyo kwa kuchukua hatua ya dharura lakini suluhisho la kudumu linakuja kwa kuanza sasa ujenzi wa maboksi kalvati yenye midomo mitatu itakayoweza kuhimili maji mengi katika eneo hilo.
Wakala wa Barabara mkoa wa Morogoro upo katika hatua za kufanya matengenezo makubwa ya barabara zenye urefu kilometa 80 ambazo zimeathirika na mvua nyingi zilizonyesha tangu mwaka jana na kuharibu miundombinu hiyo na sehemu nyingine kukata mawasiliano.