***********************************
Simba SC imezidi kujisogeza karibu na taji la tatu mfululizo la Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa 3-0 dhidi ya Mwadui FC kwenye mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es salaam.
Kwa ushindi huo, Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Sven Ludwig Vandenbroeck inafikisha pointi 75 baada ya kucheza mechi 30, ikiendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi 15 zaidi ya Azam Fc inayofuatia nafasi ya pili.
Katika mchezo wa leo, Simba wameishushia kipigo Mwadui cha mabao 3-0 huku wakicheza soka la kuvutia tofauti na ilivyokuwa katika mchezo wao wa kwanza ambapo walitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Ruvu Shooting.
Mabao ya Simba, mawili yalifungwa kipindi cha kwanza na Hassan Dilunga huku la pili beki wa Mwadui, Augustino Samson akijifunga baada ya kupigwa kwa pasi mpenyezo na Shomary Kapombe aliyepanda kushambulia.
Bao la tatu la Simba, lilifungwa na nahodha wa kikosi hicho, John Bocco baada ya shuti la Luis Miquissone kugonga nguzo na kumalizia kwa kichwa mpira ulioshiwa kutazamwa na kipa wa Mwadui, Mahmoud Amir.
Baada ya kupata mabao hayo matatu, Simba walifanya mabadiliko kwa kuwatoa, Bocco,Fraga,Kapombe, Dilunga na Luis nafasi zao wakaingia, Meddie Kagere, Francis Kahata, Cletous Chama, Yusuf Mlipili na Mzamiru Yassin.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe/ Yusuph Mlipili dk73, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Kennedy Juma, Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Gerson Fraga, Said Juma, John Bocco/ Meddie Kagere dk63, Luis Miquissone/ Clatous Chama dk63 na Hassan Dilunga/ Francis Kahata dk63.
Mwadui FC; Mahmoud Amour, Mfaume Omar, Yahya Mbegu, Joram Mgeveke, Augustino Simon, Frank John/ Mussa Chambenga dk56, Ottu Joseph, Enrick Nkhosi, Raphael Aloba/ Maliki Jaffary dk68, Gerlad Mdamu na Herman Masenga/Omar Daga dk21.
Coastal Union imelazimishwa sare ya 0-0 Mtibwa Sugar Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga na Polisi Tanzania imelazimishwa sare ya 1-1 na Lipuli FC Uwanja wa Ushirika mjin Moshi mkoani Kilimanjaro. Polisi ilitangulia kwa bao la Baraka Majogoro dakika ya 50 kabla ya Rashid Hassan kuisawazishia Lipuli dakika ya 63.