Rais wa Muungano wa klabu za Waandishi wa Habari(UTPC)Tanzania Deo Nsokolo kulia, akikabidhi vifaa mbalimbali vya kujikinga na ugonjwa wa Covid 19 unaosababishwa na virusi vya Corona ikiwemo Sanitizer,sabuni ya maji,na Barakoa kwa Mwandishi wa Habari wa kituo cha ITV Mkoani Ruvuma Emmanuel Msigwa wakati wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa Habari wa mkoa wa Ruvuma juu ya kujilinda,kutambua na kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo,mafunzo yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari wa mkoa wa Ruvuma.katikati Katibu msaidizi wa Chama hicho Ngaiwona Mkondola.
Picha na Mpiga Picha Wetu,
…………………………………………………………………………………..
Na Mwandishi Wetu,Ruvuma
RAIS wa muungano wa klabu za waandishi Tanzania(UTPC) Deo Nsokolo, ametoa wito kwa waandishi wa habari nchini kuipenda nchi yao,kuwa wazalendo na kuandika mambo mazuri yaliyofanywa na Serikali, badala ya kutumia kalamu zao kukosoa utendaji wa Serikali iliyopo madarakani.
Amesema hayo jana, wakati akiongea na waandishi wa Habari wa mkoa wa Ruvuma katika mafunzo ya kuwajengea uwezo, na jinsi ya kujilinda na ugonjwa wa mapafu makali Covid 19 unaosababishwa na virusi vya Corona, mafunzo yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Ruvuma.
Kwa mujibu wa Nsokolo, sio dhambi hata kidogo mwandishi wa habari kusifia na kupongeza kazi mbalimbali zilizofanywa na Serikali na kusisitiza kuwa,habari za kweli zitawafanya kuheshimiwa, kupendwa na jamii na Serikali.
Aidha Nsokolo, amewaasa waandishi, kuhakikisha wanashirikiana katika majukumu yao ya kila siku badala ya kuchukiana kutokana na tofauti zao za kipato na elimu.
Alisema, kama wana taaluma wanapaswa kuungana na kuepuka chuki baina yao kwani kutokana na unyonge wao, umoja miongoni mwao ndiyo silaha pekee itakayowasaidia kufikia malengo waliyonayo katika maisha yao ya kila siku.
Amewataka waandishi wa Habari hapa nchini kuboresha mahusiano yao na kuandika habari sahihi ambazo zitawezesha wananchi kupata taarifa hasa wakati huu Taifa linapokaribia kufanya uchaguzi Mkuu wa Madiwani,Wabunge na Rais.
Amewatahadharisha waandishi kujiepusha kuandika habari za uongo na zinazo chochea chuki dhidi ya mgombea au chama chochote cha siasa kwani kitendo hicho ni kosa kisheria.
Pia, amewasisitiza waandishi kuendelea kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa Corona kwa kuwa wao ni kati ya kundi kubwa linalokutana na watu wengi kila siku,hivyo ni muhimu kujiepusha na hatari ya kupata ugonjwa huo.
Amewaomba kuandika habari sahihi juu ya ugonjwa huo ili kuwasaidia wananchi kupata taarifa muhimu dhidi ya ugonjwa wa Covid 19.
Awali katibu wa chama cha Waandishi wa Habari mkoani Ruvuma Andrew Chatwanga alisema, chama hicho kimeandaa mafunzo hayo kama hatua ya kuwajengea uelewa waandishi wa habari juu ya ugonjwa wa Corona.
Alisema, waandishi ni watu ambao kila siku wanakutana na watu tofauti,kwa hiyo mafunzo hayo yatawasaidia namna ya kuepuka, kujikinga na kuchukua tahadhari ya kukabiliana na maradhi hayo.
MWISHO
Na Mwandishi Wetu,
Mpanda
WAKATI Joto la uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika mwezi Oktoba Mwaka huu likizidi kupambana moto hapa nchini,aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya wakala wa umeme vijijini(REA)Michael Nyagoga ametangaza rasmi kugombea ubunge jimbo la Serengeti mkoani Mara.
Nyagoga ambaye amewahi kuwa mjumbe wa bodi ya wakurugenzi wa taasisi mbalimbali hapa Nchini, ametangaza nia ya kugombea nafasi hiyo jana kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi jana mjini Mpanda.
Nyagoga, kwa sasa ni katibu Tawala msaidizi sekretalieti ya mkoa wa Katavi alisema, anataka kuwa mbunge wa jimbo la Serengeti ili kubadilisha maisha ya wananchi wa jimbo hilo ambao kwa muda mrefu wamekosa kupata mtu sahihi .
Alisema, kwa miongo kadhaa wakazi wa Serengeti wamewapa nafasi baadhi ya watu kuwakilisha, hata hivyo wameshindwa kuisaidia Serengeti kutatua changamoto zinazo wakabili kama miundombinu ya barabara,maji, umeme wa uhakika pamoja changamoto nyingine.
Alisema,sasa ni wakati muafaka kwa wana Serengeti kuchagua mtu mpya ambaye anaweza kusaidiana nao kutatua changamoto hizo ambazo zimechangia jimbo hilo kubaki nyuma kimaendeleo.
“mtu atakayepewa dhamana hiyo anapaswa kuwa mchapakazi,mwadilifu,mweledi, na mbunifu anayeheshimu wenzake,mwenye mahusiano mazuri na wadau wa maendeleo na kikubwa zaidi awe mtu anayepinga vitendo vya rushwa”alisema Nyagoga.
Nyagoga alitolea mfano kuwa, Serengeti ina watu wengi wenye sifa hizo akiwemo yeye binafsi ambaye ametaja sababu kubwa zilizomshawishi kufikia uamuzi huo wa kugombea Ubunge ni kwenda kuungana na wananchi kutatua kero zilizokuwepo kwa muda mrefu ili wilaya hiyo ipige hatua kimaendeleo kama ilivyo kwa maeneo mengine hapa nchini.
Anataja, changamoto ya kukosekana kwa barabara inayounganisha wilaya na makao makuu ya mkoa tangu Uhuru mwaka 1961,kutokuwepo kwa umeme wa uhakika na maji safi na salama ni kati ya kero kubwa ambazo zimechangia sana kudumuza maendeleo.
Aidha alisema, wabunge wote waliopewa dhamana kwa nyakati mbalimbali wameshindwa kuisaidia Wilaya ya Serengeti kutatua changamoto hizo akiwemo Mbunge anayemaliza muda wake Marwa Ryoba, ambaye awali alikuwa Chadema na baadaye kwa kulinda na kutetea maslahi yake akarejea Chama cha Mapinduzi.
Amewataka wana Serengeti kuchagua mtu mpya,mwenye mawazo mapya,maono mapya,mikakati,mipango mipya inayoendana na kasi ya sasa katika kutatua changamoto zinazokabili wilaya na jimbo la Serengeti.
Nyagoga anataja mafanikio ya miaka 28 katika utumishi wa umma akiwa wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi miaka 13,wizara ya fedha na mipango miaka 13 na Ofisi ya Rais Tamisemi miaka 5 ambayo ni ishara tosha kuonyesha jinsi alivyofanikisha alama za mafanikio katika kila kituo cha kazi.
Kwa mujibu wa Nyagoga, kazi hizo ni miongoni mwa kazi nyingi ambazo ameshiriki kuzisimamia na kuziratibu kwa mafanikio makubwa kuanzia maboresho ya Sera,maandalizi ya sheria na hatimaye maandalizi ya kanuni.
Ameeleza kuwa, dhamana aliyopewa ya kutumikia ameonyesha kwa vitendo namna ya mtumishi na kiongozi anavyoweza kuishi kwa mafanikio akiheshimu wenzake,akitenda haki na kupinga rushwa kwa vitendo, hivyo kwa nyenzo hizo anaweza kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya Serengeti mpya.
Nyagoga anamshukuru Mungu kwa kumuwezesha kuwa sehemu ya mafanikio hayo kwa kutumia elimu na uzoefu wake kwa manufaa ya na maslahi ya Watanzania wote