Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru akielezea kuanzishwa kwa huduma mpya ya matibabu ya kuvunja mawe kwenye figo na mfumo wa mkojo kwa njia ya mawimbi mshituko, kulia ni Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi akifuatiwa na Daktari Bingwa wa Upasuaji Mfumo wa Mkojo Dkt. Hamis Isaka na kushoto ni Dkt. Isaack Mlatie
Wataalam wakitumia mashine ya kisasa kutoa huduma ya matibabu ya kuvunja mawe kwenye figo na mfumo wa mkojo kwa njia ya mawimbi mshituko kwa kitaalamu
Pichani ni muonekano wa jiwe kabla halijavunjwa kwa kutumia teknolojia maalumu ya kuvunja mawe
Bi. Mwajuma Mbangwi akitoa ushuhudia na kuelezea jinsi mawe yalivyotoka kwa njia ya haja ndogo
Bw. Samson Makorere akiishukuru hospitali baada ya kupatiwa matibabu hayo
Muonekano wa mawe baada ya kuvunjwa mithili ya mchanga yaliyotoka kupitia njia ya haja ndogo.
…………………………………………………………………………
Na Lightness Mndeme, Muhimbili
Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imeanza kutoa huduma ya matibabu ya kuvunja mawe kwenye figo na mfumo wa mkojo kwa njia ya mawimbi mshituko kwa kitaalam Extracorporeal shock wave lithotripsy (ESWL).
Kuanzishwa kwa matibabu haya ni mwendelezo wa kutekeleza juhudi za Serikali za kuboresha huduma bobezi za kibingwa nchini ili kuongeza wigo wa huduma ambazo hapo awali zilikuwa hazipatikani hapa nchini kutokana na kutokuwepo kwa wataalamu, vifaa tiba au vyote viwili. Huduma hii inatolewa na wataalamu wazawa walioko Upanga na Mloganzila.
Huduma hii inafanywa kwa kutumia mashine ambayo inatoa mawimbi sauti yanayosafiri kupitia ngozi hadi kwenye figo sehemu yenye jiwe au mawe. Mawimbi hayo hugeuka kuwa nishati yenye uwezo wa kuvunja mawe kuwa madogo mithili ya mchanga ambapo yakishasagwa yanatoka kwa njia ya haja ndigo (kukojoa).
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa huduma hii mapema Juni mwaka huu jumla ya wagonjwa wanane wamenufaika na matibabu haya.
“Tumeanza kutoa huduma hii mapema Juni mwaka huu jumla ya wagonjwa wanane wameshanufaika na matibabu haya ambayo yameonesha matokeo mazuri, na hivi leo wagonjwa wawili wanaendelea kuhudumiwa hivyo kufikisha idadi ya wagonjwa 10 tangu ilipoanzishwa” amesema Prof. Museru.
Aidha Prof.Museru ameeleza kuwa katika kipindi cha mwaka 2019 jumla ya wagonjwa 1035 wenye mawe kwenye figo walionwa katika kliniki za wagonjwa wa nje (OPD) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga na Mloganzila ambapo kati ya hao wagonjwa wapya walikuwa 425 wakati wagonjwa waliolazwa kutokana na tatizo hilo walikuwa 114.Pia katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2017 jumla ya wagonjwa 23 wenye matatizo ya mawe kwenye figo walipatiwa rufaa ya kwenda kutibiwa nje ya nchi.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Mfumo wa Mkojo MNH-Mloganzila Dkt. Hamis Isaka ametaja faida ya matibabu haya, kuwa hayahitaji mgonjwa kulazwa hospitalini kwani anaweza kutibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani siku hiyo hiyo ili kuendelea na shughuli za ujenzi wa taifa.
“Faida ya upasuaji huu ni kuwa mgonjwa anaweza kufanyiwa siku hiyo hiyo na kuruhusiwa kuendelea na shughuli zake za kila siku pia uwepo wa huduma hii unaondoa ulazima wa upasuaji mkubwa kwa wagonjwa hawa” amesema Dkt. Isaka.
Dkt. Isaka ameongeza kuwa ziko sababu mbalimbali zinazosababisha ugonjwa huu kuwa ni uwepo wa madini kwa wingi katika mkojo, mfano madini aina ya calcium oxalate, citric acid na wakati mwingine inatokana na kutengeneza kiwango kidogo cha mkojo katika figo hasa kwa wale ambao hawanywi maji ya kutosha.
Vilevile maambukizi ya bakteria katika mfumo wa mkojo yanaweza kusababisha kupata ugonjwa wa mawe kwenye mfumo wa mkojo. Kwa kiasi kikubwa waathirika zaidi wa ugonjwa huu ni wenye umri kati ya miaka 40 mpaka 70.
Kwa upande wake mmoja wa mashuhuda ambaye amepatiwa huduma hii hospitalini hapa Bi. Mwajuma Mbangwi ameishukuru hospitali na kueleza kuwa kabla ya matibabu alikuwa akipata maumivu makali lakini kwa sasa afya yake imeimarika kabisa.
Hospitali itaendelea kushirikiana na nchi marafiki katika kufanikisha azma hii, tunatoa shukrani kwa African Future Foundation kupitia KOFIH ya Korea Kusini ambao tumeshirikiana kupitia mtandao (Zoom) kwa mgonjwa wa kwanza hatua ambayo imeleta matokeo mazuri katika kutoa tiba hii ya kibobezi.