Mkurugenzi wa Masari Investment inayojishughulisha na vipuri vya magari Faraj Abri akizungumza wakati wa kukabidhi msaada wa mtambo wa kunawa mikono kwa kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Iringa Juma Bwire
…………………………………………………………………………………..
NA DENIS MLOWE,IRINGA
KAMPUNI inayojishughulisha na uuzaji wa vipuri vya Magari ya Masari Investment ya mkoani Iringa imekabidhi mtambo maalum za kunawia mikono kwa watu sita kwa pamoja na sabuni za kutakasia mikono kwa jeshi la polisi mkoa wa Iringa ili kuendelea kupambana na ugonjwa wa Covid 19 unaosababishwa na virusi vya corona.
Akikabidhi msaada huo mkurugenzi wa Masari Investment, Faraj Abri alisema lengo la kampuni hiyo ni kuiunga mkono serikali katika mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona hivyo msaada huo umetolewa kwa ajili ya wananchi ambao wanakwenda kupata huduma kwenye kituo kikuu cha polisi mkoa wa Iringa.
Alisema kuwa mtambo huo wa kisasa utahudumia watu zaidi ya watano kwa pamoja katika kunawa mikono hivyo licha ya kutolewa kwa lengo la kuendelea kujinga na ugonjwa wa Covid 19 lakini utasaidia kwa kiasi kikubwa kuwafanya wawe wasafi na kuepukana na magonjwa ya kuahirisha ikiwemo kipindupindu.
Alisema kuwa msaada huo umekuja baada ya kuona kuna uhitaji mkubwa wa kusaidia jamii ambayo inakusanya watu wa aina mbalimbali hivyo jeshi la polisi kutokana na mazingira yake kama kampuni ikiaamua kuwapa kipaumbele.
Faraj Abri alisema kuwa katika mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona ni muhimu kwa jamii kuungana na kuunga mkono serikali ya awamu ya tano katika janga hili ambalo limeikumba dunia na misaada kama hii inahitajika hasa kwenye huduma za za kijamii ikiwemo vituo vya polisi.
“Lengo la kampuni ni kuunga mkono serikali katika mapambano dhidi ya kuenea kwa virusi vya corona hivyo ni muhimu kutoa misaada kwa jamii yenye uhitaji hasa watu wanaohudumia watu kwa wakati mmoja ikiwemo vituoni ambapo wengi wanapata huduma ”alisema
Kwa upande wake, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Iringa, Juma Bwire akizungumza msaada huo aliipongeza kampuni ya Masari Investment kwa kuwa mstari wa mbele katika kusaidia jamii na msaada huo utasaidia kwa kiasi kikubwa wananchi wanaofika katika kituo cha polisi kunawia kabla ya kupata huduma.
Alisema kuwa watahakikisha msaada huo wanatumia ipasavyo kwa kutoa elimu kwa wananchi kuweza kunawa mikono na kutoa wito kwa vyombo vya habari kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuzingatia maelekezo wanayopatiwa na wataalam wa afya kuweza kujinga dhidi ya maambukizi.