Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. John Kahyoza akizungumzia kuhusu maboresho ya miundombinu ya Mahakama yalivyorahisisha utoaji haki.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Adam Kighoma Malima akizungumia kuhusu kuwepo kwa baada ya Mahakama ya Tanzania kufanya uboreshaji wa miundombinu ya Mahakama yalivyorahisisha utoaji haki na kuokoa gharama kwa wananchi wa eneo hilo.
Baadhi ya wananchi waliofika kupata huduma katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma.
Kibarua aiyefanyakazi wakati wa ujenzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Bi. Moshi Zerange’sa akielezea jinsi alivyopata ajira ya mkataba kwenye kampuni ya kufanya usafi mahakamani hapo.
Baadhi ya vibarua waliofanyakazi wakati wa ujenzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, ambao pia wamepata ajira ya mkataba wa muda wa mwaka moja kwenye kampuni ya kufanya usafi mahakamani hapo.
Jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma.
Jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma.
Moja ya nyumba ya kuishi Jaji iliyojengwa katika kanda hiyo.
************************************
Na Magreth Kinabo na Innocent Kansha – Mahakama
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma imefungua jumla ya mashauri 59 kati ya mwezi Machi na Juni mwaka huu ambapo kati ya hayo, mashauri 56 yalifunguliwa kwa njia ya mtandao (E-filling) na mengine matatu yalifunguliwa kwa njia ya kawaida.
Akizungumza na Maafisa Habari wa Mahakama ya Tanzania ofisini kwake hivi karibuni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. John Kahyoza alisema mashauri yaliyofunguliwa ni yale yenye Mamlaka ya awali “Original Jurisdiction” .
Jaji Mfawidhi alisema, mashauri mengi yaliyopokelewa katika kipindi hicho ni yenye Mamlaka ya Awali kwa ngazi ya Mahakama Kuu ni ya mauaji ambayo ni mashauri 26, yanayotokana na migogoro ya ardhi 24 na madai tisa yaliyotokana shughuli za uchimbaji wa madini migodini, yakiwemo ya mikataba ya ajira na wafanyabiashara.
“Mashauri ya mauaji yamefunguliwa mengi hasa kwa Wilaya ya Tarime na migogoro ya ardhi inasababishwa na shughuli za kimaendeleo zinazoendelea hasa ujenzi wa miundombinu ya barabara kupita kwenye maeneo yanayomilikiwa na wananchi,” alisema Jaji Mfawidhi huyo.
Mahakama imekuwa ikisisitiza umuhimu wa mashauri kumalizika kwa wakati ili kutoa fursa kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi ambapo Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Wiki na Siku ya Sheria nchini ya mwaka huu inasema “Uwekezaji na Biashara: Wajibu wa Mahakama na Wadau kuweka Mazingira wezeshi ya Uwekezaji,’’.
Akizungumzia maudhui hayo wakati wa kilele cha Siku ya Sheria nchini iliyofanyika Februari 6, mwaka huu, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, alisema kuwa utawala wa sheria, na mfumo wa utoaji haki kwa wakati ni nyenzo muhimu katika kufanikisha na kurahisisha biashara, uwekezaji, ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi.
‘‘Hivyo tumekuwa tukiweka mikakati na malengo mbalimbali ili tuweze kutoa huduma ya utoaji haki kwa wakati ikiwa ni hatua ya kuendana sambamba na kauli mbiu hii, ’ alisisitiza Jaji Kahyoza.
Alieleza kuwa,wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutatua migogoro ya kiuchumi na biashara kwa kutumia njia mbadala ya usuluhishi na upatanishi “Alternative Dispute Resolution” (ADR) kama sheria inavyoelekeza ili kuharakisha usikilizaji wa mashauri hayo.
“Tumejiwekea lengo kwamba mashauri yote yenye Mamlaka ya Awali tunayoyapokea Mahakama Kuu tuyasikilize ndani ya miezi sita au kwa yaliyoshindikana kwa njia kusongezwa hadi muda wa miezi tisa badala ya utaratibu wetu wa kawaida wa miezi 24,” alisema.
Njia nyingine inayotumika kuharakisha usikilizaji wa mashauri hayo ni kutoahirisha mashauri mara kwa mara, ili mtu aweze kuahirishiwa shauri ni lazima awe na sababu ya msingi na nzito vinginevyo shauri lake linaondolewa mahakamani.
Jaji Kahyoza alifafanua kuwa, toka mwaka 2016 kulikuwa na masijala ya Mahakama ya Kazi iliyokuwa ikipokea mashauri ya migogoro ya kazi kwa ngazi ya Mahakama Kuu kuanzia mwaka 2016 hadi 2018 na kusajili mashauri 144 baada ya kuanza kazi kwa Mahakama hiyo, walijiwekea mikakati ya kusikiliza na kuitolea maamuzi kabla ya kuisha kwa mwaka 2019, tulifanikiwa na kubakiwa na mashauri 30 hadi Juni mwaka huu.
Kwa upande wa Teknolojia ya Habari na mawasiliano (TEHAMA), Jaji Kahyoza alisema Mahakama hiyo imepiga hatua kubwa kwa kutumia bajeti yao ya ndani katika kuhakikisha suala la matumizi ya teknolojia hiyo linafanikiwa katika Mahakama nyingine zilizopo kwenye kanda hiyo. Hivyo alisema wamesambaza vifaa vya teknolojia kwenye Magereza ya Wilaya za Tarime, Serengeti na Bunda vya kuendeshea mashauri kwa njia ya Mahakama Mtandao “Video Conference”, ruta na kuwawezesha bando.
Alisema Mahakimu Wafawidhi wa Wilaya zote wamewawezeshwa kwa kupatiwa kompyuta mpakato ili nao waweze kusikiliza mashauri kwa njia hiyo.
Mahakama hiyo imepokea na kusajili mashauri yapatayo 471 kuanzia Januari hadi Juni 12, mwaka huu na Majaji wamefanikiwa kusikiliza na kutoa maamuzi kwa mashauri 398 kwa kipindi hicho.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Adamu Malima, alimshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli na Uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kuwapatia jengo la Mahakama hiyo kwa kuwa ni jambo kubwa ambalo linawezesha wananchi wanyonge kuifikia huduma na kupewa haki zao.
Aliongeza kwamba Mahakama hiyo itakuwa na manufaa kwa wana Mara wengi.
Kwa upande wake Mtendaji wa Kanda ya Musoma, Bw. Festo Chonya alisema jengo hilo la kisasa limewasaidia kuboresha utendaji wa kazi kwa watumishi kwa sababu kila mtumishi ana eneo lake la kufanyia kazi kwa nafasi na ufanisi.
‘‘Suala la kupotea kwa majalada sasa limebaki kuwa historia, tuna mfumo wa kuhifadhi na kuyarudisha kwa wakati majalada, pia jengo hilo lina ghorofa mbili, zenye vyumba vya ofisi 50, bado tuna nafasi za kutosha hata kama Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania wakiwa wanafanya vikao vyao watafanya kazi bila bugudha. Hivyo tuko katika mazingira ya kazi ambayo ni rafiki, ’’ alisema Chonya.
Jengo hilo la kisasa lina ofisi za wadau mbalimbali wa Mahakama, wakiwemo washauri, Wadau wa Haki Jinai na Madai.
Alisema ili Mahakama hiyo iendelee kutoa huduma za kisasa kulingana na hadhi ya jengo wanahitaji watumishi 30, ambapo kwa sasa waliopo ni 34, hivyo mtumishi mmoja anafanya kazi zaidi ya moja ili kuondoa pengo hilo, mfano dereva anafanya kazi pia ya kuwapokea wageni na kutoa msaada wanaohitaji.
Mtendaji huyo alisema ujenzi wa jengo hilo, umegharimu zaidi ya shilingi bilioni sita pamoja miundombinu iliyopo, na wana wajibu wa kutunza rasilimali zilizopo ili zidumu kwa muda mrefu katika mazingira bora.
‘‘Tumejenga nyumba mbili za majaji ambazo zina miundombinu ya kisasa ya kumwezesha Jaji kufanya kazi akiwa nyumbani hata kwa kupitia Mahakama Mtandao, zenye thamani ya shilingi bilioni 1.5,’’ aliongeza Chonya.
Chonya aliendelea kusema kwamba, kupitia Mahakama hiyo wameweza kutoa ajira ya kudumu kwa watu 21, watano kati ya ni walinzi, waliobakia ni wanashughulika na usafi wa mazingira, ikiwa ni hatua ya kuwaongezea kipato.
Baadhi ya wakazi wa Musoma, ambao ni Bi. Moshi Zirang’esa na Bw.Deogratias Kimaro ambao awali walikuwa vibarua wakati wa ujenzi, walishukuru kuwepo jengo hilo ambalo limewasaidia kupata ajira ya kudumu ya mkataba wa mwaka mmoja , ambayo imewasaidia kupata kipato cha kulipia ada za shule na kutunza familia zao , kujenga nyumba, kufuga baadhi ya mifigo ilikuinua uchumi wao na taifa kwa ujumla, ikiwemo kupata uzoefu juu ya shughuli za kimahakama.
Wananchi waliofika kwa ajili ya kupata huduma mahakamani hapo, walisema wameridhishwa nazo kwa kuwa zimewapunguzia gharama.
Waliiomba Serikali iweze kujenga majengo mengine kwenye maeneo mengine, ili kuwezesha wakazi wa maeneo hayo pia kupata haki kwa wakati na kuinua vipato vyao na kukuza uchumi na pato la taifa.
Awali wananchi wa mkoa huo, walikuwa wanapata huduma za Mahakama Kuu katika Jiji la Mwanza aqmbapo walilazimika kusafiri umbali wa kilomita 220 kupata huduma za Mahakama Kuu. Nauli kati ya Mwanza na Musoma kwa bus ni Shilingi 8,000 kwenda tu, huku bado gharama nyingine mfano za kurudi , malazi la chakula kutegeamana na siku atakazotumia.