…………………………………………………………………..
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU Makao makuu, imetoa onyo kali kwa viongozi watakao bainika kutumia rushwa katika mchakato na uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Octoba mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa TAKUKURU, Brigedia Jenarali John Mbungo, amesema TAKUKURU haitamvumilia mtu yeyote atakaye jihusisha na vitendo vya rushwa bila kujali kiwango alichotoa au kupokea.
” TAKUKURU tupo macho hatutajali ni kiwango gani umepokea au kutoa, iwe elfu tano(5000) elfu kumi (10,000) au laki moja Sheria iko palepale tutakuchukulia hatua kali za kisheria” amesema Brigedia Jenarali Mbungo.
Amewahimiza watanzania wakati wa kupiga kura jambo la kujiuliza ni jambo gani mgombea anayegombea nini amekifanya wakati wa uongozi wake kama hajafanya kazi inayotakiwa wasihadaike na rushwa anayoitoa bali wachague viongozi wenye malengo mazuri.
“je mbunge au diwani wako wa jimbo anayemaliza mda wake alikuwa na mchango gani katika kuleta maendeleo katika jimbo lako” amesema.
Ameongeza kuwa” nipende kuwakumbusha wananchi kuwa kipindi cha mchakato wa uchaguzi sio kipindi cha mavuno ambacho wananchi wanaweza kukitumia kujipatia chochote kwa njia ya rishwa”
“Rushwa inapaswa kushughulikiwa bila huruma kwa sababu rushwa na hongo ni adui mkubwa wa ustawi wa jamii rushwa katika nchi inatakiwa ishughulikiwe sawa ma uhaini ” amesema.
Amesema wananchi wanapaswa kuchagua viongozi waadilifu watakaoweza kwenda sawa na kasi ya Mhe Rais Dkt Magufuli viongozi watakao jali maslahi ya wananchi na kutekeleza mipango ya serikali yao.
Amebainisha kuwa mgombea aneyejitoa katikati ya kinyang’anyilo kwa kuwa amehongwa inawezekana kwa kufanya hivyo inawanyima wapiga kura haki yao kupata kiongozi anayewafaa.