…………………………………………………………………………………………..
JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA LINAWASHIKILIA WATUHUMIWA NANE KWA KOSA LA KUPATIKANA NA VIFAA VYA KUVUNJIA.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa nane 1. RASHID KAWAYE [46] Mkazi wa tabora magili, 2. EMMANUEL SIMON [30] Mkazi wa Musoma Serengeti 3. JOHN JAMES [35] Dereva na Mkazi wa Iringa Kihesa 4. LOVENESS EDWARD NJAU [27] Mama Ntilie na Mkazi wa Iringa Masasi 5. ALFRED MASUNGA [58] Mkazi wa Dar-es-Salaam 6. JUMA SONGOLO [53] Mkazi wa Dar-es-Salaam 7. EMANUEL TUMBUKA [35] Mkazi wa Shinyanga na 8. MWIGUNE MWAMBEULE [43] Mkazi wa Msaranyaki Songea kwa tuhuma za kupatikana na vifaa vya kuvunjia.
Watuhumiwa walikamatwa mnamo tarehe 14.06.2020 majira ya saa 20:00 usiku baada ya Jeshi la Polisi mkoani hapa kupata taarifa za siri kuwa kuna watu wapatao wanne hadi sita wamepanga kuvamia duka lililopo katika eneo la Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji [TEKU] ambalo linajishughulisha na Uwakala wa NMB, CRDB, TPB pamoja na M-Pesa na Tigo pesa kwa lengo la kupora fedha.
Baada ya kupokelewa kwa taarifa hiyo, kikosi kazi cha kuzuia uhalifu Mkoa wa Mbeya kilijipanga kuzuia tukio hilo na baada ya kufika eneo la tukio kilivamia chumba walichokuwa wamejificha wahalifu hao na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne wakiwa wanaendelea na kuchimba ukuta wa duka hilo kwa kutumia K. K. (driler) na mara baada ya kuwadhibiti wahalifu hao walipekuliwa na kukutwa na vifaa mbalimbali vya kuvunjia ambavyo ni:-
- K. K. (driler) moja,
- Biti tatu,
- Mitungi miwili [02] ya Gesi pamoja na Pipe zake.
- Spana mbili [02].
- Chupa ya K-Vant iliyochanganywa dawa za kulevya na vifaa vya kukatia kasiki.
- Funguo zilizochongwa 21.
- Bisibisi moja [01].
Katika mahojiano, watuhumiwa hao wamekiri kutenda kosa hilo huku wakieleza kuwa mbinu waliyotumia kutenda uhalifu huo ni kukodi chumba katika nyumba ya kulala wageni [Guest] iliyopo karibu na duka ambalo walidhamiria kuiba ambapo walimtanguliza LOVENESS EDWARD NJAU [27] kwa ajili ya kusoma ramani/mazingira ya eneo husika na kisha wao kufika na kujifungia kwenye chumba hicho kinachotenganishwa na ukuta mmoja na duka hilo na kisha kuchimba shimo hadi ndani ya duka. Msako wa kuwatafuta watuhumiwa wengine unaendelea.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ULRICH MATEI anatoa wito kwa wananchi wote kuacha vitendo vya uhalifu ambavyo vinaweza kuwasababishia kupoteza dira za maisha yao na kujikuta katika mikono ya sheria na hatimae kupata adhabu kali ikiwa ni pamoja na kutumikia vifungo kwa mujibu wa sheria.
KUSALIMISHA SILAHA.
Mnamo tarehe 14.06.2020 majira ya saa 12:30 Mchana huko Kijiji cha Nyamakuyu kilichopo Kata ya Madibira, Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya. ENOCK MDENDEMI [38] Mkazi wa Nyamakuyu – Madibira akiwa na mwenzake ambaye hakutambulika jina waliamua kusalimisha bunduki mbili aina ya Gobole zilizotengenezwa kienyeji, zikiwa hazina namba za usajili kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyamakuyu JANGASON MPULULE [33] Mkazi wa Nyamakuyu-Madibira na kuacha ujumbe wa maandishi kuwa “wameamua kuachana na kazi ya ujangili baada ya kupata elimu toka kwa OCD Mbarali SSP-GALUS A. HYERA.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya anaendelea kutoa wito kwa wananchi wote kusalimisha silaha wanazomiliki kinyume cha sheria [bila kibali] kabla ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya halijaanza kufanya operesheni maalum dhidi ya watu wanaomiliki silaha bila kibali. Aidha anatoa rai kuacha vitendo vya ujangili na badala yake wafuate taratibu za uwindaji kwa kupata vibali kutoka mamlaka husika kwa ajili ya kufanya kazi hizo kwa mujibu wa sheria.