****************************
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
MKOA wa Pwani ,umefanya mnada wa kwanza wa zao la kibiashara la ufuta ,na kufanikiwa kuu tani 1,231 kati ya tani 3,118 zilizokwenda sokoni kwa bei ya juu ya sh.2,172 kwa kilo moja .
Tani zilizokwenda sokoni zimenunuliwa kupitia mfumo wa sanduku (box) kwa wateja watatu waliojitokeza tofauti na matarajio ya wengi kuwa tani nyingi zingenunuliwa kupitia mfumo wa kielektronik wa TMX ambapo amejitokeza mteja mmoja kwa mkoa wa Pwani kwa bei ya sh.1,952 ukilinganisha na minada ya Dodoma na Mtwara ambayo walifanikiwa .
Akizindua mnada huo wa kwanza uliofanyika ,wilaya ya Kibiti ,mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo alisema tani zinazotarajia kuzalishwa kwa mkoa huo kwa msimu huu ni tani 10,000 .
Hata hivyo ,mkuu huyo wa mkoa alitangaza mnada wa pili utafanyika Juni 19 ,mwaka huu .
“;Mkoa wetu umetumia mifumo hii miwili, bei kubwa imetokana na mfumo wa sanduku ,kupitia mtandao bei ni ya chini na mnunuzi aliyejitokeza ni mmoja ,nawaomba TMX mjipange kutafuta soko ,maana mikoa mingine imefanikiwa ,ichunguzwe kama kuna mtu anawahujumu ijulikane achukuliwe hatua ” alisisitiza Ndikilo.
Ndikilo alitaja changamoto kubwa, iliyopo kwasasa ni kukwama kwa ufuta kwenye maghala ya vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS )na kushindwa kufikishwa kwenye maghala makuu kutokana na miundombinu ya barabara kuwa mibovu .
Alielekeza ,wanunuzi waelekezwe ufuta ulipo katika maghala hayo ,na ununuliwe ukiwa huko kwa utaratibu wa mfumo wa stakabadhi ghalani na si vinginevyo.
Alikemea baadhi ya watu wanaotorosha ufuta kwa njia zisizo rasmi ,na kudai atakaebainika gari lake litataifishwa na ufuta utachukuliwa pamoja na kuchukuliwa hatua kali .
Ndikilo pia aliwatahadhalisha wakulima ,kuacha kuweka mawe katika ufuta kwa lengo la kujinufaisha na badala wauze ufuta wenyewe ili kurejesha imani kwa wanunuzi .
Nae mkurugenzi wa operesheni kutoka TMX ,Augustino Mbulumi alisema ,waliuza ufuta kwa bei ya juu sh 2,040 kwa kilo na kufikia mnada wa Pwani soko limeporomoka hadi kufikia sh. 1,952 kwa kilo moja na mteja aliyejitokeza ni mmoja tofauti na mikoa ya Dodoma na Mtwara .
Katibu tawala msaidizi na msaidizi uchumi na uzalishaji mkoani Pwani ,Shangwe Twamala alibainisha ,tani 300 za Ikwiriri zimenunuliwa na ICS trade ltd kwa sh .2,042 ,”;na tani 200 za Kibiti amechukua Mujibu Shamba kwa sh .2,142 kwa kilo na ;’:tani nyingine 731 za Ikwiriri na Kibiti amenunua HS Impex kwa bei ya juu ya sh.2,172.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama kikuu cha Ushirika (CORECU)-Pwani ,Rajabu Ng’onoma aliwataka wanunuzi wajitokeze,kwakuwa bado kuna ufuta mwingi katika maghala ya AMCOS, ili wakulima waweze kupata soko na kujikwamua kiuchumi .