*****************************
· Yaongeza kiwango cha kukopa, muda malipo na kupunguza riba
Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam. Taasisi ya huduma za kibenki ya Faidika imetenga zaidi ya Sh 40 bilioni kwa ajili ya kuwakopesha watanzania wenye ajira kupitia programu ya ‘Mshahara wako, mkopo wako,’
Mkurugenzi Mkuu wa Faidika , Bw. Baraka Munisi alisema kuwa mikopo hiyo inatolewa ndani ya saa 24 endapo mkopaji atatimiza masharti yaliyowekwa.
Bw. Munisi alisema kuwa wameamua kutenga kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kuboresha maisha ya Watanzania kupitia ‘moto’ wao, ‘Let’s Improve Life’ .
Sambamba na hilo wameongeza kiwango na muda wa malipo. Kwa sasa wanatoa mikopo kuanzia Sh 200,000/= mpaka Sh milioni 70 na malipo yake yanatakiwa kufanyika kwa kipindi cha miezi sita (6) hadi miezi 84.
Alisema kuwa mbali ya kuongeza kiwango cha kukopa na muda wa mkopaji kulipa deni, pia wamepunguza riba ambayo inatoa nafuu kwa mkopaji kulipa deni lake.
Alifafanua kuwa mikopo hiyo inakuwa inatolewa kupitia matawi yao 16 na ofisi zaidi 88 zilizopo nchini na katika mikoa tofauti.
“Pamoja na changamoto za miundo mbinu, Faidika inaamini kuwa kila mtu anastahili kupata huduma ya kifedha ndio maana tumepanua wigo kupitia mifumo ya kisasa zaidi ya teknolojia ili kuwafikia watanzania wote kwa lengo la kuboresha maisha yao,” alisema Bw. Munisi.
Alisema kuwa wafanyakazi wa serikalini na taasisi zilizo thibitishwa wanaruhusiwa kupata mikopo hiyo.
“Unachotakiwa kuleta ili kujipatia mkopo wako ni kitambulisho cha kazi, picha moja ya pasipoti, stakabadhi moja ya mshahara (salary slip) ya mwezi uliotangulia na taarifa za akaunti ya benki kuanzia miezi miwili na kuendelea. Faidika ina huduma za kipekee, rahisi, sahihi, nafuu za zenye kukidhi mahitaji, ” alisema.
Aidha alisema kuwa kwa wateja waliokopa wanaweza kutumia mikopo hiyo katika kuboresha maisha yao kupitia uwekezaji kwenye elimu, afya na kilimo.
Kwa mujibu wa Bw. Munisi, mikopo hiyo hufutwa pindi mdaiwa anapofariki na taasisi yao itatoa rambirambi ya sh200,000 kwa mfiwa.
“Taasisi yetu imedhamiria kuboresha zaidi maisha ya watanzania kwa mwaka 2020 na kuendelea. Tunawaomba wananchi kuchangamkia huduma hii ambayo ni ya kipekee na rahisi,” alisisitiza.