*******************************
Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo amesema wanafunzi wote wa bweni waliochaguliwa kujiunga na kidato cha Tano kwa mwaka 2020 wanatakiwa kuripoti shuleni tarehe 18 Julai,2020 na wale wa kutwa kuripoti na kuanza masomo tarehe 20 Julai,2020.
Waziri Jafo ameyasema hayo wakati akitoa taarifa kuhusu uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano, vyuo vya ualimu na vyuo vya ufundi mwaka 2020 mapema leo katika Ofisi za TAMISEMI, Jijini Dodoma.
Amesema wanafunzi ambao hawataripoti wiki mbili tangu tarehe ya kufungua shule nafasi zao zitachukuliwa na wanafunzi wengine ambao hawakupangiwa shule katika awamu hii.
Aliongeza kuwa Uhamisho wa shule utaruhusiwa baada ya kukamilika kwa muhula wa kwanza wa masomo, na zoezi hilo litafanyika kwa kuzingatia uwepo wa nafasi kwenye Shule kwa idhini ya Maafisa Elimu wa Mkoa husika, hivyo hakutakuwa na fursa ya kufanya mabadiliko yoyote ya shule kwa sasa ngazi za Mikoa, Halmashauri na Shule.
Akizungumzia takwimu za watahiniwa wa mtihani wa kidato cha Nne,2019 amesema watahiniwa wa shule 425,072 wakiwemo wasichana 221,813 na wavulana 203,259 walifanya mtihani wa kuhitimu kidato cha Nne mwaka 2019 na watahiniwa wa kujitegemea walikua 48,683.
“Jumla ya wanafunzi 121,251 wakiwemo wasichana 53,829 na wavulana 67,422 wamechaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano, Vyuo vya Ualimu na Vyuo vya Elimu ya Ufundi vinavyosimamiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), idadi hii ni sawa na asilimia 93.4 ya wanafunzi wenye sifa za kuchaguliwa alisema Waziri Jafo”
Aidha Waziri Jafo alifafanua kuwa wanafunzi 73,101 wakiwemo wasichana 35,005 na wavulana 38,096 sawa na asilimia 52.1 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha tano na wanafunzi 9,264 wakiwemo wasichana 4,314 na wavulana 4,950 wamechaguliwa kujiunga na vyuo vya Elimu ya ufundi, vyuo vya Afya na vyuo vya Ualimu huku wanafunzi 38,886 wakiwemo wasichana 14,510 na wavulana 24,376 wamechaguliwa kujiunga na vyuo vya Elimu ya ufundi vinavyosimamiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).
Waziri Jafo alitoa maelekezo kwa wanafunzi waliopangwa kwenye vyuo vya Elimu ya Ufundi vilivyopo chini ya NACTE kuwa wanatakiwa kuthibitisha kukubali kujiunga na kozi zinazosimamiwa na NACTE baada ya siku saba kuanzia siku ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi hadi tarehe 15 Agosti 2020.
“Mwanafunzi atafanya uthibitisho kupitia kiunganishi kinachoitwa UTHIBISHO TAMISEMI katika tovuti ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) ambayo ni www.nacte.go.tz ili kukubali kuchaguliwa kwenye kozi za vyuo walivyopangiwa.
Mwanafunzi ambaye hatathibitisha kukubali nafasi aliyochaguliwa, nafasi yake itachukuliwa na wanafunzi wengine wanaoendelea kuomba katika vyuo hivyo kwa njia ya mtandao” Alisema Waziri Jafo.
Aliongeza kuwa wanafunzi wanaotaka kufanya mabadiliko ya kozi au chuo walichochaguliwa wanaruhusiwa kufanya hivyo kuanzia tarehe 01 Agosti hadi 30 Agosti 2020 kupitia mtandao wa NACTE.
Aidha Waziri Jafo alibainisha kuwa wanafunzi waliopangwa katika chuo kikuu cha Ushirika Moshi na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya hawatahusika na utaratibu wa kubadilisha wa NACTE, hivyo wanapaswa kuwasiliana na vyuo husika.
Pia Waziri Jafo aliwashukuru wadau wote wa Elimu kwa kushiriki kikamilifu kuimarisha miundombinu ya shule ikiwemo madarasa, mabweni, maktaba,maabara na majengo mengineyaliyowezesha shule 32 mpya kuanzishwa na kupokea jumla ya wanafunzi 2,571 wakiwemo wasichana 1,584 na wavulana 987 wa kidato cha Tano kwa mara ya kwanza.
Alihitimisha kwakuwataka wakurugenzi wa Halmashauri za Kyerwa Dc, Momba Dc, Mtwara Dc, Ubungo Mc na Nanyamba Tc ambazo hazina shule za kidato cha Tano na Sita kuhakikishe kuwa kufikia tarehe 30 Januari, 2021 Halmashauri zao ziwe na Shule zenye Kidato cha Tano hususan za masomo ya Sayansi na Hisabati na ziwe zimetengewa bajeti ya chakula.