********************************
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inaungana na wadau wote wa haki za watoto katika kuadhimisha “Siku ya mtoto wa Afrika”. Siku hii inaikumbusha dunia juu ya mauaji ya watoto wapatao 2,000 wa kitongoji cha Soweto nchini Afrika Kusini, waliouawa kikatili miaka 44 iliyopita na iliyokuwa Serikali ya Makaburu.
Siku hii ilizinduliwa rasmi Mwaka 1991 na uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ili kuwakumbuka watoto hao waliokuwa wakidai haki ya kutobaguliwa na haki nyingine za binadamu.
Wakati tunaadhimisha siku hii muhimu wadau wote wa haki za watoto hatuna budi kujitathimini namna tulivyoandaa na kutekeleza mifumo rafiki na inayofikiwa na wote katika kulinda haki za watoto kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu inayosema: “Mifumo rafiki ya upatikanaji wa haki ya mtoto: Ni msingi wa kulinda haki zao.”
THBUB inapenda kupongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa hatua mbalimbali zinazochukua katika kulinda haki na maslahi ya watoto. Hatua hizo ni pamoja na kuridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda, kutunga sera, sheria, kanuni, miongozo na kuandaa mipango na mikakati mbalimbali inayolinda, kutetea na kukuza haki za mtoto.
Miongoni mwa mikataba ambayo Tanzania imeridhia ni Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto (1989) na Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto (2003).
Kwa upande wa sheria, Tanzania imefanikiwa kutunga sheria mbali mbali zikiwemo Sheria ya Mtoto Na.21/2009,Sheria ya Mtoto Na. 6/2011, Sheria ya Kanuni za Adhabu na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Tanzania Bara na Zanzibar. Aidha, kanuni mbalimbali zimetungwa zikiwemo Kanuni za Mahabusu za Watoto, Kanuni za Ulinzi wa Mtoto, Kanuni za Shule ya Maadilisho, Kanuni za Mahakama za Watoto na Kanuni za Kamati za Ustawi katika kulinda haki za mtoto.
Sera ya Mtoto (2008) na Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kuzuia na Kupambana na Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (2017 – 2022) ni miongoni mwa nyezo nyingine zilizoandaliwa kuhakikisha ustawi wa haki za mtoto hapa nchini.
THBUB inatambua kupitia Mikataba, Sera, Sheria, Miongozo na Mipango hio, mifumo rafiki ya kusimamia upatikanaji wa haki kwa watoto imeanzishwa na kuimarishwa. Mifumo hiyo ni pamoja na mahakama za watoto, madawati ya jinsia na watoto katika vituo vya polisi, mahabusu za watoto, mabaraza ya watoto na Shule ya maadilisho. Vile vile, mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi katika taasisi hizi yamekuwa yakifanyika mara kwa mara ili kuwawezesha watumishi kutekeleza majukumu yao ya kusimamia utekelezaji wa haki kwa watoto kwa ufanisi mkubwa.
Pamoja na jitihada hizo, bado kuna changamoto mbalimbali zinazoathiri upatikanaji wa haki za watoto katika jamii. Changamoto hizo ni pamoja na watoto kuwekwa vizuizini katika magereza ya watu wazima kinyume na sheria ya mtoto, watoto kutopata msaada wa kisheria wakiwepo katika mkinzano na sheria na uelewa mdogo wa jamii kuhusu Sheria ya Mtoto na Kanuni zake. Nyingine ni ukeketaji, utumikishaji wa watoto, unyanyasaji wa kingono, kimwili, kisaikolojia na mimba za utotoni ambazo zimekuwa na athari kwa mtoto kiafya na kielimu.
Hivyo basi, THBUB inapenda kutoa mapendekezo yafuatao kwa Serikali, wadau mbali mbali na jamii kwa ujumla:
- Mamlaka zinazotoa haki kwa wahanga wa ukatili, wakiwemo watoto zitoe haki kwa wakati kwa kuzingatia maslahi mapana ya mtoto.
- Wadau wa haki za binadamu waendelee kutoa elimu ya haki za binadamu kwa jamii ili kubadili mila na tamaduni potofu pamoja na kukemea vitendo vya ukatili, unyanyasaji na udhalilishaji wa watoto.
- Wazazi wawajibike katika malezi ya watoto ili kuimarisha familia zao. Aidha, wahakikishe watoto wa kike na wa kiume wanapatiwa fursa sawa ili ndoto zao katika maisha zifikiwe.
- Watoto wapatiwe elimu ya afya ya uzazi ili waweze kujitambua na kuwa na uelewa juu ya madhara ya mimba na ndoa za utotoni.
- Wadau mbalimbali wa haki za watoto wahakikishe kuwa ulinzi, usalama na haki za mtoto zinaimarishwa na kuhakikisha kuwa aina zote za ukatili na ubaguzi dhidi ya watoto zinatokomezwa.