Mtoto Faith Malosha mkazi wa Tulieni Manispaa ya Mpanda akiwa anafanya kazi za shule
Watoto wakicheza katika miti katika mtaa wa Kachoma Manispaa ya Mpanda.
************************************
Na Zilpa Joseph, Katavi
Imeelezwa kuwa serikali itakapotangaza kufungua shule za msingi baadhi ya wanafunzi wa shule hizo hasa madarasa ya awali watakuwa wamepoteza uwezo wa kusoma na kuandika kutokana na wazazi kutojihusisha kuwakumbusha masomo watoto katika kipindi hiki cha likizo ndefu
Serikali ilichukua uamuzi wa kufunga shule zote hapa nchini machi 17 mwaka huu ili kudhibiti maambukizi ya virusi hatari vinavosababisha homa kali ya mapafu
Hayo yamesemwa na baadhi ya walimu wa shule za msingi katika manispaa ya Mpanda ambao wameeleza kuwa kwa wanafunzi kama hao kuna haja ya kuanza kuwafundisha upya
“Nimekutana na mwanafunzi wangu wa darasa la kwanza ambaye alikuwa akiongoza kufanya vizuri darasani, nikamuuliza kama anakumbuka kuandika neno baba; aliponichorea chini nimetamani kucheka hizo herufi ‘b’ zimegeuzwa” alisema mwalimu mmoja wa shule ya msingi Misunkumilo ambaye hakutaja jina lake litajwe
Naye mwalimu Kapungu Mashauri wa shule ya msingi Kakese Mbugani amesema anategemea wanafunzi hasa wa madarasa ya chini watarudi shuleni wakiwa wamesahau kila kitu
“Tutaanza upya! Watakuwa doro, hii inatokana na mazingira yetu huku, watu hawana mwamko wa kutosha wa elimu, mtoto amerudi nyumbani anapewa fimbo akachunge ng’ombe!” alisema mwalimu Kapungu
Kwa upande wao baadhi ya wanafunzi wamemweleza mwandishi wa habari hizi kuwa wanatumia muda mwingi kucheza na wakati mwingine wanasaidia kazi mbalimbali za nyumbani
“Tunacheza tu hatusomi” alisema mmoja wa watoto waliohojiwa
Katika baadhi ya kaya hasa zinazoonekana zina kipato cha kati watoto wa nyumba hizo wamekuwa wakifanya mitihani mbalimbali ya kuwakumbusha masomo yao
“Mama huwa anatufuatia mitihani shuleni tunakuja tunafanya mimi na dada yangu baadae tunacheza” alisema Faith Malosha mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi nzella
Nao wazazi walipoulizwa sababu za kushindwa kuwasimamia watoto kujikumbusha masomo yao wamedai kuwa majukumu yamewabana