Home Mchanganyiko CHRAGG ANGALIENI ENEO LA UNYANYASAJI WA KIJINSIA HAPA ZANZIBAR-WAZIRI RASHID

CHRAGG ANGALIENI ENEO LA UNYANYASAJI WA KIJINSIA HAPA ZANZIBAR-WAZIRI RASHID

0

Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Hamad Rashid Mohammed (kwanza kulia), Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu (pili kulia) na Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mohamedi Khamis Hamadi (tatu kulia), wakifurahia jambo kabla ya kikao kifupi alipotembelewa na uongozi wa juu wa Tume hiyo Ofisini kwake Mjini Unguja Zanzibar.

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu (pili kulia), akifafanua jambo kwa Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Hamad Rashid Mohammed (kwanza kulia)  katika kikao kifupi walipomtembelea Ofisini kwake Mjini Unguja Zanzibar, wengine ni watendaji wa juu wa tume hiyo.

Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Hamad Rashid Mohammed (kushoto), akifafanua jambo kwa uongozi wa juu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, katika kikao kifupi na tume hiyo kilichofanyika  Ofisini kwake Mjini Unguja Zanzibar.

Watendaji Wakuu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, wakimsikiliza Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Hamad Rashid Mohammed (hayupo pichani) wakati wa kikao kifupi baina ya tume na Wizara hiyo kilichofanyika  Ofisi  za Wizara Mjini Unguja Zanzibar.

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu akikabidhi mpango mkakati wa tume hiyo wa mwaka 2018/23 kwa Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Hamad Rashid Mohammed baada ya kikao kifupi baina ya tume na Wizara hiyo kilichofanyika  Ofisi  za Wizara Mjini Unguja Zanzibar.

Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Hamad Rashid Mohammed akiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa juu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora baada ya kikao kifupi baina ya tume na Wizara hiyo kilichofanyika  Ofisi  za Wizara Mjini Unguja Zanzibar.

……………………………………………………………………

Na Mwandishi Wetu-MAELEZO.

Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibari, Mhe. Hamad Rashid Mohammed amesema kuwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, inatekeleza kazi kubwa katika kutoa haki za binadamu kwa kutoa ripoti ambazo zinahusu masuala ya haki za watu na ameitaka kujikita zaidi kwenye masuala ya kijamii hususani unyanyasaji wa kijinsia kwani ni tatizo kwa Zanzibar.

Akizungumza na ujumbe wa watendaji wa juu wa Tume hiyo Ofisini kwake Mjini Unguja Zanzibar, Waziri Rashid alisema kuwa siku za nyuma utekelezaji wa haki za binadamu hususani masuala ya unyanyasaji wa kijinsia ilikuwa ni ngumu kwani utekelezaji wa ripoti za tume hiyo zilikuwa hazifanyiwi kazi tofauti na sasa.

“Siku za nyuma mlikuwa mkiandika, kutoa na kusoma ripoti lakini zilikuwa hazifanyiwi kazi, sasa hivi kidogo utekelezaji wa ripoti mnazoandika na  kuziwasilisha zimekuwa na msaada zaidi kwa jamii, kwani haki za binadamu hasa unyanyasaji wa kijinsia wananchi  wamekuwa na mwamko wa kutafuta msaada wa upatikanaji wa haki baada ya chombo chenu hiki kufanya kazi kubwa ya kuwaelimisha wapi wanaweza kupata msaada wa haki zao”, Waziri Rashid.

Alisema, kuwa kuna maeneo Zanzibar ambayo wananchi wanahitaji kupata haki zao za msingi hususani kwenye eneo la unyanyasaji wa kijinsia na ucheleweshwaji wa haki za binadamu katika baadhi ya Taasisi za kutoa na kusimamia haki nchini.

Naye, Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu, alisema kuwa ziara yake Zanzibar inalenga hasa kujifunza mambo mengi na kupata ushirikiano kwa Serikali na Taasisi zake katika utekelezaji wa haki za binadamu nchini.

“Katika ziara yetu hii tumejifunza mambo mengi sana na kila tulipoenda tumeambiwa mambo mengi sana na tunatakiwa kuyafanyia kazi sisi kama tume ili kuwezesha wananchi wa Zanzibar kupata haki zao za msingi kila panapohitajika”, Jaji Mstaafu Mwaimu.

Alibainisha, kuwa utekelezaji wa ripoti za tume hiyo hapo mwanzo ulikuwa mgumu lakini kwa sasa hivi mambo yemebadilika na sasa kila mtu anatenda kazi yake ipasavyo hasa akipokea ripoti hizo ambazo zimekuwa zikitolewa na tume hiyo kuhusu masuala ya haki za binadamu.

Aliongeza, kuwa tume hiyo inapita katika Ofisi za Serikali na Taasisi zinazotoa na kutekeleza haki za binadamu ili kupata uhusiano na ushirikiano mkubwa kwa Serikali na kuwezesha wananchi wote kupata haki zao katika masuala mbalimbali ya kijamii.

Mwisho