Wanafunzi wa Kidato cha Sita katika Shule ya Sekondari ya Tumaini iliyopo wilayani Iramba mkoani Singida wakifurahia kupata bomba la maji kwa ajili ya kutakasa mikono ili kujikinga na Covid 19 lililo jengwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Singida (SUWASA)
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo (kulia) akika utepe kuashiria uzinduzi wa bomba la maji lililojengwa na wizara hiyo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Singida (SUWASA) kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa wa Corona katika Shule ya Sekondari ya Tumaini iliyopo Iramba mkoani Singida mwishoni mwa wiki. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo (kulia) akimkabidhi dawa ya kutakasa mikono Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Singida (SUWASA) Mhandisi Patrick Nzamba,
Bomba la maji lililozinduliwa shuleni hapo.
Mkuu wa shule hiyo, Honoratha Ndiaji alishukuru kwa shule hiyo kupata msaada huo.
Wanafunzi wakifurahia msaada huo.
.
Na Dotto Mwaibale, Singida.
WIZARA ya Maji katika mwaka wa fedha ujao itatenga Sh.Bilioni 2 kwa ajili ya kupeleka huduma ya maji kwenye mashule na vituo vya afya.
Hayo yalibainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Kitila Mkumbo wakati akizindua bomba la maji lililojengwa na wizara hiyo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Singida (SUWASA) kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa wa Corona katika Shule ya Sekondari ya Tumaini iliyopo Iramba mkoani Singida mwishoni mwa wiki.
Mkumbo alisema wizara hiyo mwaka huu wa 2020/ 2021 wameanzisha programu maalumu ya kupeleka huduna za jamii kwenye taasisi za za kijamii kwa maana vituo vya afya na shule za sekondari na msingi.
” Tunachokifanya leo hapa ni kutoa alama mbili, alama ya kwanza ni kuonesha mwaka unaokuja tunakwenda kutekeleza programu ya kupeleka maji kwenye taasisi zetu.Lakini ya pili ni kama alivyoagiza Rais wetu Dk.John Magufuli shule zetu zifunguliwe huku tahadhari ya kujikinga na na Corona hivyo tuliwaelekeza wataalamu wetu wasaidie kutengeneza miundombinu ya kunawa mikono kwa sabuni na sisi tutatoa mchango wa maji na Halmashauri zitoe sabuni.” alisema Mkumbo.
Alisema kwa Mkoa wa Singida waliichagua shule kongwe ya Tumaini na pia mtu huwa haachi nyumbani kwao kwa vile na yeye anatoka eneo hilo akaona ni vizuri msaada huo ukapelekwe kwenye shule hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa SUWASA Mjini Singida, Mhandisi Patrick Nzamba alisema wamejipanga kuhakikisha wanajenga miundombinu ya kutoa maji.
Alisema sambamba na hilo wameweza kuweka vituo vya kunawia sehemu mbalimbali katika Manispaa ya Singida, Soko la Kimataifa la Vitunguu, Stendi ya Mabasi na sasa katika shule hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula alisema msaada huo katika shule hiyo ni wa kizalendo hivyo akatoa rai ya kuhimiza miundombinu kutunzwa.
Mkuu wa shule hiyo, Honoratha Ndiaji alishukuru kwa kusema kuwa msaada huo kwao ni faraja kubwa.
Kwa upande wake Mwanafunzi wa Kidato cha Sita katika shule hiyo, Alice Katunzi alimshukuru Rais John Magufuli kwa kuruhusu kidato cha sita kuendelea na masomo hivyo wamemuahidi watahakikisha wanafunzi wote wakidato hicho nchi nzima wanapata alama A.