Maafisa usajili wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa nchini (NIDA) wakiendelea kutoa huduma za usajili kwa wananchi katika ofisi za Wilaya za Mamlaka hiyo katika Wilaya za Mkoa wa Dar es salaam huku tahadhari za maambukizi ya virusi vya Corona ikiendelea kuzingatiwa kikamilifu.
……………………………………………………………………………
Na: Agnes Gerlad
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inaendelea na shughuli za Usajili na Utambuzi wa Watu nchini kote ambapo wananchi wanaendelea kupatiwa huduma katika ofisi za Usajili za NIDA zilizoko katika kila wilaya nchini.
Kwa mujibu wa Msemaji wa NIDA, Bw. Geofrey Tengeneza amesema, NIDA kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji, Uongozi wa Wilaya/Mkoa, Serikali za Mitaa na Wadau wengine inaendelea kutoa huduma zote zinazohusiana na Usajili na Utambuzi wa watu kama ilivyokuwa awali.
Ameongeza kusema kwamba, Usajili wa awali kwa maana ya Mwombaji kujaza fomu ya Maombi ya Utambulisho wa Taifa, kuchukuliwa alama za Kibaiolojia inayohusisha mwombaji kupigwa picha, kuchukuliwa alama za vidole na kuweka saini ya kielektroniki unaendelea kufanyika katika ofisi zote za Usajili za NIDA zilizoko katika wilaya zote nchini kwa kuzingatia tahadhari na maelekezo yaliyotolewa na Wizara ya Afya juu ya kujikinga na changamoto ya janga la Corona (COVID 19).
Aidha ametoa rai kwa wateja waliokamilisha Usajili kuangalia Namba zao za Utambulisho wa Taifa kupitia Kituo cha Huduma kwa Mteja, kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno kwenda namba 15096 ama kupitia tovuti yetu www.nida.go.tz (https://services.nida.go.tz/nidportal/get nin.aspx) bila kulazimika kufika kwenye ofisi za Usajili za wilaya jambo linalowaokolea wananchi muda wao na kupunguza msongamano kwenye ofisi za Usajili.