Mkurugenzi wa Mati Super Brand, ya Mjini Babati Mkoani Manyara, David Mulokozi (kushoto) akikabidhi vitakasa mikono kwa taasisi za serikali.
******************************
Kampuni ya Mati Super Brand ya Mjini Babati Mkoani Manyara, imetoa msaada wa vyakula na vitakasa mikono kwa ajili ya kujikinga na virusi vya corona.
Vifaa hivyo ni mchele, mafuta ya kula, sabuni na vitakasa mikono kwa vituo vya watoto yatima na wazee na vitakasa mikono kwa taasisi za serikali.
Mkuu wa mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akizungumza wakati akipokea vifaa hivyo aliwapongeza viongozi wa Mati Super Brand kwa kutoa msaada huo.
Mnyeti alisema japokuwa hali ya maambukizi ya corona yamepungua hivi sasa lakini tahadhari zinapaswa kuendelea kuchukuliwa na jamii.
Aliwaasa wanasiasa kutohofia pindi misaada inapotolewa na watu kwa kudhani majimbo yao yatachukuliwa kwani suala la misaada halihusiani na kugombea.
“Jamii inahitaji misaada sasa baadhi ya wanasiasa mnaopiga kelele kwa watu wanaotoa misaada sitaki kusikia mkoani kwangu kama kuchaguliwa watu watapima ulifanya nini,” alisema Mnyeti.
Mkurugenzi wa Mati Super Brand, David Mulokozi alisema wametoa msaada huo kwa taasisi za serikali ikiwemo ofisi ya mkuu wa mkoa, polisi, hospitali, magereza na vituo vya watoto yatima na wazee ili kutambua kuwa wapo pamoja kwenye jamii.
Mulokozi alisema taasisi hizo zimekuwa zinafanyika kazi kwenye wakati mgumu hasa kipindi hiki cha uwepo wa janga la corona hivyo wanapaswa kuungwa mkono kwa kupatiwa vifaa hivyo.
Alisema taasisi za serikali watapatiwa vitakasa mikono na vituo vya watoto yatima na wazee watapatiwa chakula, sabuni, mafuta ya kupikia na vitakasa mikono.
Mkuu wa kituo cha wazee cha Sarame Magugu, Samson Munuo aliishukuru kampuni ya Mati Super Brand kwa kuwapatia msaada huo wazee hao.
Munuo alisema jamii kwa ujumla inapaswa kuiga mfano huu wa kusaidia wazee hasa wa kituo cha Sarame katika masuala mbalimbali ya kijamii kwani hivi sasa nguvu za kujitegemea wenyewe zimewaishia.