Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Bw. Andrew Massawe, akizungumza na menejimenti ya OSHA (hawapo pichani) alipotembelea ofisi hizo.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, akimsikiliza Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Bw. Andrew Massawe (hayupo pichani) wakati wa kikao baina ya menejimenti ya OSHA na Katibu Mkuu huyo.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda (wa kwanza kulia), Mkurugenzi wa Usalama na Afya, Alexander Ngata (wa pili kulia) na wajumbe wengine wa menejimenti, wakimsikiliza Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Bw. Andrew Massawe (hayupo pichani) alipofanya ziara katika ofisi za taasisi hiyo.
*********************************
Na Mwandishi Wetu
Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umetakiwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ikiwemo kuelimisha wananchi kuhusu masuala ya Usalama na Afya kazini ili kupunguza ajali na magonjwa yanayoweza kutokea katika sehemu za kazi.
Agizo hilo limetolewa na Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Bw. Andrew Massawe, alipotembelea ofisi za OSHA kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa maagizo mbali mbali ya kiutendaji ambayo aliyoyatoa kwa viongozi wa taasisi hiyo mwezi Januari.
“Nimefurahi kuona kuwa maagizo yote niliyoyatoa mwezi Januari mmeyatekeleza kama tulivyokubaliana lakini bado tunahitaji kuongeza nguvu zaidi katika kusimamia sheria, kutoa elimu kwa umma, kushughulikia changamoto za wadau wetu kwa haraka zaidi kwa njia ya majadiliano na hivyo kutimiza azma yetu ya kulinda nguvu kazi kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa letu,” alisema Bw. Massawe katika kikao chake na menejimenti ya OSHA.
Katika kikao hicho, Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, alitoa taarifa ya utekelezaji wa maagizo mbali mbali ambayo yalitolewa na Katibu Mkuu huyo alipotembelea ofisi za OSHA mwezi Januari.
Miongoni mwa maagizo yaliyotolewa na Katibu Mkuu na kutekelezwa na menejimenti ya OSHA ni pamoja na kuanzisha mfumo wa kieletroniki wa usajili na usimamizi wa sehemu za kazi (WIMS), kuanza kutumia mifumo mingine ya serikali, kuanzisha programu mbali mbali endelevu za kuelimisha wananchi na kuboresha tovuti ya taasisi.
Baada ya kupokea taarifa hiyo, Bw. Massawe alieleza kuridhishwa kwake na utekelezaji wa maagizo yake na kuwasisitiza viongozi wa OSHA kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuboresha zaidi huduma za OSHA kwa wananchi.
OSHA ni taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana,Ajira na wenye Ulemavu ambayo ina jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 ambayo inalenga kuboresha mazingira ya kazi hapa nchini.