Na. Alex Sonna, Dodoma
Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mhe. Peter Msigwa ametangaza rasmi nia ya kugombea Urais itakapofika Oktoba 2020 kupitia chama hicho.
Kauli hiyo ameitoa leo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa Habari ambapo pia alisindikizwa na wabunge wenzake, Godbless Lema, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ Hawa Mwaifunga na John Heche.
Mhe. Msigwa ameainisha vipaumbele vitatu pale watanzania watakapo mpatia ridhaa ya kuongoza kuwa ni Uchumi imara, kusimamia utawala bora na kuboresha elimu nchini.
Aidha Mhe. Msigwa amesema kuwa endapo atapata ridhaa ya kuwa Rais atahakikisha anafumua muundo mzima wa Elimu nchini na kuweka mwingine utakaokua na matokeo chanya kwa Taifa.
Mhe. Msigwa ameeleza kuwa mfumo wa elimu uliopo hivi sasa unaegemea zaidi vyeti na wala hauwapi wasomi mwanga wa kuwa wataalamu wa kuvumbua zaidi badala yake wanakua tegemezi ilihali ni wasomi.
” Nikipata ridhaa ya kuwa Rais nitahakikisha nafanya maboresho makubwa kwenye elimu, ni lazima tuwe na Nchi ya wavumbuzi wanaotafuta suluhihisho kitaalamu, tuondokane na elimu ya vyeti ”,ameweka wazi Mhe. Msigwa.
Mhe. Msingwa amesema kuwa kama Taifa hatuwezi kufanikiwa kwa kuwa na watu wenye fikra ndogo, tofauti yetu na wenzetu walioendelea ni upanuzi wa fikra na ukubwa wa elimu yao, tunapaswa kuwekeza kwenye elimu kama kweli tunataka kufikia uchumi wa kati unaotokana na viwanda.
Pia Mhe. Msigwa amesema mfumo uliopo pia unahitaji mabadiliko makubwa kwani huu wa sasa umepitwa na wakati na hauwezi kuwasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi.
Amewaomba watanzania watakapoenda kuchagua Rais Oktoba 25 mwaka huu wachague Kiongozi mwenye maono ya kuwavusha kiuchumi na mwenye uwezo wa kuvutia wawekezaji na kutoa wigo mpana pia wa watanzania wenye kujiajiri.
Mhe. Msigwa anakuwa mwanachama wa tatu wa Chadema kutangaza nia ya kugombea Urais hadharani baada ya wanachama wawili Mayjose Majinge na Makamu Mwenyekiti wa Chadema hiko, Tundu Lissu kutangaza azma yao ya kugombea kupitia chama hiko kikuu cha upinzani.