……………………………………………………………………
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inaungana na wadau wote wa haki za watu wenye ualbino duniani katika kuadhimisha “Siku ya Kimataifa ya Kuongeza Uelewa Kuhusu Ualbino” – “International Albinism Awareness Day” ikiwa na kauli mbiu “Haki Sawa kwa Wote: Boresha Afya, Elimu na Ajira kwa Watu wenye Ualbino.”
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha siku hii Desemba 18, 2014 kwa Azimio Na. A/HRC/RES/23/13. Tanzania ikiwa ni mwanachama hai wa umoja huo inao wajibu wa kutekeleza Azimio hilo kwa vitendo.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi inaendelea kutetea haki za watu wenye ualbino na kuweka msukumo wa utekelezaji wa Sheria ya Watu wenye Ulemavu ya Mwaka 2010.
Ni dhahiri kuwa matukio ya mauaji, unyanyapaa, ubaguzi na mateso kwa watu wenye ualbino hapa nchini hivi sasa yamepungua kwa kiwango kikubwa. Tume inapenda kipekee kutambua juhudi kubwa za Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wadau wote kwa juhudi kubwa za kuhakikisha ulinzi na usalama wa watu wenye ualbino.
Aidha, Tume inawataka Wananchi kuachana na imani potofu za kishirikina ambapo baadhi ya wagombea wanaamini kuwa na viungo vya mtu mwenye ualbino kunawapa bahati ya kushinda uchaguzi jambo ambalo linapelekea mauaji, unyanyapaa, ubaguzi na mateso kwa watu wenye ualbino nchini, hasa kipindi hiki ambacho Taifa linaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba Mwaka huu.
Aidha, Tume inawasihi wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapohisi au kuona vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya watu wenye ualibino.
Watu wenye ualbino wanakabiliwa na changamoto nyingine za afya, elimu, na ajira, ambapo juhudi zaidi kutoka kwa wadau wote zinahitajika. Hivyo Tume inaiomba Serikali kuendeleza juhudi za kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba, hususan mafuta ya kupunguza ukali wa mionzi ya jua (sunscreen lotions), kofia, miwani kwa ajili ya kulinda macho yao, vifaa saidizi vya kielimu na fursa za ajira kwa watu wenye ualbino ili waweze kushiriki kikamilifu katika kutoa mchango wao katika ujenzi wa Taifa.
Vilevile, Serikali iwatumie vyema watalaamu wake kutoa elimu kwa jamii kuhusu ualbino na ushiriki wa familia na jamii katika kuhakikisha watu wenye ualbino wanatambulika na kuandikishwa shuleni kwa kuzingatia uhitaji wao.
Mwisho, Tume inaahidi kuendelea kushirikiana na wadau wote katika kuhakikisha haki za watu wenye ualbino zinalindwa, zinakuzwa na kutetewa nchini.
Imetolewa na:
(SIGNED)
Mathew Pauwa Mhina Mwaimu (Jaji Mstaafu)
Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA