Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii (wa pili kulia) akifuatilia maelezo ya ujenzi wa makumbusho ya nyao za Zamadamu kutoka kwa Meneja urithi na Utamaduni wa NCAA Eng. Joshua Mwankunda.
Mtaalam wa Urithi wa Utamaduni wa NCAA Bw. Melkizedeck Mwambungu (Kulia) akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Prof Adolf Mkenda kuhusu maendeleo ya ujenzi wa Makumbusho ya nyayo za Binadamu Laetoli.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Prof. Aolf Mkenda ( wa tatu kutoka kulia) akisikiliza maelezo kutoka kwa Mhandisi Joshua Mwamkunda (kulia) kuhusu mawe yaloyotumika kufunika nyao za binadamu wa kale ambazo zimehifadhiwa ili zisiharibike.
********************************
Na Mwandhishi wetu NCAA.
Katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Prof. Adolf Mkenda ametembelea na kukagua eneo lenye nyayo za binadamu wa kale duniani (Zamadamu) na kuelekeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kuongeza kasi ya ujenzi wa makumbusho katika eneo hilo kwa ajili ya kulilinda na kuhifadhi nyayo hizo ambazo ni urithi wa dunia.
Prof. Mkenda ameipongeza NCAA kwa juhudi za kuhifadhi na kulinda nyayo hizo pamoja na uamuzi wa kujenga makumbusho ya kisasa itakayowezesha kulinda na kuhifadhi nyao hizo kwa njia ya kisasa zaidi na kuongeza thamani ya eneo la Laetoli kama sehemu pekee duniani iliyothibitishwa kisayansi kuwa binadamu alisimama na kutembea kwa miguu yake miwili miaka milioni 3.6 iliyopita.
“Tusichelewe kukamilisha mradi wa ujenzi wa makumbusho haya ya kisasa , nimeona kuna kazi kubwa inafanyika ambapo kwa sasa nyayo zimefunikwa kwa mawe meusi na njia nyinginezo kama sehemu ya kuzilinda zisiharibike, tukamilishe ujenzi wa mradi huu ili kuhifadhi kisasa maana ndio sehemu pekee inayobitisha kisayansi kuwa binadamu wa kwanza alitembea kwa miguu miwil miaka 3.6 milioni iliyopita hapa Ngorongoro Tanzania”.
Katibu mkuu huyo ameelekeza wataalam NCAA kwa kushirikiana na Chuo kikuu cha St. pertersberg, Chuo kikuu cha Dar es Salaam, wanajolojia na akiolojia kuandaa mkutano wa pamoja ili kukubaliana njia ya kisayansi ya kutunza na kulinda nyayo hizo kwa njia iliyobora zaidi. Ameongeza kuwa kwa sasa Tanzania imeendelea kuzingatia tahadhari zote za Covid-19 na anga liko wazi, kwa hiyo wataalam wa UNESCO wanaweza kuja kujadiliana njia bora za kutunza eneo hilo.
“ Tusipunguze kasi ya ujenzi wa eneo hili, Covid 19 imeanza kupungua, iteni wale wataalam wa UNESCO ili mjadiliane haraka ikiwezekana kazi ikamilike na mwisho wa mwaka tufungue eneo hili, tunajua muda hautusubiri na tukipoteza nyayo hizi hatuzipati tena, tunalinda faru, tembo na Wanyama wengine ambao wanazaliana na kuongezeka, lakini nyao hizi tukipoteza hatuzipati tena, tuongeze kasi na kama kuna changamoto ya fedha tutashirikiana ili Serikali yetu ituwezeshe kukamilisha mradi huu”. Aliongeza Prof. Mkenda.
Kwa upande wake Meneja wa Idara ya urithi na Utamaduni wa NCAA Mhandisi Joshua Mwankunda ameeleza kuwa zipo sababu za kisayansi za kuendelea kuhifadhi nyayo hizo na ndio maana kwa sasa wamefanya utaratibu wa kuzihifadhi kwa kufunika na mawe meusi ili zitakapofungiliwa na kuhifadhiwa kisasa hapo baadae zibaki katika uhalisia wake bila kupata fangasi, kupukutika au kupata vumbi.
“ Hatua za ujenzi wa miundombinu ya makumbusho haya ni shemu ya maandalizi ya mfumo wa kuzihifadhi kwa kutumia vioo maalum zikiwa zimefunikwa na kuhifadhiwa kitaalam, kwa sasa tupo katika hatua nzuri za ujenzi na tunasubiri makubaliano tu ya wanasayansi wa kidudia tukubaliana kwa pamoja namna bora ya kuzihifadhi na kuzilinda ili ziwe endelevu kwa na vizazi vijavyo.
Afisa Urithi wa Utamaduni ambaye pia ndio mkuu wa Kituo cha Laetoli Bw. Melkizedeck Mwambungu ameeleza kuwa uwepo wa nyayo hizo katika Hifadhi ya Ngorongoro umeiongezea hadhi nchi yetu kwa sababu ni sehemu ya urithi wa dunia ikijumuisha pia sehemu yenye chimbuko la fuvu la binadamu wa kale Zinjathropus katika Bonde la Olduvai ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Jumuiya zakimataifa kama UNESCO ni wadau wakubwa sana wa hii sehemu na tunafanya nao vikao vingi kuhusiana na kutunza na kuhifadhi eneo hili, huwa tunashaurina na kukaa pamoja na kuhakikisha kuwa eneo hili linalindwa na kuwa salama kwavizazi vijavyo.