Home Mchanganyiko MUHTASARI WA HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA DKT. PHILIP...

MUHTASARI WA HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA DKT. PHILIP I. MPANGO (MB), AKIWASILISHA BUNGENI TAARIFA YA HALI YA UCHUMI WA TAIFA KWA MWAKA 2019 NA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2020/21

0

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, (kushoto) akiwa na Wakuu wa Taasisi na Idara wa Wizara hiyo, wakati Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akiwasilisha bungeni Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21, jijini Dodoma.

4.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (kulia) akiwa katika mazungumzo na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Mashimba Ndaki, baada ya Waziri huyo kuwasilisha bungeni Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21, jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kulia), akifurahia jambo wakati Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Philip Isdor Mpango (Mb), akiwasilisha bungeni Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21, jijini Dodoma, kushoto ni Naibu Waziri wa Madini Mhe. Stanslaus Nyongo

Mhasibu Mkuu wa Serikali, Bw. Francis Mwakapalila (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara ya Fedha na Mipango, baada ya kuwasilishwa bungeni Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21, jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akiwasilisha bungeni Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21, jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (kulia) akizungumza jambo na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Edwin Mhede, baada ya  kuwasilishwa bungeni Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21, jijini Dodoma

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM, Dodoma)

******************************

Juni, 2020                                                                    Dodoma

 

UTANGULIZI

 

 1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee na kujadili Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21. Pamoja na hotuba hii ninawasilisha vitabu vya Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21. Taarifa hizi ndiyo msingi wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/21 nitakayowasilisha hapa Bungeni leo jioni.  

 1. Mheshimiwa Spika, awali ya yote nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutujalia afya njema. Aidha, naendelea kumshukuru kwa kulijalia Taifa letu amani, utulivu na mshikamano na kutuwezesha kukutana katika mkutano huu wa 19 na wa mwisho wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kujadili namna ya kuharakisha maendeleo ya Taifa letu.

 1. Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze kwa dhati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi anavyoendelea kuliongoza vema Taifa letu. Kwa kipindi hiki cha miaka minne na nusu ya utawala wake tumeshuhudia kuimarika kwa uchumi, mfumuko wa bei umedhibitiwa, miradi mikubwa ya maendeleo inatekelezwa, uwajibikaji katika utumishi wa umma umeimarika na kero za wananchi wanyonge zinatatuliwa. Kipekee napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniamini kuongoza Wizara ya Fedha na Mipango tangu mwanzo wa uongozi wake hadi sasa.

 

 1. Mheshimiwa Spika, vile vile, napenda kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao kwa uongozi wao mahiri wameendelea kumshauri vema Mheshimiwa Rais katika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.

 1. Mheshimiwa Spika, Napenda pia kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Waziri wa Katiba na Sheria pamoja na Mheshimiwa Dkt. Godwin Aloyce Mollel (Mb), kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

 

 1. Mheshimiwa Spika, napenda pia nitumie nafasi hii kutoa salamu za pole kwako, Waheshimiwa Wabunge na Wananchi wote kwa ujumla kwa kuondokewa na Mheshimiwa Rashid Ajali Akbar, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini (CCM), Mheshimiwa Mchungaji  Dkt. Getrude Pangalile Rwakatare, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mheshimiwa Richard Mganga Ndassa, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Sumve (CCM), na Mheshimiwa Balozi Dkt. Augustine Philip Mahiga, Mbunge wa kuteuliwa (CCM) aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi. Amina!

 

 1. Mheshimiwa Spika, nchi yetu imepata mvua nyingi zilizo juu ya wastani hali iliyopelekea kutokea kwa mafuriko katika maeneo mbalimbali. Mafuriko haya yamesababisha uharibifu mkubwa wa mazao ya wakulima, mali na miundombinu hususan barabara, reli na madaraja. Mafuriko hayo yameathiri utelekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuongeza gharama za ukarabati wa miundombinu iliyoharibika. Kwa msingi huo, katika mwaka 2020/21 kipaumbele ni kukarabati miundombinu iliyoharibika.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu, nchi yetu na dunia kwa ujumla ilikabiliwa na mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaojulikana kama COVID – 19 inayosababishwa na virusi vya Corona. Ni dhahiri kuwa ugonjwa huu umeathiri uchumi wa nchi nyingi duniani kutokana na vifo, kuongezeka kwa gharama za utoaji huduma katika sekta ya afya na kuathiri shughuli za biashara na uzalishaji hususan kwa nchi zinazotegemea utalii.

 

 1. Mheshimiwa Spika, jambo jema ni kuwa nchi yetu haikuathirika sana na ugonjwa huu kutokana na hatua madhubuti zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi imara wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kama Taifa tuliendelea kumtegemea Mwenyezi Mungu, kuchukua tahadhari za kiafya kama inavyoshauriwa na wataalam pamoja na kufanya kazi kwa bidii. Aidha, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na ugonjwa huu ambapo hadi sasa Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 15.49 kwa  ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na kinga. Hatua nyingine ni pamoja na: kutolewa msamaha wa kodi kwa aina 15 za vifaa vya kupambana na COVID – 19; kutoa elimu ya jinsi ya kujikinga na maambukizi; kutenga maeneo maalum kwa ajili ya uangalizi kwa wasafiri wanaoingia nchini na wanaobainika kuwa na dalili za ugonjwa huu; na kuanzishwa kwa huduma ya namba maalum ya kupiga simu bila malipo kwa ajili ya msaada wa kiafya. Vile vile, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania imechukua hatua mbalimbali za Sera ya Fedha ili kulinda na kuimarisha uchumi zikijumuisha: kushusha kiwango cha chini cha kisheria cha sehemu ya amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu ya Tanzania kutoka asilimia 7 hadi 6; kushusha kiwango cha riba kinachotozwa kwa benki kukopa Benki Kuu kutoka asilimia 7 hadi 5; kupunguza kiwango cha dhamana za Serikali kutoka asilimia 10 hadi 5 kwa dhamana za muda mfupi na kutoka asilimia 40 hadi 20 kwa hati fungani; na kuzielekeza kampuni zinazotoa huduma za fedha kwa njia ya mtandao kuongeza kiwango cha miamala kwa siku kwa mteja kutoka shilingi milioni 3 hadi 5 na kiwango cha akiba kwa siku kwa wateja kutoka shilingi milioni 5 hadi 10.

 

 1. Mheshimiwa Spika, kutokana na hatua madhubuti zilizochukuliwa na Serikali, hivi sasa hali imeimarika ambapo shughuli za kiuchumi na kijamii zinaendelea kufanyika kama awali. Serikali imeruhusu vyuo vikuu vimefunguliwa, wanafunzi wa kidato cha sita wamerudi shuleni kujiandaa na mitihani, shughuli za michezo yote zimeruhusiwa,  anga limefunguliwa ambapo ndege za mizigo na abiria zinaendelea kuingia nchini na hivyo kupokelewa kwa watalii kutoka nchi mbalimbali. Hii ni ishara dhahiri ya uongozi imara wa Mheshimiwa Rais kwa Taifa hususan katika kipindi cha majanga na misukosuko mikubwa kwa dunia kama ugonjwa huu.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21 zimezingatia dhana ya ushirikishwaji mpana wa wadau katika hatua za uandaaji na maamuzi katika ngazi zote Serikalini. Nitambue mchango mkubwa wa Bunge lako Tukufu chini ya uongozi wako Mheshimiwa Job Yustino Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, napenda kumshukuru Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki (Mb), Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na wajumbe wote wa Kamati hiyo kwa ushauri makini waliotupatia. Ushauri wao umezingatiwa kikamilifu katika uandaaji wa taarifa nilizowasilisha mbele ya Bunge hili.

 1. Mheshimiwa Spika, maandalizi ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21 yamezingatia vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano vilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21, Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 na ahadi za Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizotoa wakati akifungua rasmi Bunge la Kumi na Moja. Aidha, katika mwaka 2020/21 msukumo mkubwa utawekwa katika kukamilisha utekelezaji wa miradi inayoendelea ili kupata matokeo tarajiwa.

 

MWENENDO WA HALI YA UCHUMI 2019

 

Uchumi wa Dunia

 

 1. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ya Aprili 2020, uchumi wa dunia ulikua kwa asilimia 2.9 mwaka 2019. Aidha, uchumi wa dunia unakadiriwa kuporomoka na kufikia ukuaji wa asilimia hasi 3.0 mwaka 2020 ambao kwa kiasi kikubwa utachangiwa na athari za mlipuko wa ugonjwa wa COVID – 19. Katika mwaka 2021 uchumi wa dunia unatarajiwa kuimarika na kufikia ukuaji wa asilimia 5.8 kutokana na matarajio ya kutoweka kwa virusi vya Corona katika nusu ya pili ya mwaka 2020 na hatimaye, kuimarika kwa shughuli za kiuchumi duniani ikijumuisha biashara na uzalishaji viwandani na utekelezaji wa sera za kuongeza ukwasi katika nchi mbalimbali.

Uchumi wa Afrika na Kikanda

 

 1. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, kasi ya ukuaji wa uchumi ilifikia asilimia 3.1 mwaka 2019. Matarajio ya ukuaji wa uchumi ni kupungua na kufikia wastani wa asilimia hasi 1.6 mwaka 2020 kutokana na athari za mlipuko wa ugonjwa wa COVID – 19. Aidha, ukuaji wa uchumi katika nchi za ukanda huo, unatarajiwa kuimarika na kufikia wastani wa asilimia 4.1 mwaka 2021. Ongezeko hilo litatokana na jitihada za kupambana na ugonjwa wa COVID – 19, matarajio ya kuongezeka kwa misaada kutoka nchi zilizoendelea kwa ajili ya kupambana na ugonjwa huo na matarajio ya utulivu wa bei ya nishati ya mafuta katika soko la Dunia.

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019, uchumi wa nchi za ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliendelea kuimarika ambapo Tanzania ilikuwa na ukuaji wa asilimia 7.0, Rwanda asilimia 9.4, Uganda (asilimia 4.9) na Kenya asilimia 5.4. Aidha, kutokana na athari za COVID-19, ukuaji wa uchumi wa ukanda wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki unatarajiwa kupungua kidogo kwa mwaka 2020 na hatimaye kuanza kuimarika mwaka 2021 kutokana na juhudi zinazochukuliwa na nchi wanachama katika kupambana na athari za COVID-19 zikiwemo hatua za kifedha na kibajeti pamoja na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo katika sekta za uchukuzi (reli, barabara na madaraja) maji, nishati, elimu na afya.

Uchumi wa Taifa

 

Pato la Taifa

 

 1. Mheshimiwa Spika, mwaka 2019, Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 7.0 kama ilivyokuwa mwaka 2018. Ukuaji huu ulitokana na uwekezaji hususan katika miundombinu ikiwemo: ujenzi wa barabara, reli na viwanja vya ndege; kutengamaa kwa upatikanaji wa nishati ya umeme; kuimarika kwa huduma za usafirishaji; kuongezeka kwa uzalishaji wa madini hususan dhahabu na makaa ya mawe; na kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo. Sekta zilizokua kwa viwango vikubwa katika kipindi hicho ni pamoja na uchimbaji madini na mawe (asilimia 17.7), ujenzi (asilimia 14.8), sanaa na burudani (asilimia 11.2), na usafirishaji na uhifadhi mizigo (asilimia 8.7). Kwa mwaka 2020, ukuaji wa Pato la Taifa unatarajiwa kupungua kidogo kutoka maoteo ya awali ya asilimia 6.9 hadi 5.5 kutokana na hatua madhubuti zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hususan kuhimiza wananchi waendelee kufanya kazi wakati wanachukua tahadhari dhidi ya corona kama inavyoelekezwa na wataalam wa afya pamoja na matarajio ya kuimarika kwa uchumi wa kikanda na dunia.

 1. Mheshimiwa Spika, mwaka 2019, Pato la wastani la kila mtu lilikuwa shilingi 2,577,967 ikilinganishwa na shilingi 2,452,406 mwaka 2018, sawa na ongezeko la asilimia 5.1. Vile vile, Pato la wastani kwa kila mtu katika dola za Marekani liliongezeka hadi kufikia dola za Marekani 1,121 mwaka 2019 kutoka dola za Marekani 1,078 mwaka 2018.

Mwenendo wa Bei

 

 1. Mheshimiwa Spika, mwaka 2019, mwenendo wa mfumuko wa bei uliendelea kubaki katika wigo wa tarakimu moja ambapo ulifikia wastani wa asilimia 3.4 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.5 mwaka 2018. Mfumuko wa bei za nishati umeendelea kupungua na kufikia asilimia 4.1 Aprili 2020 kutoka asilimia 13.3 Aprili 2019 kutokana na kupungua kwa bei za nishati ya mafuta katika soko la dunia.

Utekelezaji wa Sera ya Fedha 2019/20

 1. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Benki Kuu imeendelea kutekeleza sera ya fedha ya kuongeza ukwasi kwenye uchumi ambayo imesaidia kupunguza viwango vya riba katika masoko ya fedha hususan riba za mikopo na amana. Wastani wa riba za mikopo ya benki kwa ujumla katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020 ulipungua hadi asilimia 16.85 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 17.16 katika kipindi kama hicho mwaka 2018/19, na riba za mikopo ya kipindi cha mwaka mmoja zimepungua na kufikia wastani wa asilimia 16.24 kutoka asilimia 17.79. Vile vile, wastani wa riba za amana kwa ujumla ulikuwa asilimia 7.02 katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020, ikilinganishwa na wastani wa asilimia 7.62 katika kipindi kama hicho mwaka 2018/19. Aidha, riba za amana za kipindi cha mwaka mmoja ziliongezeka na kufikia wastani wa asilimia 8.77 katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020 kutoka wastani wa asilimia 8.21 katika kipindi kama hicho mwaka 2018/19.

Ujazi wa Fedha na Karadha

 1. Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020, wastani wa ukuaji wa ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) uliongezeka kwa asilimia 9.9 na kufikia shilingi trilioni 28.8 mwezi Aprili 2020 kutoka shilingi trilioni 25.6 mwezi Aprili 2019. Ongezeko hili la ujazi wa fedha ni matokeo ya utekelezaji thabiti wa sera ya fedha, ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi pamoja na rasilimali fedha za kigeni katika sekta ya benki.

Mwenendo wa Mikopo kwa Sekta Binafsi

 1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020, wastani wa ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi ulikuwa asilimia 8.7 kufikia shilingi trilioni 19.7 ikilinganishwa na shilingi trilioni 18.6 Aprili 2019. Sehemu kubwa ya mikopo ilielekezwa kwenye shughuli binafsi (asilimia 31.1) ikifuatiwa na shughuli za biashara asilimia 17.6, uzalishaji viwandani asilimia 11.0 na kilimo asilimia 7.7.

 

Sekta ya Nje

 

 1. Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2020, urari wa jumla wa malipo ulikuwa na ziada ya dola za Marekani milioni 897.1 ikilinganishwa na nakisi ya dola za Marekani bilioni 1.1 katika kipindi kama hicho mwaka 2019. Hii ilichangiwa na kupungua kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho wa mali nchi za nje kulikotokana na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa nje ya nchi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, nakisi kwenye urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho mali nchi za nje ulipungua hadi kufikia dola za Marekani milioni 333.3 mwezi Aprili 2020, ikilinganishwa na nakisi ya dola za Marekani bilioni 1.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2019. Kupungua huku kulitokana na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa nje ya nchi, hususa katika bidhaa asilia na zisizo asilia kama vile dhahabu.

 

 1. Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2020, mauzo ya bidhaa na huduma nje yaliongezeka kufikia dola za Marekani bilioni 8.6 ikilinganishwa na dola za Marekani bilioni 7.3 Aprili 2019. Hii ilichangiwa na kuanzishwa kwa masoko ya madini nchini kulikopelekea kuongezeka kwa mauzo ya dhahabu sanjari na ongezeko la bei katika soko la dunia. Thamani ya uagizaji bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi ilikuwa dola za Marekani bilioni 8.6, ikilinganishwa na dola za Marekani bilioni 8.7 katika kipindi kama hicho mwaka 2019. Sehemu kubwa ilitumika katika uagizaji mafuta na bidhaa za mitaji ikiwemo mitambo na mashine inayotumika katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu ya reli, barabara, madaraja na uzalishaji umeme.

Akiba ya Fedha za Kigeni

 

 1. Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2020, akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani bilioni 5.3, kiasi kinachotosheleza kulipia uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha miezi 6.1. Kiwango hiki ni zaidi ya lengo la nchi la miezi 4.0, ambayo ni juu ya lengo la nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki la miezi isiyopungua 4.5 na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika la miezi isiyopungua 6.0.

Mwenendo wa Thamani ya Shilingi

 

 1. Mheshimiwa Spika, thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya sarafu nyingine kubwa duniani imeendelea kuwa tulivu kwa kipindi chote cha mwaka 2019/20. Katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020, dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa kati ya shilingi 2,299.3 na shilingi 2,302.7 katika soko la fedha la jumla ikilinganishwa na wastani wa kati ya shilingi 2,276.4 na shilingi 2,300.9 kwa dola moja ya Marekani katika kipindi kama hicho mwaka 2018/19.

Deni la Serikali

 

 1. Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2020, deni la Serikali lilifikia shilingi trilioni 55.43. Kati ya kiasi hicho, deni la nje lilikuwa shilingi trilioni 40.57 na deni la ndani shilingi trilioni 14.85. Deni la Serikali lilichangiwa na kupokelewa kwa mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo inayochochea kasi ya ukuaji wa uchumi. Matokeo ya tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Desemba 2019, imeonesha kuwa deni la Serikali ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.

 

Utafiti wa Sekta Isiyo Rasmi     

 

 1. Mheshimiwa Spika, mwaka 2019/20, Serikali ilifanya utafiti wa Sekta Isiyo Rasmi mkoani Dar es Salaam kwa lengo la kubaini mchango wa sekta hiyo kwenye Pato la Taifa kwa kutumia makadirio ya mapato na ongezeko la thamani ya uzalishaji wa bidhaa na huduma kutoka shughuli za kilimo na zisizo za kilimo; tija katika uwekezaji; kiwango cha ukuzaji mtaji; kutambua mahali biashara zilipo; thamani ya uzalishaji kwa kila mtu; ajira na mgawanyo wake; na mahusiano kati ya Sekta Isiyo Rasmi na sekta nyingine za kiuchumi.

 1. Mheshimiwa Spika, matokeo ya utafiti huo yanaonesha kuwa: Mkoa wa Dar es Salaam una wamiliki wa shughuli za Sekta Isiyo Rasmi wapatao 1,023,520 ambapo asilimia 47.6 wanajihusisha na biashara ya jumla na rejareja pamoja na matengenezo ya magari na pikipiki;   uwekezaji wa mitaji katika sekta isiyo rasmi ni shilingi bilioni 901.5 kwa mwaka 2019; jumla ya ongezeko la thamani kwa mwaka katika bidhaa na huduma zinazozalishwa katika sekta isiyo rasmi ni shilingi trilioni 6.2; na ajira katika sekta isiyo rasmi kwa watu wenye umri wa miaka 15 au zaidi imepungua kutoka watu 1,208,250 (asilimia 61.5) mwaka 2014 hadi 1,154,336 (asilimia 55.2) mwaka 2019. Hii inatokana na juhudi kubwa za Serikali ya Awamu ya Tano katika kupanua wigo wa kujenga uchumi wa viwanda ambao matokeo yake ni kukuza upatikanaji wa kazi zenye staha (decent work) na kuongezeka kwa ajira katika sekta rasmi.

 

 1. Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu hali ya uchumi yapo katika Aya ya 9 hadi 26 ya hotuba yangu na kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019.

 

MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO KWA KIPINDI CHA 2016/17 – 2019/20

 

 1. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka minne na nusu ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano (2016/17 – 2019/20), yamepatikana mafanikio mbalimbali katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo yakiwemo:

(i)          Ukuaji wa Uchumi: uchumi wa Taifa uliendelea kuimarika ambapo ulikua kwa wastani wa asilimia 6.9 na mfumuko wa bei kuendelea kupungua na kubaki katika wigo wa tarakimu moja, chini ya wastani wa asilimia 5.0;

 

(ii)        Reli: Ujenzi wa  reli ya kati ya standard gauge unaendelea ambapo, ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (km 300) umefikia asilimia 76.63 na kwa kipande cha Morogoro – Makutupora (km 422) umefikia asilimia 28. Hadi Mei 2020, ujenzi wa reli ya standard gauge umetumia shilingi bilioni 170, pamoja na dola za Marekani bilioni 1.5. Mradi huu umezalisha takribani ajira 13,117 na zabuni zenye thamani ya shilingi bilioni 664.7 kwa kampuni za ndani;

(iii)       Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere – MW 2,115: Kazi zilizokamilika ni pamoja na ujenzi wa miundombinu wezeshi ya mradi (njia ya kusafirisha umeme, barabara kwa kiwango cha changarawe, mfumo wa maji, mawasiliano ya simu na nyumba za makandarasi); ujenzi wa daraja la muda namba 2; utafiti wa miamba na udongo; na uchimbaji wa mtaro wa chini kwa chini (adit tunnel) wenye urefu wa mita 147.6 na mtambo wa kuchakata kokoto namba moja ambapo utekelezaji wa mradi wote umefikia asilimia 10.74. Aidha, jumla ya shilingi trilioni 1.42 zimetumika kugharamia mradi na ajira zipatazo 3,897 zimezalishwa;

(iv)       Nishati: kukamilika kwa mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa Msongo wa kV 220 kutoka Makambako – Songea ambapo shilingi bilioni 160.1 zimetumika; kuendelea na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kV 400 kutoka Singida – Arusha – Namanga ambapo utekelezaji umefikia asilimia 67 na shilingi bilioni 219.4 zimetumika; kuendelea na utekelezaji wa miradi ya usambazaji umeme vijijini kupitia REA ambapo shilingi trilioni 2.27 zimetumika jumla ya vijiji 9,112 kati ya vijiji 12,268 vya Tanzania Bara vimeunganishwa umeme, sawa na asilimia 74.3. Hadi Mei 2020, kiwango cha upatikanaji wa umeme (overall electricity access rate) kimefikia asilimia 84.6 kutoka asilimia 67.8 mwaka 2016;

(v)        Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania: Serikali imeendelea kuboresha Shirika la Ndege kwa kununua ndege mpya 11. Kati ya hizo, ndege nane (8) zenye thamani ya shilingi trilioni 1.27 zimepokelewa na malipo ya awali ya shilingi bilioni 85.7 kwa ajili ya ununuzi wa ndege nyingine mpya tatu (3) yamefanyika ambapo ndege mbili (2) ni aina ya Airbus A220-300 na moja (1) ni aina ya De Havilland Dash 8-400;

(vi)       Viwanja vya Ndege: kukamilika kwa ujenzi na ukarabati wa viwanja vya Ndege vya Mwanza awamu ya kwanza, Nachingwea na Kilimanjaro (KIA); kuendelea na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya Geita (asilimia 78) na Songea (asilimia 34). Aidha, ujenzi wa Jengo la Tatu la Abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere umekamilika na kuanza kutumika ambapo kiasi cha Euro milioni 276 sawa na takribani shilingi bilioni 722.1 zilitumika;

(vii)     Bandari: kukamilika kwa ujenzi wa Gati Na.1, 2, 3, 4 na Gati la kupakia na kupakua magari (Ro-Ro) katika bandari ya Dar es Salaam; ujenzi wa gati lenye urefu wa mita 300 katika bandari ya Mtwara umefikia asilimia 61; na kukamilika kwa uongezaji wa kina cha bandari ya Tanga na ujenzi wa Gati namba 2 umefikia asilimia 60. Aidha, kwa upande wa Bandari za Maziwa Makuu: katika Ziwa Victoria – ujenzi wa magati ya Lushamba, Ntama,  Nyamirembe, Magarine na Gati la majahazi Mwigobero umekamilika; kununuliwa kwa vifaa vya kuhudumia mizigo na meli; na ukarabati wa majengo na ofisi za bandari. Ziwa Tanganyika – uboreshaji wa Gati la Kagunga umekamilika; ujenzi wa Gati la Sibwesa umefikia asilimia 98; ujenzi wa miundombinu na Gati la Bandari ya Kabwe umefikia  asilimia 56; na ujenzi wa miundombinu na Gati la Bandari ya Lagosa umefikia asilimia 53. Ziwa Nyasa – ujenzi wa sakafu ngumu kwa ajili ya maegesho katika bandari ya Kiwira; na ujenzi wa Gati la Ndumbi umekamilika;

(viii)    Ujenzi na Ukarabati wa Meli katika Maziwa Makuu: kukamilika kwa ujenzi wa meli moja mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na mizigo tani 200 katika Ziwa Nyasa, ukarabati wa meli ya MV Victoria katika ziwa Victoria na meli ya mafuta ya MT. Sangara katika Ziwa Tanganyika; kukamilika kwa asilimia 98 ya ujenzi wa Chelezo na MV Butiama asilimia 98; na kuendelea na ujenzi wa meli mpya (MV Mwanza) yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Victoria ambapo utekelezaji umefikia asilimia 60;

(ix)       Barabara na Madaraja: ujenzi wa Barabara: kukamilika kwa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zenye urefu wa jumla ya kilometa 2,624.27 na kuendelea na ujenzi wa barabara kuu kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilometa 1,298.44; barabara ya njia nane kutoka Kimara hadi Kibaha (km 19.2) umefikia asilimia 80; na ujenzi wa Ubungo Interchange umefikia asilimia 77. Madaraja: kukamilika kwa ujenzi wa madaraja ya Mfugale (Dar es Salaam), Magufuli katika mto Kilombero (Morogoro), Momba (Rukwa), Sibiti (Singida), Mara (Mara), Lukuledi (Lindi), Mangara (Manyara) na Kavuu (Katavi); kuendelea na ujenzi wa madaraja ya Kitengule (Kagera) asilimia 50, Ruhuhu (Ruvuma) asilimia 86, Msingi (Singida) asilimia 40, New Wami (Pwani) lenye urefu wa mita 513.5 na barabara unganishi zenye kilomita 4.3 umefikia asilimia 39 na daraja jipya la Selander lenye urefu wa kilomita 1.03 na barabara unganishi zenye kilomita 5.2 umefikia asilimia 38.2; na kuanza kwa ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi (Mwanza) lenye urefu wa kilomita 3.2  ambapo malipo ya awali ya shilingi bilioni 61.4 yamefanyika.

 

(x)        Kilimo, Mifugo na Uvuvi: katika Kilimo, miche bora ya korosho 12,252,197 imezalishwa na mbolea tani 519,813 imesambazwa katika mikoa 26 ya Tanzania Bara; na kuongezeka kwa upatikanaji wa mbegu bora za mahindi, ngano, maharage, mpunga, soya, alizeti, mtama, ufuta, viazi mviringo na mazao ya bustani kufikia tani 49,040.66. Aidha, kupitia Mradi wa Kuongeza Uzalishaji wa Mpunga (ERPP), shughuli zifuatazo zimetekelezwa: ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu za Kigugu –  Mvomero (hekta 200) asilimia 50, Mvumi – Kilosa (hekta 249) asilimia 84, Kilangali – Kilosa (hekta 600) asilimia 51, Msolwa Ujamaa – Kilombero (hekta 675) asilimia 40 na Njage – Kilombero (hekta 325) asilimia 84. Mifugo: kuendelezwa kwa mashamba matano (5) ya kuzalisha mitamba; kuzalishwa na kusambazwa kwa mitamba 15,097 ya ng’ombe wa maziwa; kununuliwa na kusambazwa kwa lita 8,823.53 za dawa aina ya Paranex ya kuogesha mifugo; kukarabatiwa kwa majosho 1,129; na kutolewa kwa chanjo ya ndigana kali (east coast fever) kwa ng’ombe 70,260. Uvuvi: uzalishaji wa vifaranga 15,041,401 vya samaki; na kuongezeka kwa uvunaji wa samaki (maji ya asili) kufikia tani 470,309.23;

(xi)       Miradi ya Afya: ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya vituo  vya kutolea huduma za afya ya msingi nchini ikijumuisha vituo vya afya 487, hospitali za wilaya 71, hospitali za rufaa za mikoa 10 na zahanati 1,198; kuongezeka kwa bajeti ya dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015/16 hadi shilingi bilioni 269 mwaka 2019/20; kujenga na kuboresha miundombinu ya hospitali za rufaa za Njombe, Simiyu, Mara, Geita, Songwe, Katavi, Sekou Toure (Mwanza), Burigi – Geita, Mwananyamala – Dar es Salaam na hospitali za rufaa za kanda ya kusini Mtwara, kanda ya nyanda za juu kusini Mbeya, hospitali ya Kibong’oto na ujenzi wa Kituo Maalum cha kutenga wagonjwa wa magonjwa yanayoambukiza (Isolation Centre) katika hospitali ya Taifa Muhimbili, Temeke, na Maabara ya Taifa Mabibo; na ununuzi wa dawa, chanjo, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi ikijumuisha vifaa tiba vya kisasa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.

(xii)     Miradi ya Elimu: kukamilika na kuanza kutumika kwa Maktaba ya Kimataifa yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,600 kwa wakati mmoja katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; kuendelea na ujenzi wa maabara ya masomo ya Sayansi katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Kampasi ya Solomon Mahlangu), ujenzi wa hosteli za Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na hosteli za wanafunzi na Maktaba katika Chuo Kikuu Mzumbe (kampasi ya Mbeya); utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka shilingi bilioni 365 mwaka 2015/16 hadi shilingi bilioni 450 mwaka 2019/20; uimarishaji wa vyuo vya VETA na kukuza ujuzi kwa vijana nchini; na ukamilishaji wa maboma 364 ya nyumba za walimu wa shule za msingi kwenye maeneo yenye mazingira magumu na kuendelea kugharamia elimumsingi bila ada ambapo shilingi trilioni 1.03 zimetumika kuanzia mwaka 2015 hadi Mei 2020.

(xiii)    Miradi ya Maji Mijini na Vijijini: Serikali imeendelea kuboresha huduma za maji safi na salama vijijini na mijini ambapo miradi 1,423 (vijijini 1,268 na mijini 155) imetekelezwa na kukamilika kati ya mwaka 2015 na 2019. Miradi hiyo inajumuisha: mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria hadi miji ya Isaka, Tinde, Kagongwa, Tabora, Igunga, Uyui na Nzega ambapo ujenzi wa matanki 17 na ulazaji wa mabomba makubwa ya kusafirisha maji kutoka kijiji cha Solwa – Nzega – Tabora – Igunga (km 290.7) umekamilika. Utekelezaji wa miradi ya maji umewezesha kiwango cha upatikanaji wa maji kufikia asilimia 70.1 vijijini na asilimia 84 mijini;

(xiv)    Madini: Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na marekebisho ya sheria na mikataba ya uwekezaji katika sekta ya madini na hivyo kuanzishwa kwa Kampuni mpya ya Twiga Minerals Corporation Limited inayomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali (hisa asilimia 16) na Kampuni ya Barrick (hisa asilimia 84); na kufanyika kwa malipo ya fidia ya dola za Marekani milioni 100 kutoka Kampuni ya Barrick ikiwa ni sehemu ya kwanza  ya kiasi cha makubaliano ya awali ya kulipa fidia ya dola za Marekani milioni 300. Aidha, marekebisho ya Sheria yamewezesha kuanza kwa majadiliano baina ya Serikali na Makampuni yote makubwa ya madini kwa lengo la kupata asilimia 16 ya hisa kwa Serikali. Mafanikio mengine ni kuanzishwa kwa masoko 28 na vituo 25 vya ununuzi wa madini nchini; kukamilika kwa ujenzi wa vituo vinne (4) vya umahiri katika maeneo ya Bukoba, Handeni, Bariadi na Musoma; kukamilika kwa ujenzi wa viwanda viwili (2) vya mfano vya kuchenjua dhahabu vya Lwamgasa na Katente; kukamilika kwa ujenzi wa one stop center Mirerani, kuimarika kwa udhibiti wa madini ikijumuisha ujenzi wa ukuta wa Mirerani uliowezesha  kupungua kwa utoroshaji madini;  na kuongezeka kwa maduhuli ya Serikali kutoka shilingi bilioni 196 mwaka 2015/16 hadi zaidi ya shilingi bilioni 470 mwaka 2019/20;  na

(xv)     Uendelezaji wa Viwanda: kufanikisha ujenzi wa viwanda vipya 8,477 ambapo viwanda vikubwa ni 201, vya kati 460, vidogo 3,406 na vidogo sana 4,410. Mafanikio mengine ni pamoja na upanuzi wa Kiwanda cha Ngozi na Bidhaa za Ngozi cha Karanga (Moshi) na kuimarisha Shirika la Nyumbu (Pwani).

 1. Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa Mpango yapo katika Aya ya 32 na 33 ya hotuba yangu na Taarifa ya Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kwa Kipindi cha Mwaka 2016/17 hadi 2019/20.

MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2020/21

 

Shabaha na Malengo ya Uchumi Jumla kwa Mwaka 2020/21

 1. Mheshimiwa Spika, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21 umezingatia shabaha kuu za uchumi jumla zifuatazo:

(a)        Ukuaji wa Pato Halisi la Taifa unatarajiwa kupungua kutoka maoteo ya awali ya asilimia 6.9 na kufikia asilimia 5.5 mwaka 2020 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2019. Hii ni kutokana na athari za ugonjwa wa COVID-19 ulioenea katika nchi nyingi ambazo ni washirika wetu wakubwa wa kibiashara;

(b)        Kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki katika wigo wa tarakimu moja kati ya wastani wa asilimia 3 hadi 5 kwa mwaka 2020/21;

(c)        Mapato ya ndani kufikia asilimia 14.7 ya Pato la Taifa mwaka 2020/21 kutoka matarajio ya asilimia 14.0 mwaka 2019/20;

(d)        Matumizi ya Serikali yanatarajiwa kuwa asilimia 22.1 ya Pato la Taifa mwaka 2020/21;

(e)        Nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) kuwa asilimia 2.6 mwaka 2020/21 ikiwa ni chini ya asilimia 3.0 kuendana na makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; na

(f)         Kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango kinachokidhi mahitaji ya uagizaji wa