Home Mchanganyiko MKURUGENZI KAGURUMJULI AWEKA HISTORIA KINONDONI KUKAMILISHA MIRADI YA TAKRIBAN BILIONI 242.8 KWA...

MKURUGENZI KAGURUMJULI AWEKA HISTORIA KINONDONI KUKAMILISHA MIRADI YA TAKRIBAN BILIONI 242.8 KWA KIPINDI CHA MIAKA MITANO, ALAT YAMPA TUZO.

0

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (ALAT), Bwana Elirehemu Kaaya akimkabizi cheti cha shukrani Mkurugenzi Aron Kagurumjuli kutokana na umahiri wa utendaji kazi wake.

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mhe. Benjamini Sita akimkabidhi tuzo ya umahiri Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Ndug. Aron Kagurumjuli kutokana na utendaji kazi wake na kuleta maendeleo makubwa katika Halmashauri hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Daniel Chongolo akimkabidhi tuzo ya umahiri Mstahiki Meya Mhe. Benjamini Sita kwakuongoza vizuri baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo.

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mhe. Benjamini Sita katikati, Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Daniel Chongolo, Mkurugenzi Aron Kagurumjuli wakiwa kwenye kikao cha kuvunja baraza la madiwani la Halmashauri hiyo.

*********************

Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imeweka historia katika suala la utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ile ya kimkakati kwa kipindi cha miaka mitano iliyogharimu takribani shilingi bilioni 242.8 fedha zilizotokana na vyanzo vya mapato ya ndani, Serikali kuu na wadau wengine wa maendeleo.

Taarifa hii imetolewa wakati wa uwasilishaji wa taarifa za utekelezaji wa shughuli za Serikali kwa kipindi cha miaka mitano katika kikao cha mwisho cha Baraza la Madiwani kilichofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa.

Akitoa taarifa hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Ndg.Aron Kagurumjuli amesema Kinondoni imefanikiwa kugusa sekta zote muhimu zinazomuhusu kila mwananchi zikiwemo za uchumi, kisiasa, kijamii pamoja na miradi ya Maendeleo na kuitaja kuwa ni ujenzi na ukarabati wa Vyumba vya Madasara, Vyoo kwa shule za msingi na Sekondari, ununuzi wa madawati kwa shule hizo, ujenzi, ukarabati na upanuzi wa Zahanati , Vituo vya Afya na Hospitali, ujenzi wa miradi ya Masoko na uwekezaji.

Ametaja maeneo mengine kuwa ni miradi ya barabara kwa kiwango cha lami km. 189 kutoka km. 134, kupitia mradi wa DMDP, TARURA, uendelezaji wa miradi ya kilimo na mifugo, ujenzi wa kiwanda cha kuchakata taka na kuzalisha mbolea mboji, hali ya ukusanyaji wa mapato ya ndani na utoaji wa asilimia 10 ya mikopo ya Wanawake, Vijana na Walemavu.

Aidha amefafanua kuwa Halmashauri katika kipindi cha miaka mitano hadi kufikia Juni mwaka huu imetumia kiasi cha shilingi Bil. 3.3 kwa ajili ya kugharamia Elimu ya Msingi bila malipo, Bil. 2.2 Elimu ya Sekondari na hivyo kumpongeza Rais Magufuli kwa kuleta mpango huo.

Mbali na fedha hizo, lakini pia Manispaa imefanikiwa kujenga shule nne za Msingi, ujenzi wa vyumba vya madarasa kutoka 983 Oktoba 2015 hadi kufikia 1147, ukarabati wa vyumba 111, matundu ya choo kutoka 686 hadi 1167, ununuzi wa Madawati kutoka 12,962 hadi kufikia 28,705, Maktaba kutoka 13 hadi 22, majengo ya utawala sita pamoja na ofisi za walimu kutoka 49 hadi 49.

Kwa upande wa shule za Sekondari Manispaa imefanikiwa “kujenga vyumba vya madarasa 48, katika shule mpya za Mzimuni, Kijitonyama, Magomeni, Mbezi juu, Mivumoni, Shule mpya mbili za Alevel, ukarabati wa vyumba 21, Matundu ya choo kutoka 389 hadi 473, Viti na Meza kutoka 19,353 hadi 25,067, Hosteli moja, Nyumba nne, Walimu maabara kutoka 63 hadi 120, majengo ya utawala saba” ameeleza Kagurumjuli.

“ Kwa upande wa Afya tumefanikiwa kujenga Zahanati Nne, vituo vya Afya vitatu ambapo kimoja ni kituo cha Afya Kigogo chenye Ghorofa tano, Hospitali mbili za Ghorofa, upanuzi na ukarabati wa Zahanati sita, Magari ya kubebea wagonjwa matatu, Nyumba za watumishi mbili, Wodi ya Baba, Mama na Mtoto (RCH) 14” ameeleza Kagurumjuli.

Kwa upande wa Masoko, amesema “tumekuwa na miradi ya kimkakati na uwekezaji ambayo ni Soko la kisasa la Magomeni, Tandale, vituo vya ukusanyaji wa mapato sita, uwanja wa mpira Mwenge pamoja na Stendi ya daladala ya Mwenge” ameongeza Kagurumjuli.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Tawala na Serikali za Mitaa (ALAT), Bwana Elirehemu Kaaya akitoa salamu ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kufanya kazi nzuri na kusema kuwa ndio Halmashauri pekee Tanzania iliyoweka historia ya utekelezaji wa miradi yake kwa wakati.

Amesema kuwa Halmashauri hiyo pia imeweka historia ya kuwa na Mkurugenzi mchapa kazi, mwadilifu, msikivu, na mwenyekusimamia maendeleo iliyopelekea kutunukiwa cheti cha shukrani ikiwa ni katika kutambua mchango wake katika utekelezaji wa miradi kwa wakati .

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Mhe. Benjamini Sita amesema kuwa Halmashauri hiyo kupitia Mkurugenzi Kagurumjuli imeweka historia Tanzania nzima kwani imefanya mambo makubwa katika kipindi cha uongozi wao na hivyo kumtunuku tuzo ya kutambua mchango wake.

Amefafanua kuwa pamoja na mambo mengine wanaondoka wakiwa wameacha alama kubwa ambayo imeacha alama na kusema kuwa iwapo watakuwa na nafasi nyingine ya kurudi watafanya mambo makubwa mengine kwa ajili ya kuwaletea maendeleo Wananchi wa Kinondoni.

“Mkurugenzi hongera sana, umefanya mambo makubwa, kwenye uongozi huu tumeshirikiana kama timu, hukujali itikadi za vyama, umewavumilia madiwani wangu, mwisho wa siku umefanya jambo ambalo historia yake tunaiandika leo hii” amesema Mhe. Sita.